Mwanao (Soma muhimu)

Mwanao (Soma muhimu)

Nicodemas Tambo Mwikozi

JF-Expert Member
Joined
Aug 13, 2016
Posts
663
Reaction score
1,047
MWANAO

Ipo siku utakuja kupata mtoto. Itakuwa ni siku ya furaha kubwa sana kwako na jamaa zako. Mtoto utakayempata ataongeza thamani na ladha maishani mwako.

Kila utakapomuona utakuwa huamini kama huyo mtoto ni mali yako mwenyewe. Kuna hali itakujia na kuhisi kama vile umeazimwa, kwamba iko siku huyo mtoto atakuja kuchukuliwa na wenyewe.

Lakini ukweli utabaki kuwa hivyo, huyo ni mwanao, damu yako, zawadi yako. Na siku zinavyozidi kwenda utazidi kufurahia anavyokua na jinsi unavyozidi kufanana naye; macho, masikio, komwe, meno nk.

Utafanya kazi kwa bidii kuhakikisha mwanao anaishi maisha mazuri kwa kumtimizia mahitaji yake ya msingi.

Furaha yako kubwa itakuwa imeshikiliwa na ustawi bora wa mwanao. Afya yake ikitetereka, amani itatoweka na nyumba yako itazizima.

Utakesha na kusulubika kwa kila hali kuhakikisha jambo baya halimkuti mwanao. Utafanya hili na lile, ikiwemo kuhatarisha afya na usalama wako kuhakikisha mwanao anakula vizuri na kuvaa vizuri.

Siku zote utatamani akue haraka, ili uweze kuongea naye, utembee naye na kucheza naye. Utatamani aanze shule haraka, awe anakuwa wa kwanza kati ya wanafunzi wenzake.

Utaona fahari kusimulia sifa zake, utundu wake, ujanja wake na werevu kwa ndugu na rafiki zako.

Hata baada ya kumaliza elimu yake, ndoto yako kwake itakuwa kumwona akiendelea vizuri katika hatua nyingine ya kuanza kujitegemea.

Utampa sapoti ya hali na mali kuhakikisha anakuwa mtu thabiti mwenye kujitambua na kutambuliwa pia na jamii inayomzunguka. Na hivyo sifa njema za mwanao, kuanza kukurudia wewe.

Hata atakapofikia hatua ya kupata mwenzi wa maisha yake, utakuwa mwenye amani kubwa kwa kuhakikisha mwanao ameangukia kwenye mikono salama.

Utawapa baraka zako na utawaona wote kama wanao. Utawaombea uzao bora na maisha mema huku ukiwarithisha kila chema ulichojaaliwa kuwa nacho.

Hata ukibahatika kuufikia uzee, uzee wako utakuwa wenye amani kubwa, hasa kwa kuzingatia alama ya uthabiti na ubora uliyoiacha kwa mwanao. Na muda ukifika wa kurudi mavumbini, utalala ukiwa mwenye amani.

UPANDE WA PILI

Mwanao atakapofikia umri wa miaka 16 anaweza akawa ameshakubuhu kwenye wizi na uvutaji bangi. Magenge ya wahuni na vibaka yatakuwa yamemvuta na kushikilia ufahamu wake kiasi ambacho hatakuheshimu wala kujali maonyo yako.

Mwanao aweza kuwa tishio kwa majirani na kwako mwenyewe. Utasononeka na kukonda kwa kihoro, huku ukijiuliza ulikosea wapi?

Kisha siku moja utasikia mwanao ameuawa kikatili na raia wenye hasira kali na kuchomwa moto.

Maiti yake itakuwa haitambuliki kwa jinsi ilivyochakazwa kwa mchanganyiko wa moto na kipigo. Utalia sana na kuumia moyo, maana uchungu wa huyu mtoto unaujua wewe, kwa vile ni damu yako.

Lakini hatarudi na historia haitabadilika.

Tena binti yako umpendaye sana kiasi cha kumrithisha jina la mama yako mzazi, bibi yake; afikapo umri wa miaka kumi na tano tu anaweza akapewa mimba na safari yake ya elimu ikaishia hapo. Utaanza kulea mjukuu asiye na baba.

Saikolojia ya binti yako inaweza kuharibika, kwani baada ya miaka minne au mitano wakati ukihangaikia kumtafutia biashara ya kufanya au kumpeleka kozi ya ufundi na stadi za kazi, atapata mimba nyingine atakayopewa na mume wa mtu.

Mtahangaishana huku na kule lakini mwisho wa yote itakubidi utunze mwana na mjukuu.

Kutokana na ugumu wa maisha na mabadiliko ya mfumo wa siasa na uchumi wa nchi, itampasa binti yako kuanza kujitegemea.

Elimu duni aliyonayo itamtosha kwenda kupata kazi ya uhudumu kwenye baa. Kazi hiyo hautakubaliana nayo lakini bado hautaweza kumzuia mwanao kufanya kazi hiyo, kwani ndiyo kitu pekee anachokiweza kwa wakati huo.

Pamoja na kwamba ni ajira, kazi hiyo itamfanya bintiyo kwa upande fulani ajihusishe na ufuska.

Ujira mdogo na hali ngumu ya maisha itamfanya asichague mwanaume wa kulala naye, isipokuwa uwezo wa mfuko wake.

Haya yote utayajua na yatakuumiza nafsini, hasa ukikumbuka udhalilishaji na uonevu wanaokumbana nao mabaamedi, lakini utakaa kimya na kufa kikondoo.

Zaidi, binti yako anaweza kukutana na mwanaume mwenye uwezo wa kifedha lakini asiye na adabu wala nidhamu.

Mwanaume mchafu na mshenzi, lakini kwa kuwa binti huyu uliyempenda sana, moyo wake utakuwa umeangukia huko hautakuwa na kauli ya kupingana naye. Utamuacha aolewe.

Ndoa itakayogeuka kuwa chuo cha mateso kwa mwanao kutokatana na vipigo na udhalilishaji mkubwa kutoka kwa mkweo ambaye hata hivyo wala hatakuwa anakuheshimu wala kukuogopa.

Siku moja binti yako aliyekuwaachia wajukuu kadhaa atapigwa na mumewe kiasi cha kupoteza maisha.

Ni kweli sheria itafuata mkondo wake, lakini mwanao hatarejea. Atakuwa amekufa.

Wakati wa kumuaga utatoa machozi mengi, hasa utakapomuona alivyolala kwa utulivu ndani ya jeneza. Utaliona komwe lake, na pua yake, ambayo watu wengi walizoea kukwambia kuwa alivichukua kwako.

Utakumbuka jinsi alivyozaliwa kwa taabu. Jinsi ulivyomlea kwa taabu, jinsi ulivyohangaika kumsomesha huku ukiwa na ndoto za kumuona akija kuwa mtu mkubwa baadaye.

Ndoto ambazo zitakuwa zimeishia kwenye sanduku hilo huku akiwa na ngeu kadhaa usoni mwake. Simanzi na donge la uchungu vinaweza vikakuua.

Kuna namna nyingi ambazo mwanao anaweza kuja kukudisappoint, ambazo zitageuka maumivu kwako.

Mapenzi na uchungu wa mzazi kwa mtoto wake huwa hayaishi. Mzazi yeyote anapenda kumuona mwanae akiwa na mustakabali wenye tija.

Na zaidi mzazi yeyote anapenda kuwa karibu na mwanae ikiwezekana mpaka siku ya kifo chake. Lakini hayo hayaji kwa nasibu.

MASWALI

1) Je, unajua nafasi ya mzazi wako kwenye maisha yako? Wajua kama hivi ulivyo leo ni matokeo ya msimamo wa mzazi wako?

2) Je unajua kama mzazi ni Mungu wa Pili duniani? Unatambua thamani na maana ya kuwa baba au mama wa mtoto wako?

3) Je, wajua kama mustakabali wa mwanao, kitabia, mwenendo na mitazamo inachangiwa kwa asilimia kubwa na wewe kama mzazi?

4) Je, wajua kuwa unapomdharau mzazi wako na kumpa nafasi ya mwisho inampa simanzi kubwa katika moyo wake? Je, wajua kuwa wanao pia watakuja kukufanyia hivyo hivyo?

5) Je, unaweheshimu wazazi waliokuzalia mwenzi wako? Unahisi wanakushukuru kwa wewe kuishi na mtoto wao au wanajuta kukufahamu?

6) Bila kujali unavyompenda, unavyomuhitaji na jinsi ulivyohangaika naye, kuna siku binti yako anaweza kutaka kujiua au kujiua kabisa kwa sababu ya mapenzi. Utafanyaje? Umeanza kuchukua hatua za kumjenga mwanao leo kisaikolojia kumuepusha na hiyo zahma?

Bibi yangu anakaribia umri wa miaka tisini lakini mpaka leo, huwa anakumbuka mausia ya baba yake aliyefariki miaka zaidi ya hamsini iliyopita. Nilikuwa nashangaa nilipomsikia anasema, baba yangu alikuwa hapendi kabisa tabia za aina hii.
Au anasema, baba yangu aliwahi kuniambia kuwa.

Huwa nashangaa. Baba yako aliyefariki miaka ya sitini !? Bado unamkumbuka? Bado unashikilia mausia yake ilhali na wewe umeshazeeka hivi?

Lakini leo nimeng'amua kuwa mzazi mwenye mawazo chanya, msimamo thabiti na kujenga misingi imara ya malezi kwa mtoto wake ana nafasi kubwa ya kumjenga mtoto wake katika misingi imara siku zote za maisha yake.

Upendo wako, mtazamo wako, msimamo wako na mausia yako kwa mwanao, vinaweza kuwa katiba isiyobadilika kwa mwanao hata utakapokuwa umeaga dunia.

Hali kadhalika, mzazi dhaifu, asiyejitambua na asiye na msimamo ana nafasi kubwa ya kujenga kizazi cha watoto wasiojitambua, dhaifu na wasio na msimamo maishani. Na hatakumbukwa kwa lolote.

Nakutakia kila la kheri! Kwa Niaba ya kaka yangu Foroy Foroy nawasalimu Kutoka Milima ya Lushoto

FB_IMG_1574380305943.jpeg
 
Tangu upara wako uote nywele wikolo umekua na akili somehow. Ama kweli akili ni nywele.
 
Back
Top Bottom