Muswada wa Katiba utavuruga umoja wetu???

The Khoisan

JF-Expert Member
Jun 5, 2007
15,392
12,976
Muswada huu wa Katiba utavuruga umoja wetu

Monday, 11 April 2011 21:55 0diggsdigg


katiba.jpg
SASA ni dhahiri kwamba muswada wa marekebisho ya Katiba mpya unachukua mwelekeo wa kuvuruga umoja wetu na kutusambaratisha kama taifa. Tangu muswada huo uanze kujadiliwa na wadau mbalimbali takribani wiki moja iliyopita, jambo lililojitokeza waziwazi ni kuwa Watanzania wengi, pasipo kujali tofauti ya itikadi na imani zao, wameghadhabishwa na muswada huo kutokana na ukweli kwamba unabeba maudhui yenye lengo la kukidhi matakwa na maslahi ya watu wachache katika nchi yetu.
Pamoja na kuwapo mwangwi mkubwa utokanao na sauti za wananchi katika kila kona ya nchi yetu wanaoendelea kuupinga muswada huo, kikundi hicho kidogo cha watawala kinaendelea kuweka pamba masikioni na kusema kuwa wananchi watake wasitake, muswada huo ndio pekee utakaokuwa msingi wa mchakato utakaozaa Katiba mpya na Rais anafanywa kuwa alpha na omega.

Wananchi kwa ujumla wanasema kuwa hawakushirikishwa katika mchakato mzima wa kuandaa muswada huo, kwa maana ya kutoa mawazo yao ili yazingatiwe katika kutayarisha muswada huo. Huko Zanzibar, mijadala ya muswada huo imejaa vitimbi, ghadhabu na jazba kwa kiwango cha kutisha kiasi cha baadhi ya wananchi kuchana na kuchoma moto nakala za muswada huo mbele ya viongozi wa kitaifa wa Serikali ya Mapinduzi na ya Muungano.

Viongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na vyama vya CCM na CUF vinavyounda serikali hiyo wamekaa kimya. Kama tulivyosema hapo juu, bila shaka hali hii inachochewa na ukaidi wa kikundi kidogo cha viongozi wa Serikali ya Muungano – hasa kutoka Tanzania Bara – ambao wanaweka mbele maslahi binafsi kwa kuhakikisha kuwa Katiba mpya itakayotungwa inakuwa hati miliki yao.
Tumeshuhudia Wazanzibari wengine wakienda mbele zaidi kwa kusema kuwa hawautaki Muungano, kwa maelezo kuwa Zanzibar inaendelea kuburuzwa na kwamba mustakabali wa nchi yao bado unaamuliwa kutoka Tanzania Bara. Kwa vyovyote vile, haya ni madai mazito na ya msingi ambayo lazima yafanyiwe kazi iwapo tunataka Muungano uendelee kuwapo kwa utashi wa wananchi wa pande zote mbili.
Itakumbukwa kuwa madai hayo mazito yamepewa nguvu zaidi katika kujadili muswada huo wa Katiba mpya kutokana na kauli ya hivi karibuni ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kwamba serikali hiyo ilipeleka mapendekezo 14 katika Serikali ya Muungano kuhusu muswada huo wa Katiba mpya lakini ni mawili tu yaliyokubaliwa na hakuna sababu zilizotolewa kuhusu mapendekezo 12 yaliyokataliwa. Tukizingatia pia ukweli kuwa idadi ya mambo ya Muungano iliongezwa kinyemela kutoka 11 hadi 22 pasipo ridhaa ya Wazanzibari, ndio sababu mijadala ya muswada wa Katiba mpya imekuwa na mwelekeo huo.

Tangu mwanzo tulionya kuhusu uwezekano wa kusambaratika kwa taifa letu iwapo Serikali ya Muungano, chini ya Rais Kikwete, isingehakikisha kuwa mchakato wa kuwapatia Watanzania Katiba mpya haufanyiki kwa mizengwe na ujanjaujanja wa kutanguliza mbele maslahi na matakwa ya wachache. Tunashuhudia sasa jinsi serikali hiyo inavyofanya juhudi za makusudi kutisha wananchi wasijadili na kutoa mapendekezo kuhusu Katiba wanayoitaka.

Ndio maana mijadala hiyo inafanyika Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar peke yake, tena katika mazingira ya vitisho vya vyombo vya dola vilivyosheheni silaha za kivita, zikiwamo mabomu ya machozi na risasi za moto. Badala ya kuruhusu wananchi katika mikoa yote wajadili muswada huo kwa uhuru, Serikali imeona ikifanya hivyo ajenda yake ya siri itashindwa kwa sababu wananchi watapata muda wa kuuelewa muswada huo kwa upana zaidi na mwishowe wataukataa.
Na ndio hasa siri ya muswada huo kuletwa katika lugha ya Kiingereza badala ya lugha yetu ya taifa ya Kiswahili. Na ndio maana vyama vya siasa ambavyo ni wadau muhimu katika mchakato huo vimepigwa marufuku kuhamasisha wafuasi wake.
 
Back
Top Bottom