Nape karibu kijiweni tunywe kahawa

Jan 16, 2007
721
176
Nape karibu kijiweni tunywe kahawa


Sauli Giliard​
amka2.gif
WABOBEZI wa tasnia ya habari kila mara wanatuambia kuwa uandishi ni zaidi ya darasa. Kwamba wakati wote tunajifunza mambo mapya, hivyo tujenge utayari kukosolewa na wale tunaowakosoa.
Jumapili iliyopita niliandika kuhoji ilikoishia mikwara ya Rais Jakaya Kikwete, niligusia baadhi ya matukio ya mbwembe za utendaji alizozionesha muda mfupi baada ya kuchaguliwa kipindi cha kwanza (2005-2010).
Tulisikia akitoa maagizo mazito, ziara za kushtukiza, semina elekezi lakini mwishowe hatujaona matunda tuliyotarajia.
Nawashukuru wasomaji wangu kwa tafakari zenu, maoni na ushauri nimevipata lakini kwa ujumla maoni mengi yalieleza namna jamii isivyoridhishwa na utendaji wa Rais Kikwete pamoja na wasaidizi wake.
Kama nilivyosema hapo juu kuwa kazi ya uandishi wa habari kila siku ni kujifunza, basi nitanukuu ujumbe wa mmoja wa wasomaji wangu.
Huyu ni miongoni mwa wengi walioniandikia baada ya kusoma makala yale. Yeye kilichomchefua ni uandishi wangu wa kufupisha jina la Rais Kikwete na kumuita JK.
Hoja yake ina mashiko nami nakubaliana naye kuwa nimejifunza na nimeelewa sitarudia kosa hilo.
Ujumbe wake ulisomeka hivi: “Nadhani kwenye nominal roll alipokuwa shuleni alifahamika kama Jakaya Mrisho Kikwete (JMK) si Jakaya Kikwete Mrisho (JKM). Kujiita JK ni kujifananisha na Baba wa Taifa, hayati Julius Kambarage Nyerere (JKN) na kupata uungwaji mkono hasa vijijini.
Mimi katika hilo sina mjadala kwa leo labda wakati mwingine. Kwa sasa tumtafakari kidogo Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na kama ikiwezekana tumwombe ahamie huku kijiweni tupige majungu yetu.
Muda mrefu tangu kada huyu aanze siasa za kujulikana na kupewa nafasi kwenye vyombo vya habari hasa wakati ule akiusaka uenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), nilighafirika nikamuunga mkono kwa kudhani ana umakini lakini baada kubaini udhaifu wake kifikra na kuchanganua mambo niliamua kubadili msimamo wangu dhidi yake.
Kwa hiyo kazi kubwa niliyokuwa nayo tangu wakati huo ilikuwa ni kudadisi kujua tatizo lake liko wapi. Wahenga wanasema Mungu si Athumani, mara ghafla tu Nape akapewa rungu la kuwa mpiga debe wa chama.
Huku nako wakaniongezea mzigo wa udadisi, nikajiuliza aliyemteua ametumia vigezo gani? Jibu la haraka nikajifariji kuwa yawezekana hakuona vijana makini.
Jumapili iliyopita, kulikuwa na mdahalo kuhusu hali ya upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini, kutaka kujua kwanini tumefika hapo na nini kifanyike. Waandaaji waliwaalika watendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), wizara husika na wabunge wawili vijana, yaani January Makamba (CCM) na Kabwe Zitto (CHADEMA).
Nawashukuru waandaaji wa mdahalo huo kwa kutambua na kupima uwezo wa wasemaji, ingawa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco na wawakilishi wa wizara waliingia mitini lakini walau Makamba na Zitto walitupa majibu tuliyokuwa tukiyataka.
Kimsingi nikirejea kwenye hoja ni kwamba nilitazama mdahalo huo nikiwa nimenuna, kutokana na matamshi ya matusi na kejeli za Nape kwa wananchi wa Mwanza, aliyokuwa amewatukana hadharani kwenye mkutano wake akiwa na viongozi vijana kadhaa wa chama hicho.
Hakika nilipopata habari ile kutoka kwa mwandishi aliyeliwakuwapo mkoani Mwanza kuwa Nape amewatukana wananchi hao eti kwa vile walichagua wabunge na madiwani wa CHADEMA, niliogopa na kughadhabika.
Sikuyashangaa sana matusi yale kwa vile ilikuwa ni mwendelezo wake maana hata hivi karibuni alitoa matusi kama hayo kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani kule Singida, Serengeti, Rorya na hata Manzese jijini Dar es Salaam wakati wa mapokezi ya mbunge wao mpya wa Igunga.
Nilichoudhika ni kuona chama kikongwe kama CCM kinampa uongozi mtu aliyepotoka kimaadili kama Nape, asiyechuja kuwa anaowaporomoshea matusi hata kama ni wapinzani wake kisiasa lakini bado wanabaki kuwa wazazi wake baba na mama, walezi, kaka, dada na wadogo zake.
Nikajiuliza hakuna vijana wengine makini kama hoja ni kuongozwa na vijana? Ama aliyemteua hakujua uwezo wake au CCM ndipo alipofikia hadi viongozi sasa kuanza kutukana wananchi, kuwatisha, kuwanunua kwa kuwahonga mavazi na kuwachochea udini na ukabila?
Mwili ukazizima, nikachefuka na kujikuta naanza kutazama mdahalo wa kina Zitto na January nikiwa sina furaha. Lakini ndani ya dakika kumi baada ya kuwasikiliza vijana hao nikajawa na amani moyoni, kisha nikajiuliza kwanini CCM walimwacha January na kumteua Nape?
January nilimwona ana hekima na uwezo wa kung’amua masuala pamoja na kutoa suluhu ya nini kifanyike. Haya ndiyo wapinzani wanayalalamikia kuwa yamekosekana kwa viongozi wa CCM na serikali yake. Upeo aliouonesha kada huyo Napa hawezi hata kufika theluthi yake.
Iwe ni kwenye makongamano, mahojiano, mdahalo ama mazungumzo na wanahabari, Nape hakuwahi kuwa na fikra za kuchambua na kung’amua mambo kwa mapana kama kina January halafu akatoa suluhisho.
Yeye amekuwa wa kuropoka mambo yasiyo na utafiti, kudandia hoja zisizo na mashiko, mambo ambayo huwa tunaambiwa ni hoja za kwenye vijiwe vya kahawa, ambapo watu hupiga porojo za uongo na ukweli, kucheza drafti, karata na bao ilimradi tu kusogeza muda siku ipite.
Nasikitika kuona viongozi wa juu wa CCM wakishindwa kutambua hazina ya watu makini na waliolelewa kimaadili wenye uwezo wa kukitetea chama kwa hoja za kukubali vile vile changamoto na mawazo ya wengine kama alivyo January, badala yake anapewa uongozi mzito kada mithiri ya Nape, asiyechuja wapi aseme nini na lini.
Kama vipi, Nape tafakari na ukubali kuwa upeo wako wa kujua masuala ni mdogo, njoo kijiweni tujinywee kahawa yetu na tupike majungu muda uende!
Source:TANZANIA DAIMA.
 
Back
Top Bottom