figganigga
JF-Expert Member
- Oct 17, 2010
- 25,658
- 55,487
WANANCHI wa Kijiji cha Mwela Kata ya Kandete wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya wako hatarini kukumbwa na baa la njaa baada ya kuibuka kile kinachodaiwa ‘mzimu wa ajabu’ ambao umekuwa ukianua unga unapokuwa umeanikwa juani na kupotea hewani katika mazingira ya kutatanisha.
Hali hiyo imejitokeza siku chache baada ya ‘mzimu’ huo kuzuka katika kijiji hicho ikielezwa kuwa unga na mazao mengine yaliyokuwa yameanikwa juani yalipotea hewani.
Kutokana na tukio hilo, imewalazimu wananchi wa Kijiji cha Mwela kutisha mkutano wa halmashauri ya kijiji kujadili na kutafuta suluhu ya hali hiyo.
Akizungumza na mwandishi kuhusu tukio hilo, mkazi mmoja wa kijiji hicho, Hamfrey Mwakitwange, alisema kuibuka kwa mzimu huo kumezua hofu kwa wakazi wa Mwela na maeneo ya jirani.
Alisema mwaka huu kuna hatari ya kutokea ukame na baa la njaa baada ya kuibuka mzimu huo wa ajabu.
“Kwa tukio la kuwapo mzimu huu wa ajabu tumejawa na hofu kubwa na kuna dalili ya kukumbwa na baa la njaa mwaka huu.
“Mzimu umekuwa ukichukua chakula hasa unga na mazao yanayoanikwa juani…tunabaki tunajiuliza, na sasa kimeitishwa kikao cha halmashauri ya kijiji ingawa mtazamo umegawanyika… sasa kuna wengine wanataka hata tuhushishe waganga,” alisema Mwakitwange.
Mjumbe wa Nyumba 10 wa CCM, Matrida Mwaisumbwa, alisema kitendo cha kuibuka mzimu huo ambao umekuwa ukichukua chakula, umeleta sintofahamu kijijini hapo.
Alisema hata wanapokuwa wanapika chakula kama ugali au ndizi, kimekuwa hakina radha na inadaiwa chakula hicho pia kinakuwa kimetembelewa na mzimu huo wa ajabu.
Alisema uongozi umeandaa mkakati wa kupita nyumba kwa nyumba kukusanya michango kuwasaidia wananchi ambao wamekwisha kuathirika na mzimu huo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwale, Ferki Mwandenga, alisema licha ya kuwapo taarifa za mzimu huo wa ajabu anashindwa kuieleza kwa kina hali hiyo.
“Siwezi kulisema hili jambo maana linachanganya kidogo, sijui ni tukio la kichawi? Ingawa pamoja na hali hiyo, tambua kuwa Serikali haiamini uchawi,” alisema Mwandega.
Chanzo: Mtanzania