Mwenye nyumba ataendelea kulala?

Sokomoko

JF-Expert Member
Mar 29, 2008
1,915
129
Mwenye nyumba ataendelea kulala?

Jenerali Ulimwengu Aprili 9, 2008



KATIKA hatua niliyofikia katika mjadala wa uongozi wetu, hivi sasa inawezekana kufanya majumuisho ya vipengele nilivyovijadili, ili niweze kujenga taswira ya jumla ya hali ya kisiasa ilivyo leo na kuonyesha nani amesukumwa na nini kuchukua mtazamo gani.

Kwanza: kwa makusudi kabisa ya watawala wetu tumeingia katika mfumo tasa, unaoitwa “wa vyama vingi” bila kujali kama unaimarisha demokrasia au la. Kwa kujua kwamba upinzani katika mazingira yetu ungekuwa dhaifu katika kipindi cha mwanzo, watawala walijiona kama waliopata fursa ya kuwaridhisha “wafadhili” kwa kuwaonyesha picha ya “vyama vingi”(kama walivyotaka wenyewe) huku watawala wakihakikisha kwamba mfumo huo hautoi fursa ya kujenga demokrasia ya kweli.

Kutokana na vipengele fulani vilivyong’ang’aniwa na watawala wetu, wananchi wamenyimwa haki zao za kimsingi kabisa kwa kisingizio cha hivyo “vyama vingi.” Kwa mfano, ipo sababu gani ya kumkatalia Mtanzania kushiriki katika mchakato wa kupata nafasi ya uongozi hadi awe na chama cha siasa alichojisajili nacho?

Hii imekuwa na maana ya kuwafanya Watanzania wasiotaka kujiunga na chama cho chote wawe ni nusu raia, au hata chini ya hapo. Wapo wengi, pamoja na asasi kadhaa, wamelipigia kelele hili, lakini watawala, kwa mantiki ya kutoka wapi, sijui, wameziba masikio. Hata mahakama ilipoelekeza kwamba marekebisho yafanywe katika eneo hili, bado watawala walitumia mbinu za ujanja kuendeleza utaratibu huo batili.

Yapo pia masuala mengine mengi yanayohusu ujenzi wa demokrasia (nitayajadili mbele ya safari) lakini ambayo watawala wetu hawataki kuyagusa kwa sababu wanaamini mfumo tasa uliopo sasa utawafaa, na hili si kweli, kama nitakavyoonyesha baadaye.

Pili: Kutokana na kisingizio cha mfumo wa “vyama vingi,” viongozi mbali mbali katika ngazi zote wakazibwa midomo wasiweze kuyasemea masuala yanayolihusu Taifa kwa maelezo kwamba kukosoana hadharani kutawasaidia wapinzani, ambao wao kazi yao rasmi ni kuikosoa, kuidhoofisha na hatimaye kuiondoa madarakani serikali iliyopo madarakani.

Kwa mfano, wabunge wa chama-tawala walijikuta wakikaa kimya kwa kila jambo muhimu, wasithubutu kutoa maoni yao kwa uwazi na uhuru. Wakabakia kuremba maneno na kujipendekeza kwa wakuu wa serikali, kama si kuzungumzia masuala finyu yanayohusu maeneo wanayoyawakilisha.

Hata asasi za chama-tawala ambazo hapo zamani zilikuwa na uhuru wa kuchukua misimamo tofauti angalau na serikali, nazo zikajifunza kukaa kimya na kuangalia mambo yanayotendeka kama vile hayana uhusiano na kazi za asasi hizo. Umoja wa Vijana, Umoja wa Wanawake, na Umoja wa Wazazi, zikawa ni asasi za ki-dola, kama chama chenyewe. Hata zile kelele za vijana zilizozoeleka zikanyamaa.

Sharti mojawapo kubwa la kufinya uhuru wa wanachama katika ngazi mbali mbali kujisema watakavyo, ni kwamba watapata fursa ya kusema “mpaka wachoke” katika vikao vya ndani ya chama. Lakini vikao hivyo havikutoa mwanya wa mjadala wa aina hiyo, na pale wabunge “walipomchokoza” Bwana Mkubwa wa wakati huo kuhusu mikataba ya TANESCO alikigeuza kikao chao kuwa ni darasa la kuwafundisha jinsi ambavyo angeweza kuwamaliza kisiasa. Wakaufyata, kama chambilecho Waswahili.

Hilo ni tatizo la kutaka kutumia mifumo ya wenzetu bila kuelewa ni vipi inafanya kazi ili kulinda utangamano na maelewano ndani ya chama. Katika hili wakuu wa chama-tawala walishindwa kuona athari ya kuweka makatazo yasiyokuwa na matoleo ya kupumulia, na matokeo yake ikawa ni kuwaziba pumzi wabunge wake na viongozi wengine katika ngazi mbali mbali.

Tatu: Kwa kuwa, kutokana na hayo hapo juu, chama-tawala kilikwisha kujitoa katika mjadala wo wote wa hadhara kuhusu masuala makuu ya kitaifa, vyama vya upinzani, pamoja na uteke wake, vikajikuta vimeachiwa nafasi ya kutamba kwa kuyachukua masuala yote ambayo wabunge na viongozi wengine wa chama-tawala walikuwa hawathubutu kuyagusa na kuyafanyia kazi, kwa kuyaanika hadharani katika vikao vya Bunge na kwingineko.

Baada ya muda si mrefu ikaanza kujitokeza taswira inayostahili kuchunguzwa: kwamba wabunge pekee wanaozungumza mambo ya maana, masuala makuu yanayolihusu Taifa ni wale wa upinzani, pamoja na uchache wao na uchanga wa wengi wao kiumri. Hivyo ndivyo walivyozaliwa akina Zitto Kabwe na Wilbroad Slaa na wabunge wengine wachache wa upinzani ambao hawajai hata kiganja.

Kwa kila mwenye macho na masikio imekuwa ni dhaihiri kwamba umekuwapo ushirikiano mkubwa baina ya wabunge wa chama-tawala na wale wa upinzani. Hili wala halishangazi, kwani, kama nilivyoandika huko nyuma, wengi wao ni wazalendo, wana uchungu na nchi yao lakini wanakatishwa tamaa na mfumo unaowazuia kusikika wakikemea mambo yanayofanyika na watawala.

Nne: Kutokana na makundi mbali mbali ndani ya jamii kuchoshwa na jinsi mambo yanavyoendeshwa, ikazuka asasi mpya ya wapiga-filimbi, ambao kimsingi, wana fursa ya kuona maovu yanayotendeka na jinsi yanavyoliumiza Taifa. Wengi wao wanasukumwa na uzalendo (japo wapo wengine wana lao jambo) kuhakikisha taarifa hizo zinatoka hadharani ili wananchi wajue, na inapowezekana, hatua zichukuliwe kurekebisha hali.

Kazi ya wapiga-filimbi haiwezi kukamilika bila kuwahusisha wawakilishi wa wananchi (wabunge) na kuvihusisha vyombo vya habari, na pia kuzihusisha asasi za wanaharakati ambao ndio wapiga-debe wakuu wa masuala yanayowahusu. Kwa njia hii, ukazaliwa muungano mtakatifu ambao umefanya kazi kubwa ya kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala mengi, na pia kuhusu haki yao ya kusaili yanayofanywa na watawala.

Tano: Labda hili halikutarajiwa na watawala wetu, lakini matokeo ya mpangilio huu ni kwamba wawakilishi wa wananchi kupitia chama-tawala, pamoja na wingi wao kwa idadi, walijikuta katika uchache wa baraka za wananchi kwa sababu ndogo tu: wabunge wanaosikika wakitetea maslahi ya Taifa ni wabunge wa upinzani, pamoja na uchache wao kiidadi.

Wabunge na viongozi wengine wa vyama vya upinzani walipoamua “kwenda kwa wananchi” kuwashitakia matendo ya wakuu wa serikali ya CCM, waliwakuta wananchi waliokuwa tayari kuwasikiliza na kuyatia maanani maelezo yao. Hivyo ndivyo ilivyokuwa hadi wakuu mbali mbali wa chama-tawala na dola yake wakajikuta wakizomewa na wananchi vijijini, jambo ambalo halikuwahi kutokea huko tulikotoka.

Hiyo si hali nzuri kwa mwakilishi ye yote anayetaraji kuchaguliwa tena katika uchaguzi ujao, na ukitokea uasi miongoni mwa wabunge wanaojikuta katika hali hiyo haishangazi.

Sita: Bunge lilipokutana kujadili taarifa ya kamati teule kuhusu kashfa ya Richmond, hali ninayoieleza hapo juu ilikwisha kukomaa kiasi kwamba wabunge waliojipambanua kwa ukali walikuwa ni wa kutoka chama-tawala, akina Christopher ole Sendeka, Anne Kilango na wengine. Wapole walikuwa ni wabunge wa upinzani.

Uchungu wa kunyimwa haki ya kujadili masuala muhimu? Wasiwasi kwamba majimbo yatayoyoma mwaka 2010 kwa wapiga-kura kuwaona wabunge wa chama-tawala hawana maana? Wivu kwa wakuu wa serikali waliochukua nafasi zilizokuwa zikimezewa mate na wengi? Malipo ya madeni ya kisiasa yaliyolimbikizwa tangu kale?

Hatuwezi kujua kwa uhakika, lakini ukweli ni kwamba katika Bunge hilo ule mwamba unaoitwa CCM ulidhihirika kuwa na nyufa nyingi zilizochimba hadi ndani.

Saba: Katika sakata hili hatuna budi kuitafakari nafasi ya Spika wa Bunge, na jinsi aliyekalia kiti hicho kwa sasa, Samuel Sitta, alivyoongoza shughuli za Bunge katika kipindi hicho kuelekea “Taarifa ya Mwakyembe.”

Katika Bunge linalotakiwa kuwa muhimili wa uwakilishi wa wananchi lakini lililoegemea upande wa chama kimoja, kazi ya Spika inaweza kuwa tata. Chama chake ndicho kimempa uspika, na hilo lazima alikumbuke, kwani kinadharia kinaweza kumwondoa. Lakini wakati huo huo hana budi kuwekeza kwa makini katika nguvu za Bunge kwani hapo ndipo anapopata uzito wake kama mkuu wa muhimili huo wa dola.

Baada ya tetesi za muda mrefu kuhusu migongano baina ya Spika na baadhi ya wakuu wa serikali hii ilikuwa ni nafasi ya Sitta kuonyesha kwamba Bunge na mkuu wake si mbwa kibogoyo. Kwa kuteua kamati yake na kuipa madaraka kamili ya kufanya uchunguzi wa kina; kwa kuikubali taarifa ya kamati kama ilivyoletwa bila kuonyesha kuwa kamati ilimhoji mmoja wa wahusika wakuu wa sakata zima (Waziri Mkuu), Spika wa Bunge alikuwa amethibitisha nguvu ya hali ya juu ya Ofisi ya Spika, na (kwa njia ambayo nitaijadili baadaye) Bunge kwa ujumla.

Nane: Yote haya yanaashiria kwamba mambo yamebadilika kiasi kwamba tunaweza kusema leo kwamba hayatarejea kuwa kama yalivyokuwa zamani. Damu ilimwagika (kisiasa) katika kikao kile cha Bunge, na tabia ya damu ni kwamba huita damu nyingine. Je, huu ndio mwanzo wa chama-tawala kujitafuna chenyewe? Ni kiasi gani rais Jakaya Kikwete amedhoofishwa na damu hiyo iliyomwagika , au, kama si hivyo, tunaweza kuamini kwamba damu hiyo imemletea utakaso? Lakini, iwapo damu (hasa ya kisiasa) huita damu nyingine, ni shingo ya nani itatafutwa sasa?

Tisa: mojawapo ya matatizo ya uongozi wetu kwa muda mrefu ni kutofanya tafakuri endelevu, kwa maana ya kulichunguza, kulitafiti na kulisaili jambo katika hatua zake zote za kimantiki hadi hitimisho lake, na kuliandalia mikakati inayoendana na tafakuri hiyo. Tumezoea kuenenda kwa mishtuko na milipuko ya kipindi hadi kipindi.

Inawezekana hii ya Richmond ndiyo “imetoka,” chambile cha watoto wa kijiweni. Lakini, kwa mwenye akili, haijatoka, itarejea kutunyima usingizi. Aidha, itajitokeza tena katika mikataba mingine mingi, na katika matendo mengi yaliyofanywa na wakuu wa dola huko nyuma. Utawala huu unao ubavu wa kuyakabili haya na kuyachukulia hatua mjarrab? kwa sababu:

Kumi: Wiki jana,Joseph Mihangwa ameandika, “Minyukano ya mafisadi yamwamsha mwenye mali.” Ni kweli. Mwenye mali ameshituka kutokana na kelele za mafisadi wanaogombania mali zake. Sasa anataka kujua ukweli mzima kuhusu si tu hizi mali wanazogombania leo, bali zile nyingine ambazo ameanza kusikia wamekuwa wakinyang’anyana kwa muda sasa, bila yeye kujua.

Huyu mwenye mali ni masikini sana, yu hohe hahe. Kwa muda mrefu aliamini kwamba yeye ni masikini kwa sababu alikuwa hana kitu. Sasa anajua ana kila kitu ila anaporwa na wajanja aliowaweka madarakani yeye mwenyewe.

Mwenye mali sasa anao watoto waliofikia umri wa kupiga kura, na wanauliza maswali magumu magumu. Nani atahimili ghadhabu zao? Au bado tunasema kwamba kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala. Mwenye nyumba wa ajabu!

Source: Raia Mwema
 
mkuu hizi habari nyengine ukileta basi uwe unaandika ur analysis au ufahamu wako japo 2lines(ni mtaZAMO wangu mie tu huo).

naona unafanya mambo ya COPY PASTE.
 
mkuu hizi habari nyengine ukileta basi uwe unaandika ur analysis au ufahamu wako japo 2lines(ni mtaZAMO wangu mie tu huo).

naona unafanya mambo ya COPY PASTE.


Sidhani ni lazima nifanye utakavyo mie naona bora nifanye nitakavyo kwani napenda kuwa mimi na bora niache nifanye kama mimi kwani siwezi kuwa kama wewe. Wewe Eng bwana mie mtu mdogo sana kwahiyo wewe utabaki kuwa wewe na mimi nitabaki kuwa mimi I hope u gt the point.Tchao.
 
Back
Top Bottom