Nampenda mmoja, naye anajua!

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Nov 22, 2012
1,985
1,284
NAMPENDA MMOJA, NAYE ANAJUA.

Kiumbe silete hoja, sikiza nakuambia,
Nimpendaye mmoja, moyoni alonitia,
Hao unao wataja, si wangu wanizushia.
Jina sitakutajia, nimpendaye mmoja.

Apendeza bila koja, wallahi ametimia,
Si usoni hata paja, kila kitu avutia
Nikimuita yuaja, mtiifu wa tabia,
Jina sitakutajia, nimpendaye mmoja.

Hili jambo lina tija, mimi nilo kusudia,
Nimeshatoa mkaja, mahari yafuatia,
Nimeuchoka useja, wa mito kukumbatia,
Jina sitakutajia, nimpendaye mmoja.

Muogope sana mja, mama aliniusia
Haishiwi na harija, mapenzi kukuvunjia
Hatimaye huwa chaja, muhibu awe nokia,
Jina sitakutajia, nimpendaye mmoja.

Kwahivyo sioni haja, ya jina kukutajia,
Kutotaja sikuroja, ni mafunzo ya nabia,
Naomba sikose kuja, hiyo siku kiwadia,
Jina sitakutajia, nimpendaye mmoja.

Ukome kutajataja, njia ni'zo zipitia,
Hayo unayo bwabwaja, yasije kumfikia,
Tungule iwe tunguja, iso faa kupikia,
Jina sitakutajia, nimpendaye mmoja.

Naapa sitakufuja, ulipo nyonda sikia,
Mahaba hayatachuja, kama safi zetu nia,
Lije vumba la kangaja, jua nitavumilia,
Jina sitakutajia, nimpendaye mmoja.

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
0622845394
Morogoro.
 

Attachments

  • gold heart.jpg
    gold heart.jpg
    35.3 KB · Views: 54
Back
Top Bottom