Ngasa: Ni matokeo yaleyale ya mawazo ya kivivu ya wachezaji wetu miaka yote

GuDume

JF-Expert Member
Jan 18, 2015
6,652
14,262
MMOJA wa marafiki wa karibu na Mrisho Ngassa aliwahi kunidokeza kuwa mchezaji huyo anaipenda mno klabu ya Yanga na ana mchoro wa timu hiyo kwenye moja ya mikono wake.

Stori iliyonisisimua mwishoni mwa wiki iliyopita ilikuwa ni kiungo huyo mshambuliaji aliyeamua kuvunja mkataba wake na klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini na kurejea nyumbani bila kushawishiwa na yeyote yule tena akiwa na akili zake timamu.

Ngassa amerudi nyumbani ulikolala moyo wake. Inatajwa kilichomfanya avunje mkataba huo ni kile alichokisema timu hiyo haina malengo ya kushinda mataji na yeye amezaliwa mshindi na mara zote amezoea kushinda.

“Ninapenda sana kushinda mataji. Nimezoea kushinda mataji tangu nipo mdogo na nina rekodi ya kushinda mataji. Nimeondoka Free State na nitaenda kujiunga na timu itakayoshinda mataji” alisema Ngassa.

Haya yalikuwa maneno yake. Ukisoma hapa tu inatosha kuufahamu uelewa wake kwenye masuala adimu kama haya. Meneja wa Free State Stars, Rants Makoena, alikuwa akimpenda mno Ngassa na hakutaka aondoke na mara kwa mara alifanya naye vikao vya siri kumshawishi abaki, lakini ilishindikana kwa Ngassa mwenyewe kukubali na mwishowe ameamua kurudi.

Habari kutoka nchini humo zinasema mwezi uliopita kila siku Ngassa alikuwa akijifungia chumbani na kulia kushinikiza kuondoka. Baada ya uongozi kuona hali hiyo ukaamua kuachana nae.

Sababu nyingine iliyotajwa kumkimbiza ni mazoezi ya kocha Denis Lavagne kuwa magumu. Hizi ni sababu nyepesi kwa mchezaji wa daraja lake. Mchezo wa mpira si mchezo wa lelemama.

Ni mchezo wanaocheza watu waliozaliwa katika mazingira magumu. Ni mchezo unaokutoa machozi, jasho na damu kwa wakati mmoja. Kirahisi kabisa na bashasha usoni, Ngassa anasema mazoezi magumu na anashukuru kuona Mungu amemjibu maombi yake ya kuachana na timu hiyo. Loh!

Miaka miwili iliyopita, mmoja ya wachezaji ambao ni marafiki zangu wa karibu alienda nchini humo kwenye klabu ya Bidvest Witts kwa ajili ya majaribio.

Muda mwingi tukiwasiliana alikuwa akijilalamisha kuwa mazoezi magumu na kila siku wanafanya kwa saa 4 bila kupumzika. Sijui rafiki yangu yule hakujua kama amechagua kazi ya mpira anatakiwa kukubaliana na kila hali? Nilimshangaa.

Mchezaji aliyezoea kupewa bia za bure na kuonekana mungu mtu akikatisha korido moja ya klabu za usiku kuelekea nyingine lazima saa nne za mazoezi kwake uwe mtihani mgumu.

Mastaa wetu hawana muda wa kupumzisha miili yao wanapotoka uwanjani. Unaweza kumuona uwanjani wakati wa mechi nyakati za jioni na usiku mkawa pamoja kwenye Dance Floor mkiselebuka. Mchezaji huyu hawezi vumilia hata mazoezi ya saa mbili, atachoka tu.

Mastaa wetu wamekuwa wakipakimbia nje na kurejea nyumbani kwa wingi tena kwa sababu zilezile za siku zote. Watafute waliko Haruna Moshi ‘Boban’, Nizar Khalfan, waulize sababu zilizowafanya waondoke walikokuwa na kurudi nyumbani. Majibu watakayokupa hayatakizana sana na majibu ya Ngassa.

Ngassa, ambaye hati yake ya kusafiria inaonyesha amezaliwa mwaka 1989 kwa maana akiwa na miaka (27), alitakiwa kutumia kipindi hiki kuchota kila fedha ya mpira mpaka pale akili yake itakaposhindwa kufikiri mara mbili na miguu yake itakapopoteza shabaha za kufunga.

Mchezaji wa daraja lake hakutakiwa kurejea nyumbani na kuona kama suluhisho la mazoezi magumu na kukosa mataji. Alitakiwa aendelee kupambana kwa kila hali na mwisho wa siku awe balozi wetu kama ilivyo kwa Mbwana Samatta sasa.

Kama Ngassa ameondoka kwa sababu ya mazoezi kuwa magumu na timu kukosa mipango ya kushinda mataji wachezaji chipukizi nchini wanaomtazama kama kioo chao wanajisikiaje? Moja kwa moja tunavunja mioyo yao wanaposikia stori za namna hii.

Kucheza soka la Afrika kando ya nchi yako kuna ugumu na majaribu mengi ambayo hukatisha tamaa na kushuhudia kundi kubwa la wachezaji wasiojitambua kutazama nyuma na kurudi walikotoka. Ngassa, alitakiwa kuyashinda majaribu haya ili kila mmoja amuimbe kama anavyoimbwa Samatta.

Nwankwo Kanu mara ya kwanza anaenda Ulaya mwaka 1993, katika klabu ya Ajax Amsterdam, alikutana na mazingira tofauti na wazungu wanavyoishi hivyo muda wake mwingi aliutumia kukaa chumbani kwake akijifungia na kupiga simu nyumbani kwao Nigeria.

Licha ya Kanu kujiona yuko katika mazingira ya tofauti, aliamini kwenye kupambana ndio atapata mkate wake wa kila siku. Hakuwa na mawazo ya kurudi alikotoka.

Simshangai sana Ngassa. Haya ndio maisha halisi waliyojichagulia Watanzania walio wengi. Alichokifanya ni kuwakilisha tu akili za walio wengi waliosimama nyuma yake kumtazama.

Licha ya hivyo, Ngassa alitakiwa kufahamu muda haujawahi kuwa rafiki wa mwanadamu. Muda huu anaotumia kuzunguka huku na kule alitakiwa kutulia na kufahamu muda huu haujirudii.

Ukipita unakuwa umepita na kinachobaki huitwa historia. Karibu nyumbani Ngassa.

kwa hisani ya gazeti la raiamwema.
 
Na hapo ndipo penye tatizo kwa wachezaji wetu na soka letu kwa ujumla......

Daima jitihada huleta mafanikio.....na ndio kitu ambacho wachezaji wetu wengi hawataki kukubaliana nacho.....wanataka mambo mazuri lakini kwa njia rahisi.....

Sasa anaposema kuwa amezoea kushinda mataji ndio haya haya ya vodacom ambayo bingwa anafahamika hta kabla ligi haijaanza.......

Angeoonekana mwenye akili timamu walau angecheza japo nusu fainali ya klabu bingwa afrika......sasa kama yeye anasema hivyo na Thomas Ulimwengu asemeje...!!??

Vile vile mawazo ya Ngasa yanawakilisha mawazo ya waTanzania wengi jinsi tulivyo wavivu....wa kufikiri na kutenda.....
 
Hiyo sababu ya mazoezi ameitoa Ngassa mwenyewe?Yaani kabisa amesema mazoezi ni magumu au ni basi tu mawazo ya mwandishi?

Pia kumlaumu sana Ngassa kwa muda huu kwa kurudi nyumbani ni kumuonea tu.Umri umeenda kwa Ngassa.Kiwango chake si cha kimataifa tena.Aliwahi kuwa na kiwango hiko miaka ya nyuma na akachezea bahati.Lawama miaka hiyo ilikuwa sawa lakini si sasa.

Hakuwa na uhakika wa kikosi cha kwanza huko na ameona kuliko kulipasha joto benchi na unri wake wa ukweki ulivyo atashuka kiwango na hata ligi kuu ya vodacom atashindwa kuja kucheza.Kuepuka hilo ameamua kuja bongo kumalizia soka lake ukizingatia hiyo ndo ajira yake.

Kwa sasa kama tunataka watu wa kutuwakilisha vizuri nje ya mipaka sio hawa akina Ngassa tena au akina Msuva au akina Boban.Hawa tayari wamekubali ukweli kuwa wao ni bongo footballers,full stop.

Watu kama akina Kaseke,Hajib,Ndemla nk ndicho kizazi kipya cha soka la bongo.Lawama kwao labda zingesaidia.Sio akina Ngassa.
 
Huyu Ngassa amewafanya nini Jamani......


Mbona KAZIMOTO mmemkalia kimya sana.. Ilhali alienda uarabuni na hakudumu sana....

Vipi yule MGOSI aloyeshindwa kule Congo....

?
 
Alirudi ili apate muda mzuri na wake zake.


Huyu jamaa niliposikia tu kaongeza mke nikajua kumbe hamnazo. Mchezaji huo muda unaupata saa ngapi?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom