Neno La Leo: Ukuta na Daraja..

Neno La Leo: Ukuta na Daraja..

maggid

JF-Expert Member
Joined
Dec 3, 2006
Posts
1,084
Reaction score
1,251
Ndugu zangu,

Yumkini duniani hapa kwa mwanadamu, lililo bora ni kujenga daraja za kuwaunganisha wanadamu kuliko kuta za kuwatenganisha.

Ndilo jukumu nilojipa hapa, maana, mimi ndio wale wa Kizazi Cha Azimio. Hivyo, nimepata bahati ya kuishi na kuyaona na hata kuyafuatilia kwa karibu, matukio ya kisiasa yaliyopelekea nchi yetu kutoka kwenye mfumo wa chama kimoja kwenda vyama vingi.

Kwa muktadha huo, nayaandika haya si kwa maarifa ya kusoma vitabuni tu, au kusimuliwa, bali kuiishi historia yetu kwa miaka ambayo mwenyezi mungu amenijalia.

Ndugu zangu,

Hii ni nchi yetu sote. Nitapenda nibaki kuwa mkweli kwa Nchi yangu niliyozaliwa.

Ningelipenda nisimulie hapa kwa kirefu juu ya uzoefu wangu katika hilo nililobainisha hapo juu. Lakini, nitaanza na makala haya mafupi ili nawe upate muda wa kuyaweka akilini kwa urahisi na kuyatafakari.

Nimeyafuatilia yenye kusemwa kuwa ni maandamano makubwa ya UKUTA yatakayofanyika Septemba Mosi.

Ni jambo la kusikitisha kuwa tuna viongozi wachache wa kisiasa wenye nia ya kuurudisha nyuma mshale wa saa yetu inayotupeleka mbele kama taifa.

Katika wakati tulio nao, dunia kwa ujumla wake imekubwa na changamoto nyingi ikiwamo za kiuchumi na hata matukio ya kiugaidi. Tanzania, kama nchi, tuna bahati kuwa bado tuna amani na utulivu. Ni vitu viwili vya msingi unapotafakari kuijenga nchi.

Hivyo, kama taifa, huu si wakati wa kutanguliza sana maslahi binafsi ya kisiasa, au ya vyama, bali, maslahi mapana ya Nchi yetu tuliyozaliwa na watu wake.

Nionacho, na nilicho na hakika nacho, ni kuwa Septemba Mosi inaweza kuwa na vitu viwili vikubwa;

Mosi, utulivu mkubwa maeneo ya mijini utakaotokana na Watanzania wengi kubaki majumbani. Hivyo, hasara kubwa pia kwa taifa kwa kukosekana na mapato yatokanayo na uzalishaji mali. Wakati huo huo, katika siku hiyo, watu wa Vijijini wataendelea na shughuli zao za kawaida.

Pili, uwepo wa vurugu, si maandamano ya amani wala chenye kufanana na hicho, kati ya polisi na makundi ya vijana wasio na uelewa mpana, wasio na kazi, walio kata tamaa na wasio na cha kupoteza, bali, kwa siku kama hiyo kuwa yaweza kuwa fursa ya kupata chochote chenye kuambatana na wizi wa ngawira. Kuna watu watajeruhiwa na hata kupoteza maisha. Itatoa taswira mbaya ya nchi yetu kwa dunia.

Ukweli katika siku hiyo siyaoni matokeo mengine yenye tija ya kidemokrasia wala kiuchumi kwa nchi yetu. Kwa waliopanga haya watakuwa wamefanikiwa katika moja kubwa; kuliweka taifa letu kwenye hali ya tension kubwa.

Hiki ni kielelezo cha moja ya changamoto ya demokrasia ya vyama vingi katika nchi zetu, pale, viongozi wa vyama ambao miongoni mwao wanashutumiwa pia kwa kuiviongoza vyama vyao kwa mabavu, kwa maana ya uongozi wa - Ki-imla, nao wanaweza kutumia hali ngumu za kiuchumi za nchi, kuhamasisha yale yatakayopelekea vurugu na watu kuumia na hata kupoteza maisha.

Haiwezekani ikawa ni busara na hekima ya mwanasiasa kutumia njia hizo ili kutimiza malengo yake.
Siasa inahusu mijadala endelevu na isiyokoma, na ndio maana ya siasa. Ni wakati sasa, kwa hata wenye ndoto za kuliongoza taifa hili kuwa ni wenye subira na kuruhusu uwepo wa mazungumzo kuliko kuandaa mazingira ya wao wenyewe kuongoza nchi iliyoathiriwa na machafuko, vurugu na kukosekana kwa amani.

Hivyo, neno langu la leo linayapa MAZUNGUMZO nafasi ya kwanza kwa pande zenye kutofautiana ili wafikie kwenye MARIDHIANO.

Duniani hapa walio kwenye mgogoro kamwe hawawezi kuikimbia meza ya Mazungumzo katika kutafuta maridhiano. Maana, hiyo ndio maana ya ukomavu wa kisiasa na kiuongozi.

Na tujitahidi kuyajenga madaraja ya kutuunganisha, kama taifa.

Ni Neno La Leo.

Maggid Mjengwa
0754 678 252
 
Back
Top Bottom