This is the Msekwas Grass roots
Diwani wa CCM anaswa akidaiwa kununua shahada
Na Frederick Katulanda,Busanda
WAKATI kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Busanda zikiendelea kushika kasi, hali imekuwa mbaya kwa CCM, baada ya diwani na mabalozi wake wawili kunaswa wakidaiwa kuorodhesha majina ya watu wenye shahada kwa lengo la kuzinunua.
Tukio hilo limetokea siku chache baada ya naibu katibu mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe na msimamizi wa uchaguzi wa CUF, Maole Kuchilongulo kuituhumu CCM kuwa ilikuwa ikijiandaa kuendesha hujuma ya kununua shahada za wapiga kura kwa lengo la kupunguza kura za upinzani.
Tukio hilo lilitokea juzi katika kijiji cha Shilungule, kata ya Busanda kati ya saa 2:30 na saa 3:00 usiku baada ya mwenyekiti wa Chadema wa kata hiyo kubaini kikao cha siri cha wajumbe wa nyumba kumi kilichokuwa kikiongozwa na diwani wa kata hiyo, Alphonce Matonange (CCM).
Inadaiwa kikao hicho kilikuwa na ajenda ya kuorodhesha shahada za wapiga kura.
Kamanda wa polisi wilayani Geita (OCD), Shabani Kimei alithibitisha kukamatwa kwa watu hao na kusema jeshi lake limewakamata kutokana na malalamiko ya Chadema na kwamba wanalifanyia uchunguzi wa kina tukio hilo.
"Sisi kazi yetu ni kupokea malalamiko kama hivyo tumepokea na sasa tunafanya uchunguzi. Tumewaita watu wa Chadema wametoa maelezo na tunaendelea na uchunguzi ukikamilika tutawasiliana na msimamizi wa uchaguzi kwa ajili ya hatua zaidi ikiwa ni pamoja na kuangalia sheria za uchaguzi zinasemaje juu ya hatua hiyo," alieleza.
Akizungumzia tukio hilo, mkurugenzi wa oganaizesheni ya mafunzo wa Chadema ambaye pia ni kamanda wa kampeni za uchaguzi wa Busanda, Singo Benson Kigaila alisema mara baada ya kupata taarifa hiyo, walituma gari na kuwasiliana na polisi ambao walifika na kumtia mbaroni diwani huyo na balozi mmoja huku wengine wakikimbia.
Sambamba na mjumbe huyo kukamatwa na diwani, mjumbe mwingine wa nyumba kumi amekamatwa jana asubuhi katika Kijiji cha Musasa kilicho kata hiyo ya Busanda akidaiwa kuendesha zoezi hilo la kuorodhesha majina ya wananchi wenye shahada pamoja na namba zake.
"Baada ya kupata taarifa hiyo tulipeleka timu yetu, wakati inafika tu diwani na wajumbe wengine ambao walikuwa katika zoezi hilo walikimbia baada ya kuona mwanga wa taa za gari, mjumbe mmoja ambaye alikuwa na shahada alinaswa na baada ya kuhojiwa alikiri kuendesha zoezi hilo," alieleza.
Alisema akihojiwa na maofisa wa polisi mbele ya viongozi wa Chadema, mjumbe huyo wa nyumba kumi alisema walikuwa wakiorodhesha shahada hizo kutokana na maelekezo ya wakubwa wake ndani ya CCM ambao waliyatoa kupitia msimamizi wa chama chao ambaye alimweleza kuwa ni mwanamke kutoka wilayani Magu mkoani Mwanza.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Diwani Alphonce Matonange wa kata ya Busanda ambaye inadaiwa baada ya kukimbia usiku huo aliwahi kupiga simu polisi akidai kulikuwa na gari la Chadema ambalo lilikuwa limeenda kijijini hapo kwa nia mbaya na kwamba lilitaka kumgonga.
Mwingine ni mjumbe wa nyumba kumi aliyefahamika kwa jina la Abdalah Ibrahimu ambaye inadaiwa alikutwa akiwa na karatasi iliyokuwa imeshaorodheshwa watu 20, ikionyesha majina na namba zao za shahada za kupigia kura.
Kigaila alisema kuwa hatua hiyo ni kosa la jinai kwa vile sheria inaeleza wazi kuwa ni kosa la jinai kuorodhesha namba ya shahada ya kupigia kura ya mtu mwingine awe mwanachama wako ama wa chama kingine na kusema hatua yao ya kwanza imekuwa ni kuwakamata na kuwakabidhi mikononi mwa polisi kuthibitisha walichokuwa wakieleza katika mikutano yao.
Alisema sasa wanasubiri kuona polisi itawafanya nini ikiwa ni pamoja na viongozi wao waliowatuma kuendesha zoezi hilo.
Wakati huo huo, wanafunzi wa shule ya sekondari ya Butundwe iliyopo katika kata ya Nyakagomba wameadhibiwa kwa viboko sita kila mmoja baada ya kuzomea msafara wa mgombea ubunge wa CCM, Lolencia Bukwimba wakati ulipokuwa ukipita eneo la shule yao kutoka kwenye kampeni.
Tukio hilo hilo limetokea Ijumaa majira ya saa 10:00 jioni wakati wanafunzi hao walipoona msafara wa mgombea huyo ukipita eneo la shule na kuzomea, kitendo ambacho kiliwaudhi baadhi ya viongozi wa CCM na kuwaagiza viongozi wa kata kufuatilia shule hiyo.
Habari toka Nyakagomba zinaeleza kuwa katika maagizo hayo katibu mwenezi wa kata hiyo, Oscar Magori, ambaye pia ni mwalimu wa Shule ya Msingi Nyakagomba, ndiye aliyekwenda kulalamika kwa mwalimu mmoja wa zamu ambaye aliamua kuwaadhibu wanafunzi wote wa kidato cha kwanza lakini baadhi ya wanafunzi waligoma na hivyo kuwaadhibu sita tu.
Mkuu wa shule hiyo Monika Mzungu alisema wanafunzi hao wameadhibiwa na mwalimu huyo kwa sababu binafsi na kwamba yeye kama mkuu wa shule hiyo hakutoa amri hiyo ya kuwachapa viboko wanafunzi.
"Mimi sikuagiza watoto hao waadhibiwe. Nilishauri wasijiingize katika siasa na waepuke kushabikia vyama bali wajitahidi katika masomo. Kama kuna mwalimu amewaadhibu amewaadhibu yeye kama yeye na sina habari na hilo," alieleza mkuu huyo.