Miongoni mwa vijana hao ni mtangazaji wa televisheni na mbunifu wa maudhui ya kidijitali kutoka Namibia, David Mbeha, ambaye hivi karibuni aliwasili Beijing kuendelea na masomo ya shahada ya uzamifu ya Usimamizi wa Biashara, huku akipanua wigo wake katika anga ya ubunifu wa kidijitali. Mbeha anasema alijua Beijing ni mahali sahihi kutokana na jinsi mji huo unavyokumbatia ubunifu wa kidijitali, uchumi wa kidijitali na maendeleo makubwa katika sekta ya teknolojia, hali inayompa fursa ya kuwa sehemu ya jamii pana ya wabunifu wa kidijitali.
Mbeha anaelezea hatua hiyo kama sehemu ya mkakati mpana wa binafsi na kitaaluma unaolenga kukuza mtazamo wa kimataifa na mageuzi ya ubunifu, hatua inayolingana na umuhimu unaoongezeka wa mawasiliano ya watu kwa watu kati ya China na Afrika. Tangu alipowasili Beijing, Mbeha alijikita haraka katika mfumo wa ikolojia wa ubunifu na vyombo vya habari wa China.
Anasema tangu alipofika Beijing, amepata heshima ya kuwa sehemu ya Tamasha la Kimataifa la Filamu la Beijing 2025 kama mwakilishi kutoka vyombo vya habari vya Afrika. Aidha, mwanahabari huyo alishiriki katika warsha ya biashara ya mtandaoni mjini Wuhan, ambako alitambuliwa kwa ujuzi wake wa matangazo ya moja kwa moja mtandaoni, akiakisi kukua kwa muingiliano kati ya vyombo vya habari, biashara na uvumbuzi wa kidijitali nchini China.
Hivi karibuni, Mbeha alishiriki katika mahojiano yaliyoandaliwa na kituo cha CGTN, akielezea safari yake binafsi na kitaaluma mjini Beijing, hatua iliyoweka alama muhimu katika taaluma yake ya uanahabari wa kimataifa. Anasema kazi yake katika ubunifu wa kidijitali na televisheni barani Afrika ilitambuliwa na CGTN, ambako alipata fursa ya kushirikisha safari yake katika sekta ya ubunifu na kuunganisha Afrika na China.
Uzoefu wa Mbeha mjini Beijing unaakisi mwelekeo mpana wa wabunifu vijana wa Afrika wanaojihusisha na vyombo vya habari vya kimataifa, uvumbuzi na mabadilishano ya kitamaduni. Kwa mujibu wa Mbeha, anapanga kubaki Beijing kwa kipindi kilichosalia cha masomo yake ya mwaka mmoja. Anasema kuwa, licha ya masomo, maisha katika mji mkuu wa China yamemsaidia kupanua mtazamo wake kuhusu utamaduni, chakula na mitindo ya mavazi kwa njia mpya. Kila siku kwake ni kama darasa la hali ya juu la uvumbuzi, kuanzia mambo madogo kama mifumo ya malipo hadi treni za kasi na ufanisi katika nyanja mbalimbali, huku akiwa na mengi anayotarajia kuyafanya mjini Beijing.
Kijana huyo anaamini safari yake inaweza kuwa chachu kwa vijana wengine barani Afrika wanaotamani kufanya kazi nje ya mipaka ya nchi zao. Kuja kwake Beijing ni mwanzo wa mabadiliko ya taaluma, na anatarajia kuwahamasisha vijana wengine wenye ndoto kuendelea kujiamini.
Matarajio ya Mbeha ni kuwa daraja kati ya bara la Asia na Afrika, hasa wakati China na Afrika zinajiandaa kupanua mabadilishano ya kitamaduni na ya watu kwa watu katika miaka ijayo. Anaamini kuna nafasi kubwa kwa Afrika na China kushirikishana ubunifu wao, huku Afrika ikichukua fursa ya uhusiano wake na China kujifunza kutoka maendeleo ya kipekee ya kiteknolojia ya China na namna nchi hiyo ilivyokumbatia uchumi wa kidijitali.