Mimi nilitegemea Zitto kwa nafasi yake na kwa umaarufu ataanza kuangalia mbali zaidi, je yeye kama kijana anaanzisha ama anahamasishaje vuguvugu la vijana kujikomboa na kusimama kutetea maslahi ya taifa hili changa. Nilitegemea angekuwa mtu wa makongamano, semina na mikutano ya kuhimizana na vijana walio vyuoni na wengine walio katika ajira. Hii ni kwa sababu ya umakini aliouonyesha na mara nyingi amekuwa ana vyanzo vya kuaminika vya taarifa mbalimbali.
Kwa namna hii ndipo atakuwa anatoa mchango wa kudumu na wakuaminika kwa jamii ya nchi hii. Ila akijisahau na kuanza kuwaza masuala ya majimbo na wapi pa kugombea kwa vile anakubalika anakuwa na yeye ameanza kuwaza kama walivyo wanasiasa uchwara tuliowazoea.
Ajiulize, kugombea kwake jimbo tofauti na Kigoma kaskazini, kutainufaisha nini jamii ama kuna faida gani kwa harakati za kusafisha uchafu katika taifa hili? Labda kama anajua akiachia jimbo hilo litachukuliwa na mwanaharakati mwingine wa kuaminiwa na yeye kwa umaarufu na kukubalika kwake akachukue na kupokonya jingine toka kwa mbunge uchwara anayedhani ubunge ni kwa ajili ya tumbo lake, familia yake na walevi wenzake, haya yote yakiwa na manufaa ya kupanua wigo wa mapambano na harakati.
Zitto akifa leo hatutaki tubakiwe na historia tu ya alichowahi kukisema tunatakiwa tubakiwe na ushahidi wa alichowahi kukifanya, na mfano mzuri ni vuguvugu la wanaharakati ambalo, kwa mtazamo wangu, anatakiwa atumie uamaarufu wake katika kulikuza na kulistawisha.