Nchi hii usipokomaa unaweza kujikuta umelezwa ndani kwa mwezi mmoja ilhali kesi yenyewe ni ya kipuuzi, pengine ya kukanyaga nyanya gengeni. Wananchi wanapaswa kuamka na kujua haki na wajibu wao. Wanapaswa kusoma vitabu vya sheria vya kawaida kabisa, tena vilivyoandikwa kwa kiswahili. Isitoshe, pale polisi huwa kuna maandishi yanayoonesha haki na wajibu wa raia na askari.
Wananchi wengi wamekuwa waoga kwa sababu ya hulka ya polisi ya kuwatisha watu. Tena bahati mbaya ukifika polisi ukiwa umevaa kapensi au nguo kuukuu, utasumbuliwa sana.
Wananchi amkeni. Hakuna aliyesema dhamana lazima itolewe mchana. Hata usiku dhamana inatolewa, alimradi tu suala lenyewe liwe linakubalika kisheria. Tukisubiri polisi watuonee huruma, haki ya Mungu tutazidi kuumia. Tuwaunge mkono viongozi wa polisi waungwana watenda haki kwa kuhakikisha sisi wananchi wenyewe tunasimama imara kudai haki zetu kwa mujibu wa sheria na kwa ustaarabu.