IWAPO uongozi wa Yanga ungetoa ruhusa kwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mrisho Ngassa angefanikiwa kujipatia kitita cha zaidi ya Sh milioni 432 katika kipindi cha miaka mitatu.
Klabu ya Ligi Daraja la Pili ya Lov-Ham ya Norway iko tayari kumlipa mshahara wa dola 10,000 (shilingi milioni 12) kwa mwezi kwa kipindi cha miaka mitatu na huenda ingeongeza kiwango kama angepata mafanikio.
Iwapo Ngassa angepata ruhusa kujiunga na timu hiyo, bila ya marupurupu angekuwa anapata kitita cha shilingi milioni 144 kwa mwaka hiyo inamaanisha kwamba kwa miaka mitatu alikuwa na uhakika wa kitita cha shilingi milioni 432 au zaidi.
Ilielezwa kwamba baada ya wakala huyo kuwasiliana na uongozi kulieleza suala hilo mwamuzi wa mwisho ni mfadhili wao mkuu, Yusuf Manji kwa kuwa ndiye anayesajili wachezaji.
Mwanaspoti ilifanya juhudi za kumpata Manji aliyerejea nchini hivi karibuni kutoka Marekani lakini simu yake ilikuwa imezimwa.
Hadi jana mchana tiketi ya Ngassa ya kuondoka kwenda Norway ilikuwa katika ubalozi wa nchi hiyo jijini Dar es Salaam lakini imeelezwa hakukuwa na maelewano mazuri kati ya uongozi wa Yanga na wakala wake, Yusuf Bakhresa.
Habari za uhakika zimeeleza kwamba, klabu ya Lov-Ham ilikuwa tayari kutoa kitita cha dola 50,000 (zaidi ya sh milioni 60) kwa Yanga ili imuachie mchezaji huyo kwenda Norway.
Mchana kutwa Mwanaspoti ilimsaka Ngassa bila ya mafanikio kutokana na simu yake kuwa imezimwa, ila ilifanikiwa kumpata Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega aliyekiri kupokea taarifa za mshambuliaji huyo chipukizi kutakiwa na klabu ya Norway lakini akasisitiza suala la kufuatwa kwa utaratibu.
"Kweli niliwasiliana na wakala na akaniambia kwamba Ngassa anatakiwa Norway na tayari tiketi iko ubalozini. Lakini hivi tunaweza kufanya biashara ya mchezaji haraka bila ya kufuata taratibu namna hiyo?," alihoji Madega jana kutoka Nairobi, Kenya.
"Nimemwambia tunataka tukutane na klabu hiyo, tufanye amzungumzo kuhusu suala la Ngassa na baada ya hapo tutamuachia, sisi hatuna tatizo, mbona Ivo Mapunda na Said Maulid wameuzwa kwa kufuata utaratibu. Sidhani kama njia ya kumuuza mchezaji kupitia wakala bila ya viongozi wa klabu kuwa ni sahihi.
"Hapo hatujajua iwapo Ngassa atakuwa anauzwa klabu nyingine, Yanga itafaidika vipi. Hilo ni suala la kufuata utaratibu na kuwa na mikataba ya uhakika badala ya kufanya mambo kwa haraka tu," alisema Madega.
"Hatuna kinyongo, wala msituhukumu, tuko tayari kumuuza mchezaji yeyote lakini utaratibu ufuatwe na wanaotaka mchezaji wa Yanga basi wawasiliane na kukutana na viongozi wa Yanga ili tumalizane kiutaratibu jamani," alisisitiza Madega.
Habari zimeeleza kwamba, Lov-Ham ilikuwa tayari kutoa kitita hicho cha dola 50,000 kwa kuwa wachezaji wengi wa Afrika iliowachukua hawana mafanikio.
Lakini uongozi wa klabu hiyo ukasisitiza kwamba uko tayari kuweka kipengele ambacho kitatoa nafasi ya kuongeza kiwango cha malipo ya mchezaji huyo.
Wiki iliyopita, Mwanaspoti ilifanya mawasiliano na Kharthoum, Sudan na kupata taarifa namna ambavyo Ngassa ni lulu nchini humo huku klabu kubwa za Al Hilal na El Merreikh zikionyesha nia ya kutaka kumnasa katika dirisha la usajili la mwezi Juni.
Klabu hizo zimeonyesha nia ya kumchukua kwa dau kubwa zaidi kuanzia dola 160,000 kutoka kwa Al Hilal huku El Merreikh wakiwa tayari kutoa kitita cha kuanzia dola 400,000 (zaidi ya Sh milioni 450).
Mshambuliajia huyo, ambaye ni mtoto wa zamani wa mchezaji wa Simba, Khalfan Ngassa na Pamba ya Mwanza �TP Lindanda� ameonyesha kuwa lulu kubwa kutokana na uwezo wake uwanjani anapokuwa na Yanga pia timu ya taifa, Taifa Stars.
Ngassa ni tegemeo kubwa la Taifa Stars katika michuano ya Kombe la CHAN itakayoanza mwezi Februali nchini Ivory Coast.