Msimu wa wapinzani kuhamia CCM na athari zake

Msimu wa wapinzani kuhamia CCM na athari zake

Rubawa

JF-Expert Member
Joined
Dec 25, 2015
Posts
2,055
Reaction score
3,267
Msimu wa wapinzani kuhamia CCM na athari zake

Na Ahmed Rajab

JUZI swahibu yangu mmoja alinambia bora serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ingetangaza kwamba Tanzania inaurejelea rasmi mfumo chama kimoja cha siasa, kilicho halali. Alisema kufanya hivyo angalau kutapunguza kubughudhiwa, kuumizwa na kuuawa, kwa wapinzani au wakosoaji wa serikali.

Aliongeza kwamba kutapunguza pia mihemko ya kisiasa na viroja vya baadhi ya viongozi wa upinzani waliogeuka na kuwa vinyago vya kisiasa.

Huyo rafiki yangu aliyasema aliyoyasema baada ya viongozi wawili wakuu wa upinzani kutimkia CCM kwa kasi kubwa wiki iliyopita. Wa kwanza alikuwa Julius Mtatiro, aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kilicho kitiifu kwa katibu mkuu Maalim Seif Sharif Hamad. Wa pili alikuwa Danda Juju, katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi.

Kabla ya hapo aliyekuwa makamu mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi (Bara), Leticia Mosore, alijiuzulu Julai 13, mwaka huu, na kurudi CCM. Baada ya hapo, Jumatatu ya wiki hii mbunge wa CUF Zubeir Kachauka alijivua uanachama wake na ubunge wake na akajiunga na CCM akipokelewa rasmi na katibu mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally katika makao makuu ya chama hicho.

Ninavyoandika makala haya kuna tetesi kwamba wabunge wengine wasiopungua watano wenye madeni au wasio na uhakika wa kuchaguliwa tena kuingia bungeni 2020, nao pia watajiunga na CCM.

Mtiririko wa viongozi wa upinzani walioamua kuchupa kutoka vyama vyao haukuanza jana. Inaonesha kuwa huu ni mkakati wa muda mrefu ulioandaliwa na CCM tokea 2016 na wenye lengo la kuvisambaratisha vyama vya upinzani na hatimaye kuuua upinzani pamoja na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

Kwa sasa, mfumo huo ndio wenye kuonekana kuwa na uwezo wa kuhakikisha kuwepo kwa tawala bora katika nchi mbalimbali barani Afrika. Na demokrasia tunayoizungumzia kwa sasa, katika kipindi hiki cha maendeleo ya Afrika, ni ile iitwayo “demokrasia ya kibwanyenye”. Demokrasia ya aina hiyo huwa inaongozwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Lengo la kila chama huwa ni kutaka kunyakua madaraka ya dola, kwa njia ya uchaguzi. Na lengo la kunyakua madaraka ni kukiwezesha chama kilichoshinda kitekeleze sera zake kama zilivyoainishwa katika ilani yake.

Kuna baadhi ya nchi ambako tofauti za vyama vya siasa huwa ni kubwa mno kwa sababu vyama hivyo huwa vinafuata itikadi za kisiasa zenye kukinzana. Nchini Tanzania vyama vinavyochuana kuwania madaraka havina tofauti kubwa za kiitikadi. Hakuna tofauti za kiitikadi wala za kimaadili baina vya vyama hivyo na CCM.

Tofauti iko zaidi katika utendaji, katika mchakato wa namna ya kuendesha serikali na jinsi ya kuwahudumia wananchi kwa kuzitekeleza sera za chama kinachotawala. Aghalabu, katika nchi zenye demokrasia isiyopevuka, chama kinachotawala hukerwa na wenye kuikosoa serikali yake. Kwa ufupi, chama chenye madaraka ya kuongoza serikali huuona upinzani kuwa ni adha.

Halafu huuona kuwa ni adui na hapo ndipo vyombo vya dola vinapoanza kuwashughulikia wapinzani au hata wakosoaji wa sera au wa utekelezaji wa hizo sera.

Tangu mfumo wa vyama vya siasa uliporejelewa katika nchi nyingi za Kiafrika katika miaka ya mwisho ya 1980 na ya mwanzo ya 1990 hadi sasa, hatuoni dalili za matumaini ya wananchi kufanyiwa kazi na kuwa mikakati mibadala ya kuleta mageuzi ya maana kwa maendeleo ya wananchi.

Nionavyo ni kuwa mkakati wa CCM wa kuuua upinzani ni wa ncha mbili: ncha moja imekuwa ikiulenga upinzani wa Bara na ya pili ule wa Zanzibar. Hadi sasa CCM imefanikiwa kwa wepesi kuwavutia viongozi wa upinzani wa Bara. Baadhi yao wanaonekana kuwa tayari kuichupia CCM kama bodaboda ya kuwafikisha watakakokwenda. Ushahidi uliopo unathibitisha hayo kwani waliohamia huko na kukumbatiwa na CCM wamefika walikotaka kufika: kwenye madaraka na uluwa. Hiyo ndiyo hakika ya mambo.

Wapinzani hao waliogeuka tunaweza tukawaita wazulufu. Si kwamba hawana mashiko lakini dhana iliyopo ni kwamba wanaweza wakanunuliwa kwa bei yoyote.

Ingawa dhana hiyo ina nguvu, hata hivyo hatuna ushahidi iwapo walisaidiwa katika safari yao kwa kupewa fedha, kwa kutunzwa bahashishi, au kwa vitisho vya aina fulani.

Pengine hayo si muhimu. Lililo muhimu zaidi na lenye kupaswa kuzingatiwa kwa makini ni huu “mchezo”, kwani umekuwa mchezo, wa wanasiasa wa upinzani kushawishiwa wahamie CCM. Mchezo uchezwao ni mbaya.

Kwa upande mmoja haya si ya kushangaza; si maajabu hata kidogo kwani takriban wapinzani wote waliorudi CCM ni kama watu wanaorudi kwao. Walipata malezi yao ya kisiasa ndani ya CCM. Mfumo wa chama walichokikimbia ni uleule lakini baadhi yao walikuwa daima wamejipachika juu ya mbawa zitazoweza wakati wowote ule kuwarusha na kuwarudisha walikopata malezi yao ya kisiasa.

Ncha ya pili ya mkuki wa CCM katika jaribio la kuumaliza upinzani inawalenga wapinzani wa Zanzibar na hususan viongozi wa CUF. Hadi sasa viongozi wa CUF walio Zanzibar wanaonesha kusimama imara, wakiuunga mkono msimamo wa katibu mkuu wao, Maalim Seif Hamad. Wanasema kwamba wataendelea kupigania demokrasia halisi.

Jambo moja lisilo shaka ni kwamba demokrasia halisi haiwezi kuja hivihivi bila ya mapambano. Panaweza pakafanywa jitihada za kuiengaenga kwa uangalifu mkubwa demokrasia ya aina hiyo lakini patahitajika kazi ngumu mpaka ipatikane.

Samir Amin, mzalia wa Misri, aliyefariki Jumapili iliyopita akiwa na miaka 86, alikuwa mwananadharia wa Kimarx na mchumi. Amezitalii jamii mbali mbali za Kiafrika na ameandika mengi kuhusu nchi za Kiafrika.

Amin amewahi kuhoji katika insha moja kwamba mapambano ya kuleta demokrasia katika nchi za Kiafrika yanahitaji mengi. Miongoni mwayo ni kuwahamasisha wananchi, kuwakusanya (katika chama), kuwa na mkakati wa kupiga mbali na uwezo wa kuchagua ni hatua gani ichukuliwe na wakati gani.

Katika nchi zenye demokrasia iliyopevuka, wenye nguvu huenda wakakiachia chama cha upinzani kishinde uchaguzi ili kuuzima uwezekano wa kuzuka machafuko. Wanachokuwa wanakifanya ni kuubadilisha utawala ili pasibadilike kitu. Mambo yaendelee kuwa yayo kwa yayo, japokuwa sura za viongozi wa serikali zimebadilika.

Samir Amin aliwahi kuuliza iwapo kuna haja ya kuwa na chaguzi ikiwa chaguzi zenyewe ndio kama tunavyoziona za ulaghai na mizengwe. Au ikiwa hazisababishi pakapatikana mageuzi ya maana. Ni swali linalokwenda sambamba na lile la yule swahibu yangu aliyeshauri kuwa bora Tanzania iurejelee mfumo wake wa zamani wa kuwa na chama kimoja halali cha siasa.

CCM ilipokubali, kichwa upande, mfumo wa vyama vingi vya siasa urejelewe, mfumo huo uliwekewa vizuizi ili usiweze kuuvunja mgongo wa CCM. Miongoni mwa vizuizi hivyo ni pamoja na katazo kwamba mfumo huo usiyafanye mamlaka ya CCM yamomonyoke. Hayo yalipokubaliwa, pakawekwa kizuizi kingine kuzuia pasifanywe duru ya pili katika uchaguzi wa rais, ili kuepusha uwezekano wa kuundwa serikali ya ubia.

Hata Bunge la Katiba lilipoundwa tayari palikuwa na mkakati wa kulifanya lisifanikiwe. La kusikitisha zaidi ni kwamba bunge lenyewe halikuwa na ubavu; liliwapotezea watu wakati wao, nguvu zao na fedha chungu nzima za umma zilitumiwa kwa zoezi ambalo wakubwa wa siku hizo walikwishaamua lisende popote.

Mbinu hizi za sasa zinatumiwa baada ya kuonekana katika uchaguzi mkuu uliopita

kwamba vyama vya upinzani vinaweza vikavivuka vizingiti mbalimbali vilivyowekwa na vikashinda.

Ni dhahiri kwamba msimu huu wa wapinzani kuhamia CCM umeviumiza vyama vya upinzani. Sidhani kama upinzani unaweza kufa kwa wepesi, lakini ni wazi kwamba kuta za ngome yake zimekwishaanza kuwa na nyufa.

Mkakati wa kubomoa ngome zote za upinzani ni moja ya njama za kuudhoufisha upinzani. Njama nyingine ni kuwaingilia wapinzani na kuwashambulia bila ya huruma katika maeneo ya kupiga kura. Mashambulizi hayo yana lengo la kuwavunja moyo wapinzani na kuwakatisha tamaa.

Waliovihama vyama vyao na kujiingiza CCM, wamezishusha hadhi zao na wamejivunjia heshima zao. Mfano mzuri ni wa Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye pamoja na kujivunjia heshima yake, alionesha udhaifu mkubwa alipokiacha mkono chama chake cha CUF katika wakati uliokuwa nyeti, akajivuta na kujitenga na halafu akajaribu kujirejesha kwa nguvu.

Angalau Mchungaji Christopher Mtikila, aliyekuwa kiongozi wa chama cha Democratic na aliyefariki 2015, alikuwa mtu mwenye msimamo.

Mtindo wa kujaribu kuvibomoa vyama vya upinzani ni mtindo wenye hatari hata kwa CCM yenyewe. Ni hatari kwa sababu ndani ya CCM kuna wanaokirihishwa kuwaona mahasimu wao wa jana leo wakikumbatiwa na kupewa vyeo. Lazima nao watakuwa wanapanga mkakati wa kujikinga ndani ya chama. Kuna uwezekano pakazuka mpasuko katika siku zijazo.



Baruapepe: hamidurubawa@gmail.com
 
Mkuu usijari kuhusu hii ama ama usajiri unafungwa mwezi wa November .
 
Back
Top Bottom