[h=2][/h] Jumanne, Agosti 28, 2012 05:49 Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Mchungaji Christopher Mtikila
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imeahirisha kusoma hukumu dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila hadi Septemba 6, mwaka huu.
Hukumu hiyo iliahirishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Mosha, baada ya Hakimu Mkuu Mkazi, Illivin Mugeta, anayeisikiliza, kutokuwapo mahakamani.
Kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya hukumu, hakimu anayesikiliza kesi hii amepata udhuru, hivyo itasomwa Septemba 6 mwaka huu, alisema Hakimu Mosha wakati akiahirisha shauri hilo.
Mtikila anakabiliwa na mashitaka ya kusambaza waraka wa uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete, kwamba anataka kuuangamiza Ukristo.
Mshitakiwa alifunga ushahidi kwa kuwa na mashahidi wawili wa utetezi, akihofia kupoteza fedha za Serikali kwa kuwaleta mashahidi wengi ambao hawana kitu tofauti na mashahidi wengine waliokuwa wamewasilisha ushahidi wao mahakamani hapo.
Mtikila, anadaiwa kwamba, Aprili, 2010 jijini Dar es Salaam, alisambaza waraka aliokuwa akidai ni wa kuunusuru Ukristo wenye lengo la kuangamizwa na Jihad ya Rais Jakaya Kikwete na kwamba Wakristo wajitoe muhanga kukomesha ugaidi.
Kikwete anaangamiza Ukristo, amekuwa jasiri wa kuingiza Uislamu katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alidai Mtikila katika waraka wake huo.
Alidai waraka uliosambazwa alisaini akiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya kuunusuru Ukristo na walichapisha nakala 100,000, lakini aligoma kutaja mahali walipochapishia nakala hizo.
Maelezo yote hayo yalitolewa mahakamani kama kielelezo na SSP, Ibeleze Mrema aliyemuhoji Mtikila Aprili 14, 2010 na alipotakiwa kueleza chochote kuhusu kielelezo hicho, mshitakiwa alisema hana swali na akakubali kipokelewe na mahakama.
Hata hivyo, akizungumza nje ya mahakama hiyo, Mtikila alisema yuko katika mikakati ya kuandaa waraka mzito kuliko aliouandaa mwanzo na kuwa chanzo cha yeye kufikishwa mahakamani hapo.
Alisema waraka huo utagusia rais anayestahili kuiongoza nchi kwa masilahi ya Watanzania.
[h=4]Toa Maoni yako kwa habari hii[/h]