BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,007
Mwema akiri uwezo wa Polisi mdogo
Gloria Tesha
Daily News; Tuesday,January 13, 2009 @20:00
Gloria Tesha
Daily News; Tuesday,January 13, 2009 @20:00
MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, amekiri kuwa uwezo wa Polisi kuhimili ajali za barabarani ni mdogo kutokana na askari wengi kushindwa kufanya kazi kwa umahiri na taaluma. Kutokana na hali hiyo, Mwema ameahidi kutoa tamko lenye mwelekeo wa namna walivyojipanga kuzuia ajali za barabarani nchini.
IGP alisema hayo jana katika taarifa yake ya mradi wa ujenzi wa nyumba mpya za makazi za polisi wa kambi ya Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye aliweka jiwe la msingi la ujenzi huo.
Mwema alisema alisikitishwa na taarifa za ajali ya juzi Tanga iliyosababisha vifo vya watu 28 na wengine 22 kujeruhiwa vibaya na ya Uchira, Kilimanjaro siku chache zilizopita na kusababisha vifo vya ndugu 11, kuwa ni ishara kwamba bado tatizo lipo.
Alisema matatizo hayo wakati mwingine hutokana na baadhi ya askari kutokuwa mahiri katika kufanya kazi kitaaluma, hivyo nia ya Polisi ni kuhakikisha mihimili yake mikuu ambayo ni Weledi, Usasa na Ulinzi Shirikishi, vinakuwa na tija kwa jamii.
Mwema alisema miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele na Polisi ni kuhakikisha ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao, ikiwa ni pamoja na kulinda usalama wao barabarani kwa kuzuia ajali zitokanazo na uzembe wa ama madereva, abiria au polisi.
Wakati tunafurahia maendeleo ya nyumba hizi za askari bado Watanzania wenzetu wanaendelea kupoteza maisha kwa ajali za barabarani, naweza kukiri kuwa bado kiwango cha kuhimili ajali za barabarani ni kidogo ila tunaendelea kushughulikia suala hilo ipasavyo, alisema Mwema.
Akizungumzia suala hilo, Rais Kikwete alitumia fursa hiyo kuwapa pole walioguswa na ajali hiyo kwa kupotelewa na ndugu zao na majeruhi waliopo hospitalini na kuahidi kuwa Serikali inawajali wananchi wake, hivyo itaendelea kufuatilia na kusisitiza usalama barabarani.