OKW BOBAN SUNZU
Platinum Member
- Aug 24, 2011
- 52,045
- 114,509
WANAOFUATILIA vema siasa za Tanzania watakumbuka vizuri enzi za ‘ugaidi’ wa Chadema. Kwa bahati mbaya, mmoja wa makada wa CCM ‘walioshikilia bango’ tuhuma hizo za ugaidi alikuwa Mwigulu Nchemba, ambaye kwa sasa ndiye Waziri wa Mambo ya Ndani. Pengine ni kutokana na hali hiyo, inawezekana kujitokeza hisia, miongoni mwa wafuasi wa vyama vya upinzani kuwa “wasiyempenda kaja.”
Kwa kuzingatia historia yake huko nyuma, Mwigulu kama waziri mwenye mamlaka ya utendaji katika Jeshi la Polisi anaweza kutumia fursa hiyo kudhibiti vilivyo vyama vya upinzani na kibaya zaidi, uteuzi wake umekuja katika wakati ambao uhusiano kati ya Serikali ya Rais Magufuli na CCM, kwa upande mmoja, na wapinzani kwa upande mwingine, si mzuri.
Katika makala yangu ya wiki iliyopita niliyataja makundi mawili yanayofanya kila jitihada kustawisha siasa za mfarakano, ambayo ni kundi la viongozi wa vyama vya siasa na baadhi ya wafuasi wa vyama hivyo.
Kwa mfano, uamuzi wa Bunge kuwafungua baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani ni dhahiri uamuzi huo utaathiri wananchi na si wabunge wanaowawakilisha. Kwa nini busara haikutumika hapa angalau kuwaonya wabunge hawa?
Baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani na kulifanya suala la vita dhidi ya ufisadi kuwa ajenda yake kuu, kulianza kujitokeza hisia kuwa upinzani utadhoofika kwa sababu suala hilo ndilo limekuwa turufu yao kuu. Sasa sijui ni kitu gani kimetokea, ghafla inaonekana kama CCM inawatafutia wapinzani hoja. Na hoja inayoonekana sasa ni kama kuna unyanyasaji dhidi ya vyama vya upinzani.
Kuanzia suala kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge na baadaye kupiga marufuku maandamano na mikutano ya siasa ya vyama vya upinzani ni mambo yaliyochangia kubadili hali ya awali ya wapinzani kukosa ajenda.
Tumeona Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akikamatwa lakini pia Kiongozi Mkuu wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe, naye akihojiwa polisi kwa madai kuwa ametoa hotuba ya kumkashifu Rais Magufuli.
Na wakati nikijiandaa kuandika makala hii, sio tu kuwa kongamano la chama hicho kujadili bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 lilizuiliwa na Jeshi la Polisi lakini pia polisi wanaendelea kumfuatilia Zitto. Kwa lipi hasa?