Chachu Ombara
JF-Expert Member
- Dec 11, 2012
- 6,162
- 11,229
Dodoma. Serikali imesema zaidi ya Sh 1.6 trilioni zinapotea kwa mishahara hewa nchini kila mwaka.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alipokuwa akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu.
"Ukisoma taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), utagundua zaidi ya Sh1.6 trilioni zinapotea kutokana na mishahara hewa, fedha inayotosha bajeti ya wizara," alisema.
Alitoa mfano wa deni la walimu lililopelekwa wizarani kwake lilikuwa Sh19 bilioni, lakini baada ya uhakiki ikaonekana kiasi kinachodaiwa ni Sh5 bilioni tu.
Mfano mwingine ni walipolipa kupitia akaunti za watumishi waliokoa Sh40 bilioni kwa mwezi.
"Na hilo ni eneo moja tu hatujahakiki sana majina ya akaunti. Deni la trilioni 1.6 na kati ya hizo Sh1 trilioni ilikuwa imeshalipwa, lakini tuliwaambia wakague pia na hizo zilizolipwa,"alisema.
Hata hivyo, alisema Sh142 bilioni kati ya Sh500 bilioni zilizokaguliwa, ndizo zilikuwa halali.
"Lakini pia taasisi zilizokuwa zikipokea mishahara kwa fungu yaani moja kwa moja ndizo zilikuwa zikiongoza kwa mishahara hewa,"alisema.
Alisema kwa upande wa vyuo vya elimu ambavyo vilikaguliwa hivi karibuni ilibainika kuwa kati ya deni la Sh10 bilioni ni Sh2 bilioni tu zilikuwa ni halali.
Hatua zilizochukuliwa
Mwigulu alisema wale wote waliobainika kughushi malipo wamepelekwa kwenye vyombo vya dola.
"Wengine tumewapeleka Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), kama kuna mwalimu mmoja alikuwa anadai Sh50 milioni wajanja wakaongeza 0 tumewapeleka huko,"alisema.
Alipotakiwa kusema idadi ya watumishi waliochukuliwa hatua kutokana na mishahara hewa, Mwigulu alisema idadi yao ni kubwa.
"Ni idadi kubwa tuliowachukulia hatua kwa sababu madeni yamesambaa eneo kubwa hayako eneo moja," alisema.
Mwigulu alisema pia amemwambia katibu wake, amwandikie Katibu Mkuu wa Utumishi awachukulie hatua za kinidhamu pamoja na kwamba watachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema suala la kuchukua hatua linahitaji ujasiri kwa kuwa kuna Watanzania ambao wanatarajia viongozi kuchukua hatua.
"Wizara ya Fedha tumesema tutasonga mbele na hatuyumbishwi na mtu yeyote ambaye anakwamisha jitihada na hatua ambazo zinalenga katika kuokoa fedha za Watanzania," alisema Mwigulu.
Alisema kwa kuhakikisha kuwa wanaondokana na mishahara hewa, hivi sasa wizara imeanza kulipa moja kwa moja na kuhakiki taarifa.
Maeneo yenye changamoto
Mwigulu alisema wanasimama kwa jitihada zote ili kuhakikisha mipango iliyoamuliwa kutekelezwa inaleta tija kwa nchi.
Mwigulu alisema maeneo mawili makubwa yanahitaji mabadiliko ili Taifa liweze kupiga hatua.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni maadili na kuondokana na kufanya kazi kwa mazoea.
"Utaona kuwa hili la maadili nimeweza kupambana nalo kwenye mishahara hewa. Nashukuru Mungu watu wanaliunga mkono. Kwenye hili la mishahara hewa utaona linatokana na maadili na kufanya kazi kwa mazoea," alisema na kuongeza:
"Kuna watu wanafanya kazi kwa mazoea tu. Hawarekebishi taarifa za watumishi. Taarifa za watu waliostaafu, waliofariki dunia, walioacha kazi, waliofukuzwa, anaacha wanaendelea kulipwa tu. Hili ni kufanya kazi kwa mazoea na kutokuwa na shauku ya kufanya kazi kwa ufanisi," alisema.
Mwigulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi, alisema kuwa mishahara hewa mingine ni njama ambapo wanataka kuibia serikali kwa makusudi.
"Wanajua kwamba watu hawastahili kuwa kwenye ‘payroll' (orodha ya mishahara), wanaacha walipwe halafu wanachukua fedha hizo," alisema na kuongeza:
"Lingine ni la watu kukwepa kodi na kutotaka serikali kupata mapato. Watu wanaokwepa kodi na wale wanaofuja fedha za umma ni la kimaadili."
Alisema kosa la kufanya kodi isifike serikalini ni la mazoea mabaya.
Alisema baadhi ya Watanzania hawajui uhusiano wa risiti na kodi inayokwenda serikalini. "Baadhi ya watu wanafanya majadiliano kabisa ya bei isiyo na risiti na yenye risiti, lakini hajui kuwa mapato hayaendi serikali,"alisema.
Mwigulu alisema wapo baadhi ya watu wako tayari kutoa rushwa ya Sh50,000 kuliko kulipa kodi ya Sh 10,000 na kwamba hayo ni mazoea mabaya.
"Nimekuwa nikiwaambia wizarani kuwa mabadiliko ni vitendo kwa mtu mmoja mmoja. Mtu mmojammoja akianza kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea utaona Taifa hili linapiga hatua,"alisema.
Sheria kikwazo
Mwigulu alisema changamoto kubwa wanayokutana nayo katika mapambano hayo ni mlolongo mrefu wa uchukuaji wa hatua kwa watu wanaothibitika kuhusika na mishahara hewa.
"Hili suala la mtu kulindwa sana kwa mtu ambaye amewaibia waliowengi mimi silipendi. "
Alisema kuwa mtumishi ambaye amethibitika kuhusika na ubadhirifu wa fedha na makosa mengine kuna mlolongo mrefu sana wa kumchukulia hatua.
"Mimi nilitaka kufanya kazi kwa vitendo na kwa mfano watu waone kufanya makosa hayo kuna gharama yake. Lakini sasa utaona inachukua miaka mitano hadi 10 ili watu waone, hiyo ni moja ya changamoto,"alisema.
Alisema changamoto nyingine ni ya watu kushindwa kutoa taarifa kuhusiana na ukiukwaji wa maadili.
Unaibu Uwaziri
Alisema alipoingia katika nafasi hiyo alikuwa anataka kutekeleza miradi mipya, lakini alikutana na viporo vya madeni ya miradi.
"Wakati ule kulikuwa na viporo vya madeni mengi sana na mbaya zaidi ni madeni ambayo hayapo katika bajeti. Sasa hapa unapata changamoto kubwa, fedha unayoipata unalipia miradi mipya ama madeni," alisema na kuongeza,
"Wazabuni wadogo wengine walikopa katika benki kwa hiyo usipowalipa hawa unawaingiza katika umaskini. Mtu amekopa benki na amesha ‘supply' (sambaza) kwa maana hiyo ameshaitumia fedha unaacha kumlipa kwa miaka miwili ama mitatu maana yake unamtia umaskini."
Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, alisema alikutana na changamoto kubwa sana kwa sababu fedha za kulipa madeni hayo hazikuwa katika bajeti.
Alisema mara alipokuwa akikutana na watu ambao wengine wanataka kufilisiwa na benki, kuuziwa nyumba ilikuwa ni changamoto kubwa sana kwake katika nafasi hiyo.
"Lakini ukienda hata katika wizara hawakutenga fedha kwa ajili ya kulipa madeni. Kwa mfano katika barabara deni pekee linacheza katika Sh600 bilioni hadi Sh800 bilioni bajeti ya wizara iko karibia trilioni moja na sehemu,"alisema.
"Utaona changamoto ya uandaaji wa bajeti inapaswa kuangalia mambo hayo yote mawili (bajeti na madeni), unapoweka bajeti uweke pia na miradi inayoendelea, kazi zilizofanyika na mipango inayofuata," alisema.
Alisema changamoto kubwa ni nchi kushindwa kutumia ushirikiano wa sekta binafsi na umma (PPP), ambapo hata miradi mikubwa bado inatekelezwa kwa fedha za serikali.
"Wenzetu walishavuka hapo miradi mikubwa haitekelezwi na fedha za serikali. Fedha za serikali zinatekeleza miradi midogo midogo kama ya huduma za jamii,"alisema.
Hata hivyo, alisema hapa nchini hali ni tofauti miradi kama ya viwanja vya ndege, ujenzi wa reli, bandari inatumia fedha za serikali na hivyo kuvuta fedha ambayo ilikuwa iende katika miradi ya jamii.
Matumizi ya anasa
Mwigulu alisema kuna matumizi mengi ya anasa ilhali watu hawana maji safi na salama na huduma za afya.
"Ingali watoto wengine wanasoma katika shule za kata kwa kuuza matembele, kusomeshwa na wajane kuuza karanga halafu anaenda kidato cha tano anasoma kwa shida hivyohivyo, anachaguliwa chuo kikuu anakosa mkopo ilhali mashirika ama taasisi zimetumia fedha kwa matumizi yasiyo ya lazima," alisema.
Alisema hilo si jambo mwafaka kwa Taifa sasa hivi kutumia fedha za umma kwa mambo ambayo hayana ulazima.
Alitaka kila mtu aliyepewa nafasi katika siasa na utumishi kutambua kuwa kuna Watanzania maskini.
"Atambue kuwa kuna Watanzania maskini leo hawawezi kununua maji, watambue kuwa Sh20,000 ya ada ni fedha nyingi sana zinawasumbua,"alisema.
Mwigulu alisema alihangaika sana hadi kufikia uamuzi wa kukata asilimia tano ya bajeti ya mwaka jana na kwamba ilikuwa ni njia ya haraka.
"Mtu uliyezaliwa katika kijiji ambacho hakina maji, unawezaje ukaipangia wizara Sh900 milioni kwa ajili ya tamasha la wizara la wiki moja, halafu wilaya ukaipangia Sh300 milioni za miradi ya maji?" alihoji.
Alisema hiyo ni kupoteza mwelekeo. "Unawezaje kutumia bilioni moja kwa wiki ya maji katika kijiji ambacho hakina maji ambacho ili kipate maji kinahitaji Sh100 milioni," alisema.
Alisema nchi ina wiki zaidi ya 90 zinazohusiana sherehe ambazo zimekuwa zikitumia fedha kwa ajili ya maandalizi, kulipana posho, ununuzi wa fulana, karatasi, kofia na kufunga ofisi.
Licha ya kutumia matumizi hayo bado kuna matumizi hewa ambayo yanaambatanishwa na sherehe hizo.
"Shule nyingine za mjini hazina madawati, wanafunzi wake wanaketi chini, shirika la serikali wafanyakazi wake wanajaa kwenye ndege kwenda kufanya semina mwezi mzima nje ya nchi?" alihoji.
Alisema wizara imechukua hatua kwa kuzifanyia kazi bajeti za mashirika yote ya umma ikiwa ni hatua ya kupambana na matumizi yasiyo na lazima.
"Tulitaka kubadilisha sheria watu wajanja wajanja wakatuzidi nguvu ndani ya Bunge, tulitaka fedha yote ya ziada na matumizi yasiyofaa yaende kusaidia Watanzania walio maskini,"alisema na kuongeza;
"Hatuwezi kukimbizana na wajane kwa kutaka Sh20,000, ikiwa kuna wafanyabiashara wakubwa wanakwepa kodi ama kuna mashirika yanatumia fedha zake katika anasa," alisema.
Makusanyo ya kodi
Alisema kunatakiwa adhabu kali sana kwa watu wanaokwepa kodi.
Alisema nchi za ughaibuni hakuna msamaha kwa mtu ambaye anakwepa kodi.
"Wenzetu mtu anayeheshimika anaweza kurudi kuwa zero kwa kukwepa kodi. Kwa hiyo kama tunataka kuongeza mapato lazima adhabu ziwe kali kwamba ukikwepa kodi hakuna dhamana,"alisema na kuongeza;
"Tutaziba mianya ya mtu kukwepa kodi na kudunda mitaani. Haya ni baadhi ya mambo ambayo mimi nayaangalia kama Taifa kwa miaka tunayokwenda."
Alisisitiza badala ya mtu aliyekwepa kodi kulipa malipo aliyoyakwepa tu, ashtakiwe na kufungiwa dhamana pamoja na adhabu ya kwenda jela.
Alisema hatua nyingine ni ya kuchukulia hatua kali watu wote watakaobainika kutumia vibaya kodi ili kuondoa kufanya kazi kwa mazoea.
Alisema pia kinachotakiwa kufanyika ni kuimarisha usimamizi, uwajibikaji, vita dhidi ya rushwa.
Alisema baada ya kumalizika mchakato zitatengenezwa upya sheria ambazo zitaainisha mambo hayo.
"Naomba Mungu ifike siku moja na ningetamani sana mtu ajutie kukwepa kulipa kodi na pia akwepe kutumia kodi za walalahoi kwa ubadhirifu. Nafsi yake imwonyeshe kuwa kutumia kodi za wananchi kwa ubadhirifu ni kosa kubwa sana,"alisema na kuongeza angetamani mianya rushwa izibwe.
Chanzo: Mwananchi