Nani anajali Mwigulu akiivuruga nchi?

Tulimumu

JF-Expert Member
Mar 11, 2013
14,305
12,969
SIJUI waliompa nafasi aliyonayo walizingatia vigezo gani. Naambiwa ni msomi "mzuri" tu aliyehitumu kile chuo kikongwe pale Mlimani. Chuo ambacho waliosoma enzi hizo, wakishindana kufuga ndevu kama hayati Samora Machel wa Msumbiji ama wakichana staili ya nywele kwa kuweka barabara kushoto pembeni kama alivyofanya hayati Dk. Milton Obote wa Uganda.

Kwamba huyu ambaye sasa analilia na kuimba kila siku akitaja chama kile kinachomkosesha raha na akielea hata kusahau jina la chama chake, naye alikanyaga mitaa ya ile milima ambayo wale wa zamani walitembea huku wakiimba kale kawimbo kalikokuwa maarufu wakijaa matumaini mapya baada ya kuhitimu kitabu; "Niko kilimani naranda, nangojea pijo kupanda, Mwalimu Nyerere kasema, vijana fungeni mikanda".

Sina uhakika kama mwana-Mlimani huyu wa sasa anajua kuwa sehemu hiyo ndilo lilikuwa "jiko' la fikra nzito za kimapinduzi zilizojaa uzalendo ambapo wasomi walisimama katika ukweli, wakiona soni kuropoka maneno yanayofanana na mtu ambaye hakuona darasa.

Narudia tena, sina nia ya kuwashushia hadhi na heshima vizito wa chama changu cha Mapinduzi, lakini nasita kukaa kimya hasa kwa maneno na vitendo vinavyofanywa na mtu aliyejitambulisha kwa Watanzania akitaka tumwite Mwiiingulu Lameck wa Nchemba.

Kijana huyu ambaye ameaminiwa hadi kupewa cheo kikubwa cha kiutendaji makao makuu CCM kwa kweli bila chuki wala husuda hafanani, haelekei wala hana haiba ya kushika cheo hicho! Hajali waliomfikisha hapo, hajijali yeye mwenyewe na mbaya zaidi hajali watu wengine ambao kwa mujibu wa dini yake wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kwa muda sasa Mwigulu katika sijui niziite ziara zake ama nini, anaongozana na kijana mmoja toka Singida ambaye ameharibika uso kutokana na majeraha ya kuunguzwa na tindikali wakati wa kampeni za uchaguzi mkoani humo. Mwigulu amekuwa akimpandisha kijana huyo katika majukwaa sio kwamba anamnadi kwa wapiga kura ili wamchague, bali kuwaonesha kwamba upinzani na hasa CHADEMA ni magaidi, hivyo wasijaribu hata kuwaza kuwapa uongozi hata wa serikali ya mtaa!

Mwigulu anapaza sauti kwa nguvu kama desturi yake akidai kwamba kama CHADEMA wameweza kutenda ukatili kiasi hicho, hapana shaka kwamba wakipewa nchi wataangamiza maisha ya wengi maana kwao uhai wa mtu si kitu cha maana; ni takataka. Katika hali ya kawaida ya mtu anayejali utu wa mwingine, haiingii akilini kamwe kutumia ulemavu wa mwingine kwa faida yako; kupata ulaji wako bila kujali kama huo ni udhalilishaji mkubwa.

Mwigulu anaishambulia CHADEMA kana kwamba ana ushahidi na vyombo vya sheria vimethibitisha hayo! Hivi akiburuzwa mahakamani akatakiwa kutaja majina ya hao wana-CHADEMA waliohusika ataweza? Sijawa wakili wala sijatumwa kuwa msemaji wa CHADEMA, bali kama Mtanzania makini ninayejali kwanza utaifa alafu ndo hayo mambo ya vyama.

Yaani Naibu Katibu Mkuu wa chama maarufu duniani anaeneza sera za pumba za kutangaza uhasama kwa maumivu ya mwingine! Naibu Katibu mkuu wa chama tawala anakosa jema la kuwashawishi wapiga kura hadi afanye anavyofanya sasa! Masikini kijana wa watu, naye anakubali kugeuzwa sanamu la kutundikia nguo dukani badala ya kugomea ujinga huo. Yaani shauri ya njaa, anakubali kutumiwa kama ngamia wa jangwani.

Hajali ikiwa anadhalilishwa na hajui siku zaja, naam tena zakimbia kwa kasi kabla jimbi hajawika atatemwa kama ganda la muwa. Hapo ndo atakapojua maana ya usemi wa ‘CCM ina wenyewe'. Chezea CCM weye! Mwanasiasa huyu sijui kasomea chuo gani toba maana anatoa matamshi kama kipofu anayepapasa apate pa kukanyaga. Hajali matokeo ya kile anachotamka. Hajali zaidi ya tumbo lake na kwakweli huyu sio CCM maana tulikotoka hatukuwa na mtu aina ya Mwigulu.

Atoke wapi? Nani apitishe jina la mtu anayetaja majina ya watu kuwa magaidi, tena akienda mbali zaidi na kubwata ana jambo zito sana na tumwombee kwa Mungu ajaliwe kuliseme siku moja! Jamani jambo zito na la hatari analo yeye, na atalisema siku atakapotaka! CCM woyeeee! Polisi, usalama na wengineo hawaaminiki tena kuwapa siri nzito na ya hatari isipokuwa akae nayo mtu mmoja; Mwiguluuuu! Haya nayo ni moja ya maajabu ya dunia. Kama ni mkweli na ana uchungu na maisha ya watu, mbona haendi kufukua makaburi mawili ya makada wa CHADEMA waliouawa huko Igunga na Arusha, akabeba majeneza yao na kutoa kauli ya kukubali tuhuma zinazoelekezwa kwa CCM kuhusika na mauaji yao na hivyo wananchi nao waikatae? Jeuri ya Mwigulu na kufanya ama kusema lolote atakalo anaipata wapi?

Je, wakubwa zake na viongozi wengine hawaoni kama jamaa huyu anakiangamiza chama chao kwa mambo yake haya? Wote hawajali kabisa? Waswahili walisema mchelea mwana kulia hulia mwenyewe! Mwache aendelee kutojali maana muda si muda Watanzania kwa maelfu watageuza shingo watazame kwingine na kuwaacha akina Mwingulu wakisaka mwingine wa kumnadi!


Chanzo: Tanzania Daima 15/06/2013
 
Bora wewe umeliona hili katika sura hii. Wengi wamelinyamazia as if madhara yake ni madogo. Kwa kuzingatia kuwa pesa yake imetokana na jasho letu wenyewe ni jambo zuri tu kuwa receipients wazipokee ila ikifika kwenye kutakiwa kumpigia kura wawe na utashi wa kutojali alichowapa.
 
Wapo watu walioko kwenye list ambapo vurugu ikitokea vichwa vyao vitatangulia, Mwigulu na Nape, Lusinde hawatapona
 
Back
Top Bottom