Naibu Waziri ataka Copa Coca Cola ya wanawake

sulphadoxine

JF-Expert Member
Nov 1, 2010
2,257
645
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Kasim Majaliwa, amelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuhakikisha linaandaa ligi ya vijana ya Copa Coca Cola kwa wanawake.


Waziri huyo, pia ameagiza kuwepo kwa timu za soka za wanawake kutoka kila kanda katika mashindano ya Umoja wa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na ule wa Shule za Sekondari (UMISSETA).

Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati wa kufungu kozi ya kimataifa ya mpira wa miguu kwa wanawake iliyoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Dunia (FIFA), alisema ni wakati sasa wa soka la wanawake kupewa thamani ya juu na kwamba, Serikali imejipanga kusaidia kozi zote za mchezo huo ili kutoa makocha wengi.

"Tunataka kuona soka la wanawake linachezwa katika ligi mbalimbali, ikiwemo michuano ya UMISETA na UMITASHUMTA ya mwakani, tayari tuna hazina ya walimu wenye taaluma ya kufundisha mchezo huu," alisema Majaliwa.

"Kwa upande wa TFF, tutashirikiana nao ili kuona kozi hizi zinafanyika bila kikwazo, pia tunaomba TFF katika ligi yenu ya Copa Coca Cola ya vijana kuanzishwe na mashindano ya wanawake ,naahidi kama serikali tutashirikiana nanyi," alisema.

Majaliwa alisema kwa sasa serikali imewekeza zaidi kwenye michezo na kwamba, watatilia umuhimu zaidi soka la wanawake kwa kuwa, limeanza kupata mafanikio makubwa na kuwepo katika ramani ya Dunia.

Naibu Waziri huyo amewataka wahitimu hao kuzingatia sheria ili kufundisha soka lenye utaalam zaidi na kwamba, wanategemea vijana watakaofufuliwa kupitia kwa walimu hao, ni wenye kucheza soka la kitaalamu zaidi.

Kozi hiyo ambayo ilishirikisha walimu wa shule za msingi na sekondari, imeendeshwa na mkufunzi wa Shirikiso la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), kutoka nchini Namibia, Jacqueline Chipanga, ambaye amesifu jitihada za TFF katika kuhakikisha soka la wanawake linapata mafanikio.

Mkufunzi huyo, pia amevutiwa na kiwango cha timu ya soka cha Twiga Stars kupitia mashindano ya Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Ukanda wa Kusini mwa Afrika (COSAFA), na kusema ni timu bora Afrika, ambayo itaweza kupiga hatua kubwa ikiwa nguvu ya pamoja kati ya serikali na TFF, itawekwa.

Naye, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema wameamua kuendesha kozi hizo za wanawake kwa kushirikiana na FIFA, ili kuona mchezo huo unafundishwa na wanawake wenyewe.

Alisema TFF imeandaa semina ya pamoja ya mpira wa miguu itakayofanyika Oktoba mwaka huu, ambayo itakuwa ni maalumu kwa ajili ya kufafanua umuhimu wa mpira wa miguu kwa wanawake.

Kozi hiyo inatarajiwa kumalizika leo, ambapo wahitimu hao watarudi sehemu zao za kazi kwa ajili ya kuanza kufundisha soka la wanawake nchini kote.
 
Back
Top Bottom