NAMPENDA MKE WANGU..
sijuti japo dakika
kumpenda mwari yule
na kwao nilishafika
Kuchunguza pole pol
Nikapewa data zake
Tena kinagaubaga
Na sifa za waze wake
Hakika ndizo kaiga
tabia yake adimu
sijapata kuiona
Mwingi wa kutabasamu
Nyumbani atulizana
Nimedata na niqabu
baibui vazi lake
kafunzwa kwao adabu
kanifaa kuwa mke
Karidhia yangu hali
Sioni kwake kasumba
Basmati wake mwili
Umbo lake moja namba
mtaalamu jikoni
Kwa hili namuelewa
nakomba paka sahani
Nikizidi kunogewa
Mwenzenu nabembelezwa
Kwa uchovu wa kazini
kifuani natulizwa
Na maneno malaini
Mke wangu katulia
Wala sio mcharuko
Sie kiguu na njia
kucha haeshi vituko
*Chakula nala vizuri*
*Na Maneno ya mahaba*
*Matonge anahimili*
*Anakula na kushiba*
Hasira anadhibiti
si mtu wa kupayuka
Kumpiga haupati
Wala haombi talaka
Vyakula anavyopika
Sijawai kukinai
Anaziweza pirika
roho yangu yafurahi
Macho yake alegeza
Pindi nikimtazama
Haeshi kunikonyeza
Anipa yangu heshima
yarabi nijaalie
nidumu na huyu mwana
Riziki nifungulie
na tuzidi kupendana