Muuaji azirai baada ya hukumu

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
MWANAMKE mkazi wa Kijiji cha Musimihi, Tarafa ya Ilongero, Wilaya ya Singida, Juliana Ibrahim (52), ameanguka kizimbani na kisha kupoteza fahamu baada ya kuhukumiwa yeye na mtoto wake kutumikia miaka mitatu jela kila mmoja.

Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma inayoendelea na vikao vyake mjini hapa, ilimhukumu Juliana adhabu hiyo baada ya kukiri kosa la kumuua jirani yake, Maria Mussa, bila kukusudia kwa madai ya kunyimwa makande kwenye sherehe ya harusi.

Mshtakiwa alihukumiwa adhabu hiyo pamoja na mtoto wake, Pendo Yohana, ambaye naye atatumikia jela miaka mitatu kwa kukiri kosa hilo.

Ilidaiwa kuwa washtakiwa wote kwa pamoja, siku wanaanza kuishi mahabusu gerezani walikuwa na watoto wachanga na hadi jana wanahukumiwa, Juliana alikuwa bado anaishi na mtoto wake mahabusu.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa shtaka la mauaji ambalo walilitenda Agosti 5, 2006, wote kwa pamoja bila hofu kila moja kwa wakati wake, alikiri kosa hilo.

Awali, Mwanasheria wa Serikali, Ahmed Seif, alidai mbele ya Msajili wa mahakama hiyo, Renatus Rutatinisibwa kuwa, Agosti 5, 2006 muda usiofahamika, washtakiwa wote kwa pamoja walimpiga Maria na kusababisha kifo chake siku 27 baadaye.

Seif alidai kuwa, siku ya tukio, Juliana akiwa amefuatana na mtoto wake Pendo, walikwenda nyumbani kwa Maria, kumuliza sababu za kuwanyima makande kwenye sherehe ya harusi.

Seif alisema Maria aliwajibu kuwa hawezi kujibu swali hilo na kwamba, mwenye uwezo wa kulijibu ni Dilu Mohammed.

Alidai kuwa washtakiwa walikasirishwa na jibu hilo na kuanza kumshambulia.

“Mshtakiwa wa pili Pendo alimbana Maria na mama yake Juliana alipata fursa ya kumpiga ngumi sehemu mbalimbali za mwili, baada ya kupigwa sana alianguka chini,” alidai.

Seif alidai wakati washtakiwa wakiendelea kumpiga Maria, mtoto wake Joshua Yesaya, alipiga yowe.

“Uchunguzi wa daktari umeonyesha wazi kuwa kifo cha Maria, kimesababishwa na kuvuja kwa damu nyingi,” alidai Seif.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa kujitegemea mjini hapa, Raymond Kimu, aliomba mahakama kuwaonea huruma wateja wake kwa madai kuwa, wanafamilia kubwa zinazowategemea na wamekaa rumande zaidi ya miaka sita.

Akitoa hukumu hiyo, Rutatinisibwa alisema mahakama katika kufikia uamuzi wake, imezingatia maombi ya pande zote kwa makini.

Hata hivyo, Rutatinisibwa alisema kitendo cha kuua binadamu kwa sababu ya kunyimwa makande kwenye harusi, hakikubaliki.

“Kwa hali hiyo, mahakama inawapa adhabu ya kila moja kutumikia jela miaka mitatu ili iwe fundisho kwenu na watu wengine wanaotarajia kufanya makosa ya aina hii,” alisema.
 
Back
Top Bottom