Mtoto huanza kupata hisia akiwa tumboni mwa mama yake

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,569
9,430
Kwa kipindi kirefu tangu enzi za kale, wazazi walijitahidi kuwalea watoto wao kwa lengo la kuwafanya wazingatie maadili mema. Walitaka watoto wao tangu wakiwa wachanga wafuate mila na destruri nzuri kwa kuzirithisha kizazi hadi kizazi. Mambo yaliyokuwa yakirithishwa ni lugha, maadili mema ya upendo, ushirikiano, uadilifu na pia ujasiri.

Madhehebu ya dini yalipowasili nchini kutoka nchi za nje, baadhi ya mila zilipigwa vita na nyingine ziliimarishwa. Malezi waliyokuwa wakitoa yalianza mapema tangu mtoto alipoanza kutambua mema na mabaya kwa maana ya umri wa miaka minne au mitano na kuendelea.

Hata hivyo yafaa tuelewe kuwa mtoto anaanza kupata hisia kabla hata hajazaliwa. Kwa mfano, utafiti uliofanyika huko Uingereza hivi karibuni ulibaini kuwa kitoto kichanga (Kijusi kwa lugha ya Kiingereza ni Foetus) ambacho bado kiko tumboni mwa mama yake kinaonyesha hisia za uchungu na hata furaha.

Huu ni utafiti uliofanyika huko Uingereza katika Vyuo Vikuu vya Durham na Lancaster. Iligundulika kuwa kijusi (kitoto kichanga) hujifunza kwa njia mbalimbali za mawasiliano. Utafiti huu ulifanyika kwa kuchunguza vijusi kwa njia ya ‘Ultrasound’ na kuviona vikitabasamu na pia kukunja nyuso.

Utafiti huu unatuelimisha kuwa kinamama wajawazito hawana budi kuachana na tabia ya kukasirika au kununa wakiwa na ujauzito.

Nakumbuka siku za nyuma wazazi wetu walituambia kuwa mama mjamzito akipita mahali kama shambani na akatamani kitu fulani kama tunda, aliruhusiwa kula bila kikwazo. Tamaa ya kupenda vitu vya aina fulani ilitokana na msukumo wa kichanga kilichomo tumboni.

Mtoto baada ya kuzaliwa huwa na hisia tofauti na mojawapo ya hisia anazokuwa nazo ni kulia. Je, kwa nini mtoto analia sana katika kipindi cha siku za mwanzo ya maisha yake? Ziko sababu nyingi na mzazi anatakiwa kuwa macho hasa kama ni uzazi wake wa awali.

Siku chache baada ya kuzaliwa kitoto kichanga hujikuta katika mazingira mapya. Hatua yake ya kwanza ya mawasiliano siyo kwa maneno bali ni kwa njia zisizo za maneno. Hawawezi kuonyesha dalili za kufurahi kwa maneno ila ni kwa tabasamu. Hisia za mtoto anapopata uchungu au hasira haziwezi kuelezeka ila ni kwa kulia. Mara nyingi watoto wanapolia huwa ni kero kwa wazazi.

Kwa kawaida tabasamu hupokelewa vizuri lakini kilio hakipokelewi vizuri.

Watoto wanaolia hakuna anayewajali na hujenga hisia za chuki na kutopendwa na hatimaye hujenga hisia za mwelekeo hasi. Ifahamike kuwa hisia za hasira na kutojaliwa kwa mtoto hujengeka hatua kwa hatua kwa kipindi kirefu na kumfanya mtoto ajenge hisia hasi.

Watoto wadogo kama walivyo watu wazima wana haki ya kusikilizwa. Wanahitaji kupendwa, kusikilizwa na kusaidiwa. Mtoto hueleza hisia zake kwa kumlenga mzazi katika kueleza mahitaji yake.

Kama mtoto analia mara kwa mara, ziko sababu mbalimbali zinazomsibu. Kwanza mtoto anaweza kuwa na njaa. Siku chache za kwanza tumbo la mtoto ni dogo hivyo huhitaji kupata maziwa kidogo kidogo lakini kwa utaratibu fulani mfululizo.

Sababu nyingine za mtoto kulia ni kiu. Ni wazazi wachache wanaotambua kuwa mtoto anahitaji maji. Mazingira ya sehemu za joto maji ni muhimu kwa watoto na pia kwa watu wazima hivyo ni muhimu kwa mzazi kuwa makini. Hata hivyo wako wataalamu wanaodai kuwa mtoto mchanga asipewe maji bali anyonye tu maziwa ya mama muda wote hadi anapotimiza miezi sita. Nadharia hii inapingwa na baadhi ya wazazi waliowapa maji watoto wao wachanga bila madhara yoyote.

Wakati mwingine mtoto analia anapokuwa hana raha kama anapojikojolea, anapokwenda haja kubwa au anapojisikia kuwa hana raha kwa kubanwa. Hajisikii raha na hivyo analia ili abadilishiwe mazingira yake.

Kwa maana hiyo, wazazi vijana wanashauriwa kuhudhuria kliniki mara kwa mara kabla na baada ya kujifungua ili kupata maelekezo muhimu ya kuwalea watoto wao wachanga.

Wataalamu wa saikolojia ya watoto wanashauri kuwa ni vyema kuwachunguza watoto wachanga ili kubaini wanachotaka na wanachokichukia. Wako wengine wanataka kula chakula cha aina fulani na kuchukia kula chakula cha aina nyingine.

Mama wengi hawana ukaribu wa watoto wao tangu wangali wachanga. Wanawaachia watoto wao waangaliwe na yaya jambo ambalo si jema. Wako yaya wasiokuwa na mapenzi na watoto.

Endapo mtoto hapendi kula, yaya hamjali. Matokeo yake mtoto anadhoofika kufikia hatua ya kuwa na tatizo la kiafya.

stephenjmaina1965@yahoo.com

smaina1@tz.nationmedia.com



source; Mwananchi
 
Back
Top Bottom