General Galadudu
JF-Expert Member
- Nov 7, 2015
- 1,868
- 2,200
Mmoja wa wahanga hao akiwa na majeraha mwilini mwake.
DAR ES SALAAM: Wakazi wa Chanika Mtaa wa Vikongolo B, Wilaya ya Ilala jijini Dar, wamevamiwa usiku wa manane wakiwa wamelala na baadhi kukatwa sehemu mbalimbali za miili yao huku anayedaiwa kuongoza kikosi hicho cha uvamizi akiwa anatamba mitaani akidai hakamatiki.
Waliojeruhiwa katika tukio hilo ni pamoja na Mfaume Said na Chacha Chacha ambao hali zao siyo nzuri kwani hawainuki vitandani na wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni hospitalini hapo, Said alisema ilikuwa Machi 9, mwaka huu saa saba usiku akiwa amelala nyumbani kwake alimsikia Chacha akipiga mayowe akihitaji msaada akaamua kutoka kwenda kujua kilichomsibu.
“Nilitoka kwangu nikiwa na mkanda wa jeshi mkononi, nilikuta kundi la watu wakiongozwa na mtu tunayemjua (jina tunalihifadhi) wakimkatakata Chacha kwa mapanga, ghafla walinigeukia, walinikata mguuni mara mbili na chini ya kwapa la kushoto nikaishiwa nguvu.
…..Akionyesha baadhi ya sehemu alizojeruhiwa.
“Chacha alipata upenyo, akakimbia na kujificha sehemu huku mwili wake ukiwa umeloa damu, mke wangu ndiye aliyepiga simu kwa mwenyekiti wa mtaa naye akawapigia polisi ambao walifika muda mfupi eneo la tukio lakini watuhumiwa walikuwa wameshakimbia,” alisema Said.
Said alidai kuwa mtu huyo aliyewashambulia aliwahi kuwavamia katika eneo hilo Septemba 11, mwaka jana saa sita usiku na akabomoa nyumba 152 bila kibali kutoka serikalini na mkuu wa wilaya akiwa na Kamanda Simon Sirro kabla hajawa kamishna wa kanda maalum ya Dar waliwasaidia chakula na kutaka sheria ichukue mkondo wake.
“Tunashangaa mtu huyo huyo ndiye amerudi kutukata mapanga na sasa yupo mitaani anatamba, namuomba Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, SACP Lucas Mkondya atusaidie kumkamata,” alisema Said.
Wananchi wa eneo hilo waliohojiwa na waandishi wetu, wamelaani kitendo hicho kwani familia za majeruhi hao wakiwemo watoto wao wanaosoma zipo katika hali mbaya kiuchumi.
Kamanda Mkondya alipoulizwa alisema wote waliohusika katika uvamizi huo wameshakamatwa.“ Kama kuna mwingine anaonekana mitaani taarifa itolewe polisi haraka ili waweze kutiwa nguvuni na sheria ichukue mkondo wake,” alisema kamanda huyo.