Mzio au aleji (allergy) ni matokeo ya mpambano uliopitiliza kati ya kinga ya mwili na kitu chochote ambacho kwa ujumla huwa hakina madhara kwa mwili pale inapotokea kimeingia ndani ya mwili au kimegusa sehemu fulani ya mwili. Mpambano huu ndio husababisha mtu kuwa na dalili za aleji au mzio. Kwa kawaida kinga ya mwili huulinda mwili dhidi ya vitu mbalimbali hatari kwa afya kama vile vimelea vya magonjwa kama bakteria na virusi, lakini wakati mwingine inaweza kupambana pia na vitu ambavyo havina madhara yeyote kwa mwili ambavyo huitwa allergens. Baadhi ya vitu vinavyosababisha mzio ni pamoja na vumbi, baadhi ya dawa, baadhi ya vyakula, kung'atwa na wadudu kama vile nyuki, aina fulani ya uyoga, vumbi vumbi la maua (pollens) na kadhalika. Kuwa na mzio ni jambo la kawaida. Haishangazi kuona kuna baadhi ya watu wanaopatwa na mafua karibu kila siku au wengine kushindwa kuvaa baadhi ya nguo, vitu kama saa au cheni za dhahabu kwa vile tu huvimba mwili au kuwashwa pindi wanapofanya hivyo. Watu wenye aleji au mzio huwa na hisia zisizo za kawaida za mwili dhidi ya baadhi ya vitu. Mwili unapokumbana na vitu vinavyosababisha aleji mfumo wa kinga ya mwili huzalisha kemikali mbalimbali ikiwemo histamine ambayo hupambana na allergens hizo. Matatizo ya kijenetiki pamoja na hali tofauti tofauti za kimazingira zote zinahusika katika kusababisha mtu kuwa na mzio. Wapo baadhi ya watu ambao hukumbana na mzio pindi wanapokuwa katika mazingira ya joto au baridi, huku wengine hupatwa na mzio pindi wanapopigwa na jua kali. Wakati mwingine, hata msuguano mdogo tu wa ngozi unaweza kuwasababishia baadhi ya watu dalili fulani fulani za mzio. Kwa kawaida, mzio wa aina fulani huwa haurithishwi miongoni mwa wanafamilia. Kwa mfano kama mzazi ana aleji na baridi si lazima watoto wake pia wawe na aleji hiyo hiyo ya baridi ingawa wanaweza kuwa na aina nyingine ya aleji. Uwezekano wa mtoto kupata aleji huongezeka zaidi iwapo wazazi wote wawili wana aleji na vitu fulani fulani na huwa zaidi iwapo mama ndiye mwenye aleji. Nini dalili za mtu mwenye aleji?
Dalili za aleji ni nyingi kwa kutegemea eneo husika la mwili, lakini kwa ujumla kama ni mfumo wa hewa ndiyo ulioguswa, mtu anaweza kuwa na matatizo katika kupumua yaani akapata kikohozi au kubanwa na pumzi, makamasi na kuziba kwa pua, muwasho kwenye pua na koo, au kupumua kwa kutoa sauti kama mtu anayepiga filimbi. Lakini kama macho yataguswa, muhusika huhisi hali ya macho kuchoma, kutiririkwa na machozi na muwasho kwenye macho, macho kuvimba na kuwa mekundu na kadhalika. Iwapo mtu atakula kitu ambacho ana aleji nacho anaweza kuwa na dalili kama vile kuharisha, kichefuchefu, kutapika, kusokotwa au kuumwa na tumbo na hata hali mbaya ya kutishia maisha. Vinavyosababisha mzio au allergens vinapogusa ngozi vinaweza kusababisha ngozi kuwa na mabaka mabaka, kubabuka, kuvimba, muwasho, kuota vipele na malengelenge, michubuko au ngozi kuwa nyekundu. Aleji zinazohusisha mwili mzima zinaweza kuwa na mkusanyiko wa dalili zote tulizozitaja. Wakati mwingine aleji inaweza kushadidisha hali ya baadhi ya watu wenye magonjwa kama ugonjwa wa ngozi wa eczema au pumu na kufanya hali iwe mbaya zaidi.
Vipimo na uchunguzi wa mzio
Mgonjwa ataulizwa kuhusu historia ya tatizo lake, ni lini lilianza na vitu gani humfanya awe hivyo. Aidha tabibu pia atapenda kufahamu kuhusu dalili nyingine zinazoambatana na tatizo linamlomkabili mgonjwa. Baadaye vipimo vya aleji vinaweza kufanyika ili kufahamu hasa ni kitu gani mgonjwa ana aleji nacho na kama kweli dalili alizo nazo zinatokana na aleji au zinatokana na sababu nyingine. Hii ni kwa sababu, kuna baadhi ya mambo yanayoweza kumsababishia mtu dalili zinazofanana kabisa na mtu aliye na aleji ya kitu fulani. Kwa mfano matumizi ya aina fulani ya dawa yanaweza kumsababishia mtu mikwaruzo au michubuko katika ngozi inayofanana na aleji nyingine, au mtu anaweza kuwa na mafua au kikohozi kwa sababu ya maambukizi ya bakteria au virusi na si kwa sababu ya aleji. Kipimo maarufu kabisa cha kutambua aleji kwa mtu ni kipimo cha ngozi (skin testing) ambapo mgonjwa huwekewa baadhi ya vitu vinavyokisiwa kumletea aleji juu ya ngozi yake na kisha ngozi huchomwa kidogo kwa sindano, ili hivyo vitu viweze kuingia ndani ya ngozi na wakati huo daktari akichunguza kama kuna mabadiliko yeyote kama vile uvimbe au ngozi kuwa nyekundu katika eneo lilichomwa. Kipimo cha namna hii hufaa zaidi kwa watoto wadogo kwa vile ni rahisi kufanyika kwao bila usumbufu mkubwa. Aina nyingine ya kipimo cha aleji cha ngozi hufanyika kwa kubandika vitu vinavyohisiwa kuleta mzio kwenye ngozi kinachojulikana kama (patch testing) au kuchoma sindano zenye allergens sehemu ya juu ya ngozi na kuchunguza uwepo wa mabadiliko yeyote katika ngozi.
Vipimo vingine ni pamoja na vipimo vya damu ambavyo huonesha ongezeko la immunoglobin E ambayo huashiria uwepo wa vitu vinavyosababisha aleji, na kipimo cha damu chenye kuonesha ongezeko la eosinophil iwapo kuna aleji, ambayo ni sehemu ya chembe nyeupe za damu. Lakini pia daktari anaweza kumshauri mgonjwa kuepuka baadhi ya vitu hasa dawa au aina fulani za vyakula ili kuona kama atapata nafuu yeyote au kumshauri kutumia baadhi ya vitu anavyohisi vitamletea matatizo ili kuona kama atapata dalili zozote zile.
Je mzio au aleji inatibika?
Njia bora zaidi ya kutibu na kupunguza uwezekano wa kupata aleji ni kutambua kitu au vitu vinavyokusababishia hali hiyo na kuviepuka. Kama ni chakula au dawa au kemikali, epuka kabisa matumizi yake, na kama ni vumbi jitahidi kukaa mbali nalo. Kadhalika shambulio kali la aleji linaweza kusababisha muhusika kulazwa hospitali kwa vile lisipodhibitiwa kifo kinaweza kutokea. Zipo aina mbalimbali za dawa zinazotumika kutibu na kuzuia aleji, kulingana na jinsi daktari atakavyoona inafaa kwa kuzingatia ukali wa tatizo, dalili zake, umri wa mgonjwa pamoja na hali yake ya kiafya kwa ujumla. Dawa hizi ni pamoja na za jamii ya antihistamines, za jamii ya corticosteroids ambazo ni maalumu kwa kutuliza mcharuko mwilini ambazo huwa katika miundo mbalimbali kama vile krimu, matone ya kuweka machoni au masikioni, za kuvuta au kupulizia, sindano au vidonge. Kwa wale wenye mafua na kuziba kwa pua, hushauriwa kutumia dawa zinazosaidia kufungua pua, hata hivyo dawa hizi hazina budi kutumiwa kwa uangalifu hasa kwa watu wenye magonjwa ya shinikizo la damu au moyo. Dawa nyingine ni zile zinazosaidia kuzuia vitu vinavyosababisha aleji. Aina nyingi za aleji hutibika kwa urahisi kwa kutumia dawa. Wapo baadhi ya watu khususan watoto wanaoweza kujenga hali ya aleji dhidi ya aina fulani za vyakula, hali wanayoweza kuendelea nayo mpaka ukubwani. Kwa kawaida, kitu kikimletea mtu aleji utotoni huendelea kumuathiri daima. Madhara ya aleji ni pamoja na kupata shambulio kali ambalo linaweza kusababisha kifo kama matibabu hayatofanywa haraka. Kuna baadhi ya watu ambao, kwa mfano, wakila baadhi ya vyakula huvimba mwili na kushindwa kupumua mpaka kuhitaji kulazwa hospitali na kusaidiwa kupumua kwa mashine. Madhara mengine ni pamoja na shida ya kuvuta pumzi au kushuka kwa shinikizo la damu (kupata shock). Namna ya kujikinga na aleji
Kuna baadhi ya watu wanaonasibisha aleji na itikadi za kichawi suala ambalo si sawa, kwani mzio ni tatizo linalojulikana kitiba na pia kuweza kutibika. Pindi mtu anapopatwa na aina fulani ya aleji, kinga bora ni kukwepa mambo yote yanayoweza kuchochea kutokea kwa shambulizi la aleji. Kama ni chakula, ajitahidi kuepuka aina hiyo ya chakula na kama aleji inasababishwa na dawa, basi muathiriwa aache matumizi ya dawa hizo na pia amueleze daktari wake au muuguzi kuhusu hali hiyo mapema kabla hajapatiwa dawa hizo pindi anapokwenda hospitali kwa matibabu ya matatizo mengine. Wapo watoto wachanga ambao hupatwa na aleji mara tu wanaponyweshwa maziwa ya ng'ombe kwa mara ya kwanza. Hii hutokana na aina fulani ya protini iliyopo kwenye maziwa hayo. Ili kuwakinga wasipatwe na aina hii ya aleji, mama hushauriwa kumnyonyesha mtoto wake angalau kwa miezi
minne ya mwanzo huku akiepuka kumpa maziwa ya ng'ombe katika umri huu. Baadhi ya kinamama hudhani kwamba kubadilisha aina ya chakula wakati wa kunyonyesha kunaweza kusaidia kumuepuesha mtoto na aleji. Hii si kweli kwa kuwa imeonekana kuwa, kitendo hiki hakisaidii kumkinga mtoto dhidi ya mzio.
Uchunguzi umewahi kuonesha kuwa watoto waliozaliwa katika mazingira yenye vumbi na mifugo ambako kuna kiasi kikubwa cha manyoya ya wanyama na vumbi, wana uwezekano mdogo wa kupata aleji ya vitu vya aina hii pindi watakapokuwa wakubwa, ikilinganishwa na wale waliozaliwa katika mazingira yasiyo na hali hizo. Hii ni kwa vile, mazingira ya vumbi huwajengea watoto hawa aina fulani ya kinga dhidi ya aleji, tofauti na wenzao. Hata hivyo, watoto waliohamia katika mazingira haya wakiwa na umri mkubwa wameonekana kuathirika kwa vile wamekosa ile kinga ya utotoni.
Ugonjwa wa Pumu (Bronchial Asthma): Chanzo, dalili na tiba
Utangulizi
Ugonjwa wa pumu ni ugonjwa ambao huathiri sehemu ya kupitisha hewa kwenda kwenye mapafu ya binadamu zinazojulikana kitaalamu kamabronchioles. Mtu mwenye pumu huwa na mcharuko mwili sugu (chronic Inflammation) kwenye mirija yake ya
kupitishia hewa (bronchioles tubes) hali ambayo husababisha kuvimba kwa kuta za mirija hii, kujaa kwa ute mzito (mucus) na kupungua kwa njia ya kupitishia hewa, hali ambayo humfanya muathirika kushindwa kuvuta na kutoa hewa
nje na hivyo kupumua kwa shida sana. Hali hii inaweza kudumu kwa muda mfupi au mrefu kiasi cha kuhitaji tiba ili kumuwezesha mgonjwa kupata nafuu. Kutokana na kuwepo kwa msuguano na uzuiaji wa kupitisha hewa wakati wa kupumua hwa nje, pumu hujulikana pia kama obstructive lung disease . Mtu aliye na pumu, huwa nayo kipindi chote cha maisha yake.
Makundi ya Pumu
Pumu inaweza kugawanywa katika makundi mawili;
Pumu ya ghafla (Acute asthma): Wagonjwa wanaopatwa na kundi hili la pumu huwa na hali ya kawaida katika njia zao za hewa isiyobadilika kati ya shambulizi moja na jingine.
Pumu sugu (Chronic Asthma): Kundi hili la pumu huwa na tabia ya kuwa na njia nyembamba za kupitisha hewa na kadiri jinsi mgonjwa anavyoendelea kupata matukio zaidi ya pumu, njia za hewa huzidi kuwa nyembamba zaidi.
Aina za ugonjwa wa pumu
Bila kujalisha mgonjwa anaingia katika kundi gani, ugonjwa wa pumu unaweza kugawanywa katika aina kuu nne, ambazo ni 1.Pumu inayobadilika(brittle asthma): Kulingana na tabia ya kujirudia rudia kwa matukio ta ugonjwa huu na madhara yake kwa mgonjwa, aina hii ya pumu inaweza kugawanywa zaidi katika aina nyingine mbili, ambazo ni
Aina ya kwanza ya pumu inayobadilika (type 1 brittle asthma) ni pumu yenye tabia ya kuwa na matukio na mashambulizi ya kubadilika kila mara japokuwa mgonjwa anaweza kuwa anapata matibabu kadhaa.
Aina ya pili ya pumu inayobadilika (type 2 brittle asthma) ni pumu ambayo mgonjwa anatokea kupata shambulizi la ghafla (asthmatic attack)wakati hapo awali ugonjwa wake uliweza kuthibitiwa kwa matibabu.
2.Pumu hatari isiyobadilika(status asthmaticus): Hii ni aina ya pumu iliyo hatari zaidi kwa mgonjwa. Pamoja na
matumizi ya dawa kadhaa,zikiwemo vitanua njia za hewa (bronchodilators) na vipoza mcharuko mwili(steroids), mgonjwa wa aina hii ya pumu anaweza asipate nafuu ya haraka, na anaweza kupoteza maisha. 3.Pumu
inayosababishwa na mazoezi (Exercise Induced Asthma): Hali hii husababishwa na ufanyaji wa kupitiliza wa mazoezi ya viungo. Kwa kawaida wakati wa kufanya mazoezi mtu hupumua kwa kutumia pua na kupitia mdomoni. Hata hivyo wakati
mwingine hutokea hewa aivutayo huingia ndani ikiwa haijapozwa vya kutosha puani na hivyo kusababisha ongezeko la mtiririko wa damu katika mishipa inayosambaza damu katika mirija ya kupitisha hewa. Hali hii husababisha kuvimba
kwa kuta za mirija hiyo na muhusika kupata shambulizi la pumu. Aina hii ya pumu yaweza kudhibitiwa na dawa. Inashauriwa sana kwa watu wenye matatizo kama haya kupasha moto misuli kwa mazoezi mepesi (warming up) kabla
ya kuanza mazoezi mazito na ya muda mrefu. 4.Pumu inayosababishwa na aina ya kazi afanyayo muhusika (Occupational Induced Asthma): Wakati fulani, mazingira ya kazi yanaweza kusababisha kutokea kwa pumu hata kwa baadhi ya wafanyakazi wasio na tatizo hili. Mara nyingi aina hii huweza kuwatokea watu wanaofanya kazi kwenye viwanda vya kutengeneza matairi, vigae, rangi, kemikali mbalimbali, mbolea, chuma, unga na mbao.
Pumu husababishwa na nini?
Kuna mambo kadhaa yanayoweza kusababisha kutokea kwa pumu au yanayohusishwa na shambulizi lake. Mambo hayo ni pamoja na
Matatizo ya kinasaba: Matatizo ya kinasaba yamehusishwa na kutokea kwa karibu asilimia 90 ya ugonjwa wa pumu hususani kipindi cha utoto.
Uvutaji wa sigara au tumbaku kipindi cha ujauzito pia unahusishwa na kusababisha pumu kwa mtoto atakayezaliwa.
Maendeleo ya kiuchumi: Ugonjwa wa pumu umeonekana sana kwenye nchi zilizoendelea kiuchumi ikilinganishwa na nchi zenye maendeleo na hali duni ya kiuchumi.
Magonjwa ya mapafu kama bronchitis
Vyanzo vya mzio (allergens)kama vile vumbi, vinyesi vya wanyama na baadhi ya vyakula.
Uchafuzi wa mazingira kama moshi na baadhi ya harufu kali.
Baadhi ya kemikali kwenye maeneo ya kazi hasa kwenye viwanda kama vya rangi, chuma, sementi na vigae.
Baadhi ya wagonjwa wanaotumia dawa za kushusha shinikizo la damu zilizo katika jamii ya beta-blockers kama vile propanolol wapo katika hatari ya kupata shambulio la ugonjwa wa pumu.
Magonjwa kwenye mfumo wa kupumua yasabishwayo na baadhi ya virusi na bakteria kama vile rhinovirus, Chlamydia pneumonia auBordetella pertusis.
Matumizi ya mapema sana ya baadhi ya dawa hasa antibiotiki kwa watoto yanaweza kubadilisha mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa na hivyo kumfanya mtoto kuwa katika hatari ya kupata pumu.
Ongezeko la msongo wa mawazo huweza kusababisha pumu na matatizo katika mfumo wa upumuaji
Upasuaji wakati wa kujifungua (caesarian section): Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa kujifungua kwa njia ya upasuaji huongeza uwezekano wa kupata pumu kwa vile njia hiyo yaweza kuathiri mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya maradhi.
Vihatarishi vya ugonjwa wa pumu
Uwezekano wa kupata ugonjwa wa pumu huongezeka iwapo mtu
Atakuwa na magonjwa ya mzio kama vile magonjwa ya ngozi (eczema) yasababishwayo na aina fulani ya vumbi au homa (hay fever)
Atavuta chavu (pollen) kutoka kwenye maua au miti
Atajihusisha na uvutaji sigara
Ana historia ya ugonjwa wa pumu au mzio kwenye familia
Utumiaji wa dawa aina ya aspirin
Ana msongo wa mawazo
Ana uambukizi wa magonjwa ya virusi kamarhinovirus
Mazoezi
Anaishi sehemu zenye baridi
Ana matatizo katika njia yake ya chakula (Gastroesophageal reflux disease au GERD)
Dalili za ugonjwa wa pumu
Dalili za ugonjwa wa pumu ni pamoja na
Kuishiwa na pumzi na kupumua kwa shida (shortness of breath)
Kutoa sauti kama mtu anayepiga miluzi wakati wa kupumua (wheezing)
Kukohoa sana (chronic cough) hasa nyakati za usiku au asubuhi. Aidha kikohozi huambatana na kutoa makohozi mazito, yasiyo na rangi au yenye rangi ya njano.
Kubana kwa kifua.
Kwa mtu aliyepata shambulizi kubwa la pumu (severe asthmatic attack) anaweza kushindwa kuzungumza na pia kuwa na hali kama ya kuchanganyikiwa.
Vipimo na Uchunguzi
Pamoja na daktari kutaka kufahamu historia ya mgonjwa, anaweza pia kuamua kufanya vipimo vifuatavyo ambavyo vitamsaidia kufahamu chanzo na madhara ya ugonjwa wa pumu kwa muathirika.
Kipimo cha damu (complete blood count) msisitizo ukiwa kwenye wingi wa seli za damu aina ya eosinophils ambazo uhusika na kuwepo kwa shambulio la mzio.
Kipimo cha kuchunguza uwezo wa mgonjwa kutoa hewa nje mara baada ya kuivuta (spirometery). Aina hii ya uchunguzi hufanyika kabla ya mgonjwa kupewa dawa kwa kutumia nebulizer.
Kipimo cha kuchunguza kiwango cha hewa ya oksijeni kilichopo kwenye damu ya mgonjwa (oximetry).
Kipimo cha kuchunguza uwezo wa mgonjwa kupumua hewa nje wakati wa shambulizi la pumu (Peak flow meter).
X-ray ya kifua kwa ajili ya kutofautisha pumu na magonjwa mengine yenye dalili za kufanana kama vile ugonjwa wa moyo (congestive heart failure), magonjwa sugu ya kuziba kwa njia za hewa (COPD kama vile chronic bronchitis na emphysema) na magonjwa mengine ya kuzaliwa kama vile cystic fibrosis.
Kipimo cha mzio cha ngozi(skin allergy test) kwa ajili ya kutambua aina ya mzio inayomsababishia mgonjwa shambulizi la pumu.
Matibabu ya Pumu
Kwa ujumla matibabu ya pumu hujumuisha kuepuka visababishi vya ugonjwa huu na matumizi ya madawa kwa walio na hali mbaya. Aidha, kwa wanaopata ugonjwa huu kwa sababu ya msongo wa mawazo hupewa ushauri nasaha kwa ajili ya
kusaidia kutatua matatizo yanayowakabili. Vilevile inashauriwa kwa wenye tatizo hili, kuwa na dawa karibu muda wote kwa ajili ya matumizi pindi shambulizi litakapotokea. Pia inashauriwa sana kuepuka mazingira na hali za baridi ambazo
huweza kuchochea kutokea kwa shambulio la ugonjwa huu. Matibabu ya kutumia dawa hujumuisha matumizi ya dawa za kusaidia kupunguza na kuondoa makohozi (expectorants), dawa zinazosaidia kutanua mirija ya hewa (bronchodilators), dawa za kuondoa mcharuko mwili kama vile cortisone ya drip (hasa wakati wa dharura) au nebulizer, na dawa za kuzuia
mzio (antihistamine drugs). Hata hivyo, kuna matibabu ya ziada kulingana na hali ya mgonjwa pamoja na kundi na aina ya pumu inayomuathiri mgonjwa. Kwa wagonjwa wenye pumu ya ghafla na wenye hali mbaya (acute asthma) matibabu hujumuisha matumizi ya dawa za kutanua mirija ya hewa (bronchodilators) pamoja na kuongezewa hewa ya
oksijeni, dawa za kutuliza mcharuko mwili (steroids) pamoja na dawa za kutuliza kukakamaa kwa misuli ya mwili (intravenous muscle relaxants). Aidha kwa vile mara nyingi shambulizi hili laweza kuwa la hatari sana, mgonjwa hulazwa
hospitali na huongezewa hewa ya oksijeni, na kwa wagonjwa wasioweza kupumua kabisa, husaidiwa kufanya hivyo kwa kutumia mashine maalum iitwayo (mechanical ventilator). Kwa wagonjwa wenye pumu sugu, jambo la muhimu ni
kuepqka visa"abishi vya pumu na kuendelea na matumizi ya dawa zinazosaidia katika kutanua mirija ya hewa. Kwa wagonjwa wanaopata mashambulzi ya mara kwa mara wanaweza kushauriwa na daktari kutumia dawa kadhaa zikiwemo zile zinazopunguza mcharuko mwili (mast cell inhibitors, inhaled steroids au oral steroids), pamoja na dawa za
kutuliza kukakamaa kwa misuli ya mwili (muscle relaxants). Aidha ni vema pia kutibiwa na kuthibiti kutokea kwa magonjwa yote yahusuyo mfumo wa hewa. Matumizi ya chanjo ya magonjwa kama influenza na pneumococcal pneumonia nayo husaidia sana katika uthibiti wa kutokea kwa pumu. Ni vema pia kuepuka matumizi ya dawa za jamii ya beta-blockers kwa wagonjwa wenye shinikizo la damu na ambao pia wana pumu.
Nini madhara ya pumu kwa mama wajawazito?
Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa takribani theluthi moja ya wajawazito wenye pumu hupata nafuu kipindi cha ujauzito, theluthi nyingine hupata matatizo kipindi hiki na theluthi iliyobakia huwa na hali ya kawaida kama kabla ya ujauzito.
Kwa kawaida dalili za pumu hujirudia kama awali miezi mitatu baada ya kujifungua. Dalili za pumu kwa mjamzito zinaweza kuwa mbaya zaidi kuanzia wiki ya 24-36 (mwezi wa sita mpaka wa nane). Ni mara chache sana mjamzito
anapata shambulizi la pumu wakati wa kujifungua. Inakisiwa kuwa, ni asilimia 10 tu ya wajawazito wenye pumu wanaopata shambulizi la pumu wakati wa kujifungua. Baadhi ya dawa zinazotumika wakati wa ujauzito na baada ya
kujifungua huongeza madhara ya pumu, hivyo ni vizuri kumueleza daktari kwamba una pumu kabla ya kupewa dawa. Aidha na si vyema kunywa dawa kwa mazoea. Wanawake wenye pumu isiyoweza kuthibitiwa kipindi cha ujauzito
hupata madhara ya kuzaa mtoto njiti (premature baby), kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo, kifafa cha mimba, shinikizo la damu (Hypertension), na iwapo atapata shambulizi hatari wakati wa ujauzito mtoto anaweza kufa kwa kukosa hewa ya oksijeni.
===================================
Ugonjwa wa Pumu ( Athma kwa watoto
===================================
Nini maana ya Pumu?
Pumu ni hali ambayo huathiri njia za hewa, njia hizi za hewa pia huitwa mirija ya kupumulia. Mirija hii huanzia kwenye njia ya hewa(trachea) hadi kwenye mapafu.
Mchakato wa kupumua kwa watoto walio wengi ni rahisi : Watoto huingiza hewa kupitia puani au mdomoni na hewa huingia kwenye njia ya hewa(trachea) na kuelekea kwenye mapafu. Lakini Kwa watoto wenye pumu, hupumua Kwa shida Kwa sababu njia ya hewa hushindwa kupitisha hewa kwa sababu ya njia yao kuwa imehathiriwa na hali ya pumu.
Shambulio la pumu (Asthma attack) ni nini?
Hii ni hali ambayo hutokea wakati njia ya hewa inapo vimba na kuwa nyembamba na inakuwa vigumu kwa hewa kuingia na kutoka kwenye mapafu. Wakati mwingine njia za hewa zinapokuwa zimevimba hutoa majimaji mfano wa makamasi, hali ambayo husababisha mchakato mzima wa mabadlishano ya hewa katika mapafu kuwa mgumu na hii hali ndo inapelekea tatizo zima la mtotoanapo patwa na pumu kushindwa kupumua vizuri.
Wakati ugonjwa huu unaanza, upumuaji kwa mtoto unaweza kuwa wa kawaida na kuonekana kama vile hakuna tatizo, Lakini kipindi ugonjwa unapoanza, unaweza kuhisi kwamba mtu anapumua kupitia kwenye mrija. Mtoto mwenye pumu anaweza kutoa mlio kama wa filimbi (anapopumua), kukohoa, na kusikia kifua kubana.
Wakati shambulio la ugonjwa wa pumu(asthma attack), hali inaweza kuwa mbaya zaidi kama mtoto hatatumia dawa sahii za pumu. Baada ya kutumia dawa na kupata matibau sahii wakati wa shambulio la ugonjwa wa pumu, njia ya hewa mara nyingi hurudia hali yake ya kawaida, ingawa inaweza kuchukua muda mrefu kidogo wakati mwingine.
Pumu huwapata watu gani?
Pumu ni ugonjwa ambao huwapata watu wengi zaidi ya unavyo weza kufikiri.Karibia watoto milioni sita nchini marekani wanaumwa ugonjwa wa pumu(Hatujui hapa kwetu Tanzania ni idadi gani?).Ugonjwa wa pumu humpata mtoto mmoja hadi wawili katika kila watoto 10 kwa marekani. Hii ina maana kwamba kama una watoto 20 darasani, watoto 2-4 kati yao wanaweza kuwa na ugonjwa wa pumu. Ugonjwa wa pumu unaweza kumshika mtu katika umri wowote- kuanzia mtoto mchanga hadi mtu mzima-lakini huwashika zaidi watoto wenye umri wa kwenda shule(kuanzia miaka sita na kuendelea)
Hakuna anayejua kwa uhakika kwa nini ugonjwa huu unampata mtu mmoja na kuacha mwingine, lakini tunajua kwamba ugonjwa wa pumu unatokea ndani ya familia zetu. Hii ina maana kwamba kama mtoto ana pumu, yeye pia anaweza kuwa na mzazi, ndugu, mjomba au jamaa mwingine mwenye pumu au alikuwa na ugonjwa huu wakati bado mtoto.
Ugonjwa wa pumu unapoanza,huonyesha kama vile ni mafua,ambayo huambatana na kikohozi chenye kutoa mlio wa filimbi,lakini ugonjwa wa pumu siyo wa kuambukizwa. Huwezi kuambukizwa Kama unavyopata mafua
Ni sababbu zipi zinazopelekea Kupata shambulio la ugonjwa wa pumu (Asthma attack)?
Visababishi hutofautiana kutoka mtoto mmoja hadi mwingine. Sababu zipo nyingi.Baadhi ya watoto huwa na mzio(allergy), kwa vile vitu ambavyo huathiri njia ya hewa. Mara nyingi vitu vinavyoleta mzio kwa watoto wenye pumu ni vijidudu vidogo jamii ya mchwa vinavyopatikana kwenye vumbi, harufu mbaya (kama ulikuwa karibu na dimbwi na kuvuta harufu hiyo), mbelewele(pollen) kutoka mitini, majani na kwenye magugu.
Watoto wengi hupata shambulio la pumu wanapokuwa karibu na wanyama wenye manyoya kama Paka na mbwa,baadhi watoto wanapovuta hewa iliyochanganyika na chembechembe za manyoya hawa wanaweza pata shambulio la pumu.
Visababishi vingine ni pamoja na marashi(perfumes), vumbi la chaki, na uvutaji wa sigara. Uvutaji wa sigara sio mzuri hasa kwa mtu mwenye pumu.
Wakati mwingine maambukizi mbalimbali yanaweza kusababisha kulipuka kwa ugonjwa wa pumu,maradhi kama mafua, Kwa baadhi ya watoto, hali ya hewa yenye baridi inaweza kusababisha kulipuka kwa ugonjwa huo,baadhi ya watoto hupatwa na matatizo ya pumu wanapokuwa wanafanya mazoezi,hii ni aina ya pumu inayosababishwa na mazoezi.
Jinsi gani unaweza kutibu ugonjwa wa pumu kwa watoto?
Watoto wenye ugonjwa wa pumu wanatakiwa kujaribu kuepuka visababishi vyote vinavyoweza kuwasababishia shambulio la hewa.Ingawa kuna baadhi ya visababishi kama vumbi la chaki ni vigumu kuviepuka katika mzaizngira yetu hasa shuleni,lakini mtoto,wazazi na walimu wajaribu kuwasaidia watoto wenye matatizo haya.
Sura ya ugonjwa wa pumu hutofautiana kutoka kwa mtoto mmoja hadi mwingine, hivyo kuna dawa mbalimbali za kutibu ugonjwa wa pumu,na matibabu haya hutofautiana kati ya mtoto mmoja na mwingine hii ni baada yake daktari kujaribu kufuatilia sababu zilizopelekea ugonjwa huo, ni kwa kasi gani ugonjwa umetokea, na kiwango cha madhara ya ugonjwa huo. Hapo ndipo ataamua tiba ipi itakuwa sahii na bora kwa mtoto.
Baadhi ya watoto wanatakiwa wameze dawa za pumu mara kwa mara punde wanapopata ugonjwa huu. Hii huitwa dawa ya dharura kwa sababu hufanya kazi ya kufungua njia ya hewa ili mtu aweze kupumua. Watoto wengine wanatakiwa kutumia dawa za kudhibiti ugonjwa wa pumu kila siku,Dawa hizi huzuia shambulio la ugonjwa(asthma attack) kutokea.Kwa hiyo matibabu ya Pumu yanatofautina kutoka mtoto mmoja na mwingine.
Kwa watoto walio wengi ugonjwa wa pumu hupona au hupata nafuu wanapokua wakubwa. Baadhi ya madaktari wanadai kwamba hii hutokea kwa sababu, njia ya hewa hupanuka kadri mtoto anavyokua mkubwa. Njia ya hewa inapopanuka, hewa huingia na kutoka kiurahisi
Baadhi ya watu wazima hupata ugonjwa wa pumu, lakini hii haiwasumbui.Wanariadha wengi katika mbio za olimpiki na magwiji wengine wa michezo wanaweza kuendelea na michezo hata wanapokuwa na ugonjwa wa pumu.
UJUMBE WA KUPELEKA NYUMBANI:
Mzazi au mlezi anayeona mtoto mwenye dalili za ugonjwa wa pumu kama nilivyouelezea hapo juu kitu cha kwanza cha kufanya ni kumwaisha Katika kituo chochote cha Afya au Hospitali iliyo karibu nae.
Na kwa wale watoto walikwisha gundulika tayari na ugonjwa huu wa Pumu ni kuhakikisha wanafuta masharti yote ya Matibabu ili kuzuia shambulio la ugonjwa huu.
Mtoto anayejua mapema kwamba kuna vitu vinamletea madhara katika njia ya hewa au sababu nyingine anaweza kutumia dawa mapema zitakazosaidia kufanya njia ya hewa iendelee kuwa wazi.Mtoto ambaye hupata pumu anapofanya mazoezi anaweza kutumia dawa kabla ya kufanya mazoezi ili waweze kumaliza mbio au michezo vizuri.
Kwa watoto walio wengi ugonjwa wa pumu hupona au hupata nafuu wanapokua wakubwa. Baadhi ya madaktari wanadai kwamba hii hutokea kwa sababu, njia ya hewa hupanuka kadri mtoto anavyokua mkubwa. Njia ya hewa inapopanuka, hewa huingia na kutoka kiurahisi
Baadhi ya watu wazima hupata ugonjwa wa pumu, lakini hii haiwasumbui.Wanariadha wengi katika mbio za olimpiki na magwiji wengine wa michezo wanaweza kuendelea na michezo hata wanapokuwa na ugonjwa wa pumu.
UGONJWA WA PNEUMONIA NI NINI? CHANZO NA TIBA YA PNEUMONIA
Katika ukurasa huu tutauzungumzia ugonjwa ambao huathiri watu wengi sana, wa rika zote, ugonjwa unashambulia mapafu uitwao pneumonia. Pneumonia ni ugonjwa unaoweza kuwa wa kawaida au unaoweza kuwa mbaya hadi kusababisha kifo. Ni ugonjwa mbaya kwa makundi ya watoto wadogo na hasa vichanga vyenye umri wa chini ya miaka miwili, kwa wazee wenye umri unaozidi miaka 65, na kwa watu wenye matatizo ya kiafya na wenye upungufu wa kinga za mwili. Tutaanza kwanza kwa kujua pneumonia ni nini na baadaye kujadli dalili za pneumonia na tiba zake.
Pneumonia ni ugonjwa unaoongoza duniani kwa kusababisha vifo kwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano. Asilimia 50 ya wagonjwa wa pneumonia hushambuliwa na virusi na hawapati madhara makubwa kama yale wanayopata wagonjwa wa pneumonia walioshambuliwa na bacteria. Ugonjwa wa pneumonia unaweza kuzuilika kwa kupata chanjo na hutibika kwa kutumia antibiotics, antiviral drugs na dawa mahsusi kwa ugonjwa huu.
Pneumonia Ni Nini?
Pneumonia ni ugonjwa unaoshambulia vifuko vya hewa kwenye pafu moja au yote mawili. Vifuko hivi huweza kujaa maji au usaha na kusababibisha kikohozi kinachotoa uchafu unaotoka kwenye mapafu, homa na kupata shida katika kupumua. Vijidudu wa aina nyingi wanaweza kuhusika katika ushambuliaji wa mapafu hayo. Mara nyingi pneumonia hutokana na mashambulizi ya bacteria, virusi, fangasi (fungi) au vijiumbe wengine tegemezi (parasites).
Mtu anapovuta hewa yenye wadudu hawa wadogo (germs) wanaosababisha maradhi, wadudu hawa huingia kwenye mapafu na
kama kinga za mwili za mtu huyu zitashindwa kuwazuia, wadudu hawa hukaa kwenye vifuko vidogo (alveoli) vya kwenye mapafu na kuanza kuzaliana. Mwili utakapopeleka chembechembe nyeupe za damu kupambana na wadudu hawa, vifuko hivi hujaa majimaji na usaha na kusababisha pneumonia.
Nini Chanzo Cha Pneumonia
Pneumonia husababishwa na bacteria, virusi, fangasi na vyanzo vingine. Hapa chini tutaona baadhi ya vyanzo hivi kwa undani zaidi:
Bacterial Pneumonia
Wagonjwa wengi wa pneumonia hushambuliwa na bacteria aitwaye Streptococcus pneumoniae. Watu wanaougua kwa muda mrefu ugonjwa wa obstructive pulmonary disease (COPD) au wale wanaotumia pombe kwa wingi hupata pneumonia kutokana
na bacteria waitwao Klebsiella pneumoniae na Hemophilus influenzae. Baadhi ya wagonjwa wengine hupata ugonjwa huu
kutokana na bacteria aitwaye Mycoplasma pneumoniae.
Maji yasiyo salama yakinywewa au kutumika ndani ya viyoyozi husababisha pneumonia kutokana na bacteria aitwaye bacterium Legionella pneumoniae. Kuna aina ya pneumonia, pneumocystis carinii pneumonia, ambayo hushambulia mapafu yote mawili inayotokana na mwili kuwa na upungufu wa kinga unaotokana na magonjwa ya kansa au UKIMWI au kutibiwa rheumatoid arthritis na baadhi ya dawa.
Viral Pneumonia
Hii ni pneumonia inayotokana na virusi na ambayo haisikii tiba za antibiotics. Baadhi ya virusi wa aini hii ni Adenoviruses, rhinovirus, influenza virus (flu), respiratory syncytial virus (RSV), na parainfluenza virus.
Fungal Pneumonia
Aina hii ya pneumonia husababishwa na fangasi wa aina za histoplasmosis, coccidiomycosis, blastomycosis, aspergillosis, na cryptococcosis.
Nosocomial Pneumonia
Viumbe wadogo walioishi kwenye mazingira ya antibiotics kwa muda mrefu hujijengea uwezo wa kuhimili dawa hizo na pindi wakiingia katika mapafu husababisha nosocomial pneumonia. Bacteria wa aina hii hupatikana kwenye majumba ya kuuguzia wagonjwa na katika hospitali.
Mazingira Yanayosababisha Pneumonia
Mazingira au hali zifuatazo zinaweza kusababbisha ugonjwa pneumonia:
Moshi
Unywaji wa pombe wa kukithiri
Magonjwa kama chronic obstructive pulmonary disease (COPD), emphysema, pumu, au UKIMWI.
Umri pungufu ya mwaka mmoja au zaidi ya miaka 65.
Kuwa na kinga nogo za mwili
Utumiaji wa dawa za magonjwa, gastroesophageal reflux disease (GERD).
Kushambuliwa na kifua na mafua
Kuwa na lishe duni
Kulazwa kwenye hospitali kwenye kitenge cha uangalizi maalumu (Intensive care unit).
Kuwezepo kwenye mazingira ya kemikali za aina fulani au uchafuzi wa hewa.
Kuwa mwenye asili ya Alaska au koo fulani za kimarekani
Kuwa nanmatatizo yanayoruhusu chakula kutoka tumboni kuingia kwenye mapafu
Dalili Za Pneumonia
Pneumonia inayotokana na bacteria huonyesha dalili mapema zaidi kuliko ile inayotokana na virusi. Watu wengi wanaopata ugonjwa huu huanza kwa kushikwa na kifua au mafua, kisha kupata homa kali inayoambatana na kikohozi chenye kutoa makohozi. Pamoja na kwamba dalili za pneumonia zinaweza kuwa za aina tofauti kulingana na chanzo chache, wagonjwa wengi huona dalili zifuatazo:
. Kukohoa
. Makohozi ya rangi ya kahawia au kijani
. Homa
. Kuhema kwaharaka na kukosa pumzi
. Kutetemeka
. Maumivu kifuani hasa unapovuta pumzi
. Mapigo ya moyo kwenda mbio
. Uchovu na udhaifu wa mwili
. Kichefuchefu na kutapika
. Kuharisha
. Kutokwa jasho
. Kichwa kuuma
. Maumivu ya misuli
. Kuchanganyikiwa
Tiba Ya Pneumonia
Tiba itakayotolewa kwa mgonjwa wa pneumonia itategemea aina ya pneumonia aliyo nayo na hali aliyonayo mgonjwa. Pneumonia inayotokana na bacteria hutibiwa na antibiotics wakati pneumonia zinazotokana na virusi hutibiwa kwa kumpa mgonjwa muda wa kupumzika na kumpa vinywaji kwa wingi. Pneumonia zinazotokana na fangasi hutibiwa na dawa za kutibu fangasi.
Dawa nyingine hutolewa ili kumsaidia mgonjwa kupunguza homa, kuondoa maumivu ya kichwa, kuondoa mafua na kikohozi. Ni muhimu sana kwa mgonjwa wa pneumonia kupata muda wa kupumzika na kupata usingizi. Mgonjwa hutakiwa kutumia
vinywaji kwa wingi sana.
Mgonjwa hulazwa hospitali pale hali yake inapokuwa mbaya au pale inapobainika kuwa ana upungufu wa kinga za mwili. Kwenye hospitali mgonjwa atapewa antibiotics kupitia mishipa ya damu na wakati mwingine kupewa msaada wa kupumua kupitia mitungi ya oksijeni
Ukiwa na Shida yoyote ile
Usipo pona kwa Dawa za Hospitali nitafute mimi nipate kukutibia upate kupona ukihitaji matibabu yangu
Unaweza kunitafuta kwa Mawasiliano Herbalist Dr. MziziMkavu Email barua ya pepe. fewgoodman@hotmail.com What's App na Viber +905344508169
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.