kbm
JF-Expert Member
- Oct 5, 2012
- 5,224
- 1,676
- " *Balozi Mahiga asema anataraji kwenda ughaibuni hivi karibuni".
Rais alikwenda Rwanda kwa ajili ya kufungua daraja la kimataifa la Rusumo na kituo cha biashara chenye huduma za pamoja, ambacho ni kiunganishi muhimu kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.Katika safari hiyo, katika kile kinachoonekana kuwa ni muendelezo wa hatua yake ya kubana matumizi ya serikali kadri iwezekanavyo, Rais Magufuli alikuwa na msafara usiozidi watu 10.
Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustino Mahiga, aliiambia Nipashe jana kuwa Rais Magufuli anatarajia kusaifiri tena kwenda nje ya nchi hivi karibuni.Balozi Mahiga alisema katika safari hiyo, msafara wake utaendelea kuhusisha watu wachache wenye umuhimu katika safari husika ili kuepukana na gharama zisizokuwa za lazima.
Hata hivyo, Balozi hakutaja nchi hiyo itakayofuatia baada ya ziara ya Rwanda wala siku ya kusafiri.“Rais atasafiri tena hivi karibuni… na utaratibu huu wa kuwa na msafara wa watu wachache hautabadilika,” alisema Balozi Maiga.
Taarifa ambazo Nipashe ilizipata na kuthibitishwa jana zilidai kuwa Rais Magufuli alikuwa nchini Rwanda na ujumbe wa watu wasiofikia 10, akiwamo Balozi Mahiga.
Akiwa Rwanda, Rais Magufuli pia alihudhuria kumbukumbu ya miaka 22 ya mauaji ya halaiki nchini humo, ya mwaka 1994.
Chanzo kiliiambia Nipashe kuwa katika msafara huo wa kwanza kwa Rais Magufuli nje ya mipaka tangu aingie Ikulu Novemba 5 mwaka jana, aliambatana na maafisa wanne kutoka Wizara ya Mambo ya Nje akiwemo Mahiga, na maafisa wasaidizi wengine wa Rais.
“Ni kweli msafara wa Rais ulihusisha watu wachache sana. Ni mimi, maafisa wengine kama wanne hivi kutoka wizarani kwangu (Mambo ya Nje) na wasaidizi wa Rais," alisema Balozi Mahiga wakati akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana.
"Sidhani kama jumla yetu ilifikia watu kumi.” Alipoulizwa uzoefu wake kuhusiana na idadi ya maafisa ambao huambatana na Rais katika ziara kama iliyofanywa na Rais Magufuli nchini Rwanda, Balozi Mahiga alisema hafahamu kwa sababu hakumbuki kama kuna Rais aliwahi kwenda nchi jirani akitumia usafiri wa gari kama alivyofanya Magufuli.
“Sifahamu kwakweli. Kumbuka kuwa katika ziara hii Rais alitumia usafiri wa gari,” alisema Balozi Mahiga.
Balozi Mahiga alisema utaratibu huo wa kuhusisha watu wachache katika safari za Rais Magufuli nje ya nchi utakuwa ni wa kudumu kwa sababu lengo kubwa ni kubana matumizi yanayoweza kuepukika ili hatimaye kuipa serikali uwezo wa kutimiza malengo yake ya kuhakikisha kuwa inaboresha huduma za jamii zikiwamo za afya, maji, miundombinu na pia utoaji wa elimu bure.
Akiwa Rwanda, Rais Magufuli alisema hapendi kusafiri kwenda ughaibuni kwa sababu anapenda kubana matumizi kwa vitendo.
Akizungumzia kauli hiyo, Mahiga alisema ni kweli, mara zote Rais Magufuli amekuwa akisisitiza juu ya umuhimu wa kila mmoja ndani ya serikali yake kubana matumizi yasiyokuwa ya lazima na ndiyo maana amekuwa akilidhihirisha hilo kwa vitendo.
“Rais anachosema kuhusu kubana matumizi ni kweli kabisa… ndiyo maana msafara wake katika ziara hiyo (ya Rwanda) hatukuzidi watu kumi. "Hii inamaanisha hataki kuwapo kwa matumizi makubwa katika safari za nje.”
Aidha, Balozi Mahiga alifafanua kuwa baadhi ya mawaziri na maafisa wengine kadhaa walioshiriki shughuli ya uzinduzi wa daraja la Rusumo waliishia hapo na kurudi wakati yeye na maafisa wachache wa serikali wakiongozana na Rais katika ziara ya Rwanda.
“Nafikiri mliwaona baadhi ya mawaziri pale Rusumo… wale walitokea huku Tanzania na kurudi. Hawakuwamo katika msafara uliokuwa Rwanda,” alisema Balozi Mahiga.
MZIGO WA SAFARI ZA NJE
Wakati akilihutubia Bunge la 11 kwa mara ya kwanza katika uzinduzi wa chombo hicho Novemba 20, Rais Magufuli alisema serikali yake itadhibiti safari holela za nje kwa sababu hutumia fedha nyingi ambazo zinaweza kuelekezwa katika matumizi mengine yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Akitaja mfano wa gharama ambazo taifa lilikuwa likibebeshwa kila uchao kutokana na safari holela za nje ya nchi, Rais Magufuli alisema katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 na 2014/2015 peke yake, zilitumika zaidi ya Sh. bilioni 357.6 kugharimia safari za nje, ikiwamo kulipia tiketi za ndege na posho; fedha ambazo zingewezesha kujengwa kwa barabara za lami za urefu wa kilomita 400.
Chanzo: NIPASHE