Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,284
Unapojua ukweli, kisha sikiza urongo,
Ni raha utakubali, kumsikiza mrongo,
Mara lile mara hili, ushasoma lake lengo,
Tulia mwanangu tuli, sijaribu toa nyongo.
Mwana sikiza urongo, zingatia ilo kweli.
Wata amalize yote, naomba sitie neno,
Ya unguja hata Pate, ayaseme kwa mawano,
Kumbe umepita kote, na ukafanya kigono,
Wazijua zake kete, mnase bila ndoano,
Mwana sikiza urongo, zingatia ilo kweli.
Afanye juu kupaa, mithili yake kwarara,
Usipatwe na fazaa, wala sifanye harara,
Atakuja tu kukaa, akiwa ameparara
Augulie kwa njaa, simpatie karara,
Mwana sikiza urongo, zingatia ilo kweli.
Mwana usiwe jununi, kusaka kuku njiani,
Haraka hasa ya nini, msubirie bandani
Ondoa shaka moyoni, jioni tarudi ndani,
Huishia ukingoni, mkimbia sakafuni,
Mwana sikiza urongo, zingatia ilo kweli.
Akisha tia kikomo, hapo mzodoe mato,
Soma yote yaliyomo, koma siseme mkato,
Siseme mumo kwa mumo, siogope piga kato,
Mfunde na mpe somo, ghururi hazina pato,
Mwana sikiza urongo, zingatia ilo kweli.
Dotto Rangimoto Chamchua
whatsapp/call 0622845394