Nilikuwa miongoni mwa watu wa awali kupinga uamuzi wa RPC wa Mwanza, kwa kushinikizo la Mkuu wa Mkoa huo, kupiga marufuku wafuasi wa Ukawa na wananchi wengine kuuaga mwili wa Alphonce Mawazo. Kwa kweli sikutarajia Jaji mwenye weledi wa sheria anayezingatia mila na desturi za jamii yetu, aunge mkono marufuku hiyo haramu. Jaji Mlacha amefanya kazi yake nzuri. Tunampongeza.
Uamuzi wa RPC hata kama ulikuwa ni wa shinikizo, ulikuwa na athari kubwa kwa Rais Magufuli, ambaye tangu mapema kabisa aliahidi kuiongoza Tanzania bila kujali itikadi, kabila, dini, kanda wala hali ya mtu. Hiyo ndiyo Serikali ya Magufuli ambayo Watanzania wanataka kuiona.
Mimi si mfuasi wa vyama vya siasa, lakini linapokuja suala la haki na usawa, mara zote nimesimamia misingi hiyo; na wala siwezi kujifanya hamnazo na kuona vitu hivyo vikipuuzwa. Sasa kumejitokeza taasisi eti zinazoshangazwa na suala la msiba wa Mawazo kufanywa la kisiasa! Sijui ni kutafuta sifa, au kitu gani. Mawazo alikuwa Mwenyekiti wa chama Mkoa. Hadi anauawa, alikuwa na wadhifa huo. Ameuawa muda mfupi akitoka kwenye siasa! Ameuawa muda ambao bado moshi wa kisiasa ukiendelea kufuka huku na kule nchini kote.
Msiba wa mtu wa aina hiyo hutarajii kuona ukiishia kwenye mapambio pekee bila kuingiza neno la kisiasa. Kama Mawazo angekuwa amekufa kifo kilichosababishwa na malaria au ugonjwa mwingine, kweli hapo siasa isingekuwa mahali pake. Angekuwa ameuawa kwa ugomvi wa ardhi, kweli hapo siasa isingekuwa mahali pale! Mtu aliyeuawa katika mazingira yanayoashiria kuwa ni ya kisasa itakuwaje msiba wake usitawaliwe na hisia za kisiasa? Marafiki wakuu wa Mawazo aliokuwa karibu nao ni wanasiasa. Je, wanaopinga siasa kwenye msiba huu, wanatarajia Mbowe, Mbatia, Lowassa, na wafuasi wengine wa Ukawa, wazungumze nini kisichoshabihiana na siasa? Je, wanatarajia jeneza lenye mwili wa Mawazo lifunikwe kwa kitambaa gani zaidi ya bendera ya Chadema?
Huu ni mtazamo wangu ambao hauna vimelea vya kiitikadi, isipokuwa mimi ni katika wale wanaoamini kuwa kuusema ukweli kutatuweka huru; na kwa njia hiyo tutakuwa tunashiriki kuijenga Tanzania yenye Haki na Usawa. Kuzuia Siasa kwenye msiba wa Mawazo ni sawa na kumtaka Padre au Sheikh asimtaje shetani wakati wa ibada; kitu ambacho hakiwezekani aslani.