Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
- TTCL ilitumia Billioni 56 kununua minara hewa.
- Kwa mujibu wa barua aliyoandikiwa Spika Ndugai na wafanyakazi wa TTCL kuomba uchunguzi wa kibunge ufanyike, kuna deni hewa lililotengenezwa na management la Tsh Billioni 240 kwa ajili ya kusimika minara kwa mfumo wa "Base Tranceiver System (BTS),’ minara ambayo kimsingi haikusimikwa TTCL.
- Mwekezaji aliyepewa kuendesha TTCL kwa hisa asilimia 35 aliposhindwa kuendesha alifanya hujuma ya kung'oa mitambo yote iliyokuwa katika Chuo cha TTCL kilichokuwa eneo la Kijitonyama (Dar es Salaam) na kukifunga chuo hicho na kung’oa mtambo wa kutoa ankara kwa wateja (Subscriber Order Billing System - SOBS) ambao, kwa mujibu wa wahandisi wa kampuni hiyo, ulikuwa bado na uwezo wa kufanya kazi kisasa.
- TTCL ilikusanya vibanda vya kupiga simu mitaani(call box) na kuviuza kama chuma chakavu.
- Mtambo wa kutengeneza Kadi za kuongeza muda wa maongezi (Scratch Card) ulikamatwa maeneo ya Mikocheni-Maji Machafu, kwenye nyumba ya mmoja wa wabunge vijana wa Bunge la sasa, ambaye ana uhusiano wa nasaba na vigogo wakubwa wa nchi hii.
WAKATI Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikionyesha Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) imekuwa ikitengeneza hasara mfululizo kutokana na vizuizi vya kusambaa kwa mtandao na kukosa vifaa vya kisasa, kampuni hiyo inatajwa kutumia Sh. bilioni 56 kununua minara ‘hewa.’
Katika ripoti yake ya mwaka 2014/2015 iliyotolewa mwezi uliopita CAG ameeleza kuwa kampuni hiyo imekuwa ikitengeneza hasara mfululizo.
“Kampuni imekuwa ikiendelea kutengeneza hasara mfululizo mwaka hadi mwaka, hali iliyopelekea iwe na hasara ya jumla ya kiasi cha shilingi milioni 360,847 kwa mwaka 2014 (mwaka 2013 ikiwa shilingi milioni 334,480). Hasara hii imechangiwa na uwepo wa vizuizi vya kusambaa kwa mtandao, kutokuwepo kwa teknolojia ya kisasa, kukosekana kwa ufanisi wa mgawanyo wa masoko, na ukosefu wa fedha za kujikuza kibiashara ikilinganishaw na kampuni nyingine za simu,” inasema ripoti hiyo.
Wakati ripoti hiyo ikionyesha hivyo, tumefanikiwa kuona nyaraka zinazoonyesha za manung’uniko ya wafanyakazi ndani ya kampuni hiyo kuhusu utata katika ujenzi wa minara hiyo.
Katika barua waliyomwandikia Spika wa Bunge, Job Ndugai, Februari Mosi, mwaka huu, wameliomba Bunge, kuchunguza suala ambalo hata hivyo, lilikwishachunguzwa na Kamati Ndogo ya Bunge ya Miundombinu iliyofanya kikao Juni 20, 2015, kwa mahojiano ya kiuchunguzi.
“Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabau za Serikali (ukaguzi maalumu) 2013/2014 ulibaini kuwa TTCL ilikuwa inadaiwa shilingi bilioni 384, kati ya hizo shilingi bilioni 240 lilikuwa deni ‘Base Tranceiver System (BTS),’ minara ambayo haikusimikwa TTCL, deni hilo hewa,” inasema sehemu ya barua hiyo kwa Spika wa Bunge.
Hata hivyo chanzo chetu kingine kimeeleza kuwa awali uongozi wa TTCL ulitengeneza hesabu na kuonekana deni la BTS hizo kwa ajili ya CDMA lilikuwa shilingi bilioni 236, lakini baada ya kuhojiwa na baadhi ya wafanyakazi kuonyesha wasiwasi, uongozi ulitoa ufafanuzi kuwa kulikuwa na makosa katika deni hilo na baadaye walivyokokotoa hesabu, deni lilibaki kuwa shilingi bilioni 56.
“Lakini hata hiyo bilioni 56 italipwa ya nini, kwa sababu minara haikujengwa yote, ndiyo maana ukiwa na simu ya mkononi ya TTCL ukitoka kuelekea nje ya mji mtandao unasumbua na kwingine haupo kabisa, kama ingejengwa, kusingekuwa na shida hii,” kinaeleza chanzo chetu kingine.
Uchunguzi wetu umeendelea kubaini kuwa, pamoja na kampuni hiyo kutakiwa kulipa deni hilo la shilingi bilioni 56 kwa Kampuni ya Huawei, tayari TTCL wameanza maandalizi ya awali kuzima mitambo ya CDMA ili wahamie kwenye teknolojia ya GSM.
“Kwa hiyo hata kama hiyo minara ingejengwa yote, mradi huu tayari ni ‘white elephant’ kwa sababu mipango ya awali ya kuzima mitambo ya CDMA imeanza, kwa hiyo deni hilo linalipwa hata sijui kwa faida gani,” anaeleza mtaalamu wa mawasiliano ya simu wa kampuni hiyo ambaye kwa sababu za wazi hatutataja jina lake na kuongeza; “Na kama minara hiyo ingekuwepo, tatizo la vizuizi kwenye mtandao lisingekuwepo, kazi ya BTS ni kupokea mawimbi, kuyachuja na kuyasambaza kwenye eneo lake na kuyatuma kwenye minara mingine, mtandao wetu ungekuwepo karibu nzima.”
Ubinafsishaji ulivyoimaliza TTCL
Uchunguzi umebaini pia kuwa mwekezaji aliyenunua hisa asilimia 35 za TTCL, DETECON/MSI, alishinda zabuni hiyo kwa kuahidi kujenga njia za simu 800,100 pamoja na kulipa Dola za Marekani milioni 120.
Kwa mujibu wa taarifa kwa wafanyakazi kuhusu ubinafsishaji wa TTCL, iliyotolewa kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo Juni 29, 2000, njia hizo zilipaswa kufungwa katika kipindi cha miaka minne, mpaka mwaka 2003.
“Kampuni zilitakiwa kuonyesha waziwazi katika zabuni zao bei ya kununulia asilimia 35 ya hisa za TTCL na pia kueleza njia za simu watakazofunga katika kipindi cha miaka minne. Hivyo ndivyo vigezo vilivyotumika kuwatathmini wazabuni kumpata mshindi,” inasema sehemu ya taarifa hiyo iliyotiwa saini na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa wakati huo, A. Mpatwa.
Kampuni iliyoshinda zabuni hiyo, haikujenga njia hizo za simu ilizoahidi na badala yake masharti waliyoweka baada ya kuingia ubia yalisababisha kupungua zaidi kwa wateja wa simu za mezani (land line) badala ya kuongeza njia.
“Kitu cha kwanza menejimenti ikavunja mikataba yote ya wateja ambayo awali ilikuwa ya malipo baada ya kutumia (post paid) na kuifanya kuwa ya malipo kabla ya kutumia (pre paid) bila kujali masharti ya mikataba ya awali, hili lilipoteza wateja zaidi ya robo, lakini pia hata waliobaki kukawa na mlolongo wa namba nyingi ukitaka kupiga simu mpaka umpate unayemtafuta, wengi wakaona usumbufu, nalo likatupotezea wateja zaidi,” kinaeleza chanzo chetu kingine kutoka ndani ya TTCL.
Aidha inaelezwa kuwa MSI walishindwa kufanya matengenezo ya mitambo na miundombinu, badala yake waling’oa mitambo yote iliyokuwa katika Chuo cha TTCL kilichokuwa eneo la Kijitonyama (Dar es Salaam) na kukifunga chuo hicho na kung’oa mtambo wa kutoa ankara kwa wateja (Subscriber Order Billing System - SOBS) ambao, kwa mujibu wa wahandisi wa kampuni hiyo, ulikuwa bado na uwezo wa kufanya kazi kisasa.
Wafanyakazi wa TTCL wamekuwa pia wakilalamikia mwenendo wa mwekezaji huyo kuigeuza kampuni hiyo kuwa shamba la bibi. Katika barua waliyomwandikia Spika wa Bunge, Job Ndugai, Februari Mosi, mwaka huu wakitaka Bunge liunde kamati ya uchunguzi kuhusu mambo mbalimbali wanayolalamikia katika kampuni hiyo, wameeleza jinsi watendaji walivyokiuka sheria ya TTCL namba 20 ya mwaka 1993, kifungu cha 6(2) (b) (c) na kuwapendelea wageni.
“ Wawekezaji hao hawakulipa pesa yote iliyokuwa imekubaliwa kwenye mkataba. Walikodisha hisa asilimia 35, jenga endesha rejesha (Build, Own and Transfer). Wawekezaji kwa nyakati tofauti ‘walifaulisha’ ukodishaji wa hisa kwa kampuni zifuatazo, Celtel International, Zain Kuwait na sasa Bharti Airtel India. Wawekezaji wakati wote wamekuwa na migogoro na serikali, wafanyakazi na wateja, hawakuwekeza chochote TTCL kwa mujibu wa mkataba,” inaeeleza sehemu ya barua hiyo kwa Spika, ambayo tumefanikiwa kuiona nakala yake.
‘Cha mlevi huliwa na mgema’
Katikati ya malalamiko hayo dhidi ya uwekezaji huo, serikali na uongozi wa kampuni hiyo uko kwenye mchakato wa kumlipa mwekezaji huyo shilingi bilioni 14.9, ili arejeshe asilimia 35 ya hisa kwa TTCL.
“Sisi tumepinga hiyo, mali za nchi hii zimekuwa kama za mlevi tu zinaliwa na mgema, hawa jamaa hawajawekeza chochote wamekiuka masharti mengi ya mkataba, wamekuwa wakihamishiana hisa hizo kutoka kampuni hii kwenda ile bila serikali wala TTCL kupata chochote, hizo bilioni 14.9 wanataka kulipwa za nini?” kinaeleza chanzo chetu kingine ndani ya menejimenti ya TTCL.
Katika barua yao kwa Spika, kamati ya wafanyakazi inasema; “Watendaji wanataka kuilipa Bhart Airtel shilingi bilioni 14.9 zinazotokana na tozo zinazolipwa kwa wateja kwa ajili ya kuunganishwa (Internet) ‘optic fibre’ wakati hakuna mpango mahsusi wa kuwawajibisha walioiba mali ya kampuni wala kuwalipa wafanyakazi haki zao.”
Vituko vya kadi za rafiki
Katika mchakato wa kupunguza wafanyakazi uliokuwa ukifanywa na uongozi mpya wa kampuni hiyo, walifukuza wafanyakazi wote katika kitengo cha simu za vibani (call box).
“Wafanyakazi waliofukuzwa wakaondoka na mtambo maalumu wa kutambua kadi wakati unapiga simu kwenye kibanda, tukapata matatizo makubwa sana kwa wateja, simu zikawa haziendi, uongozi wa MSI wakaamua kuondoa huduma hiyo na kadi zenye thamani ya shilingi bilioni tatu zilichomwa moto,” kinaeleza chanzo kingine.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kampuni hiyo ilikusanya vibanda vyote vya kupigia simu na kuviuza kama chuma chakavu.
Hujuma kwa ‘scratch card’
Katika kile kinachoelezwa na baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya TTCL kuwa zilikuwa ni hujuma za makusudi kuidhoofisha kampuni hiyo, mwaka 2011 wafanyakazi walikamata mtambo wa kutengeneza kadi za kuongeza muda wa maongezi kwa simu za mkononi za TTCL.
Mtambo huo ulikamatwa maeneo ya Mikocheni-Maji Machafu, kwenye nyumba ya mmoja wa wabunge vijana wa Bunge la sasa, ambaye ana uhusiano wa nasaba na vigogo wakubwa wa nchi hii.
Inaelezwa kuwa kila mafundi walipopanda kwenye nguzo kufanya mategenenzo jirani na nyumba hiyo, walinzi waliwafukuza. Baada ya kutilia wasiwasi nyumba hiyo, waliharibu simu ya mezani iliyokuwa ikitumika katika nyumba husika, wenyewe wakalazimika kuwaita mafundi wa TTCL ndipo walipogundua ufisadi huo.
“Hizo kadi feki zikaingizwa kwenye mzunguko, ule mtambo wa kutambua kadi zitumike (Activation Machine) ukawa unazitambua hizo feki, kadi halisi zikawa hazitambuliwi, ukijaribu kuiweka unaambiwa namba hizo hazijafikiwa,” kinaeleza chanzo chetu.
Hiyo ni moja ya sababu zinazoelezwa kuifanya kampuni hiyo ishindwe kushindana vyema sokoni na kujikuta ikipata hasara.
Mgogoro na wafanyakazi
Kutofanya vizuri kwa kampuni hiyo kunasababishwa pia na mgogoro kati ya menejimenti na wafanyakazi, ambapo mwaka 2003, MSI walianzisha muundo mpya uliotambua vyeo vya wafanyakazi katika ngazi ya menejimenti peke yake, lakini wafanyakazi wengine wakipewa wadhifa wa ‘team members’ bila kujali elimu, weledi na uzoefu kazini.
Kubadili huko kwa muundo kulisababisha mgogoro kati ya pande hizo na hata kufunguliwa kesi tatu mahakamani; kesi namba 34 ya mwaka 2004 kati ya Lucas Michael na wenzake dhidi ya Menejimenti ya TTCL na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kesi namba 90 ya mwaka 2004 kati ya Menejimenti ya TTCL dhidi ya Lucas Michael na wenzake na kesi namba 204 ya mwaka 2004 kati ya Geroge Mwafalo na wenzake dhidi ya Menejimenti ya TTCL.
“Huwezi ukafanya kazi kwa ufanisi na watu ambao wanahisi hawathaminiwi, watu wameshushwa vyeo, kama ulikuwa mhandisi unafaywa kuwa fundi mchundo (technician), hili limewachanganya na kuwavunja moyo wafanyakazi,” anasema mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Katika barua yao kwa spika, wafanyakazi hao wanaomba Bunge liingilie kati ili walipwe haki zao kwa wakati.
“Bunge lijadili na hatimaye liisimamie na kuishauri serikali kulipa haki za wafanyakazi kabla mwekezaji, Bhart Airtel India kuondoka TTCL ili wafanyakazi tupate haki zetu,” wanaeleza wafanyakazi hao.
Menejimenti yafafanua
Akizungumzia malipo ya shilingi bilioni 14.9 kwa kampuni ya Bhart Airtel, Meneja Uhusiano wa TTCL, Nicodemus Thomas, alisema kiasi hicho ni uamuzi wa mwisho wa serikali kuwalipa wawekazaji hao ili waachie hisa hizo.
“Kilichokuwa kinafanyika sasa hivi zilikuwa ni hatua za mwisho zinazowashirikisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ili kubaini kama kuna kodi inatakiwa kulipwa, vinginevyo huo ni uamuzi sahihi kabisa wa serikali na ulitangazwa na waziri mwenye dhamana,” alisema na kuongeza; “Katika suala hili hakuna kurudi nyuma ni kuwalipa hawa jamaa, tulitarajia kabla ya Aprili lakini sijui nini kimechelewesha, serikali ilikwishakuridhia kumlipa mwenkezaji ili arejesha 35% za TTCL na kuifanya TTCL kuwa mali ya umma.”
Kuhusu deni la shilingi bilioni 236 zinazodaiwa kuwa za minara hewa, meneja huyo aliahidi kufanya utafiti wa kutosha kwa kuwa ni deni lenye historia ndefu.
Chanzo: Raia Mwema