CHADEMA yajipanga kuchukua jimbo la Mramba
na Dixon Busagaga, Moshi
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeanza kupanga mikakati ya ya kuhakikisha kinanyakua Jimbo la Rombo, ambalo kwa sasa linaongozwa na Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Basil Mramba, anayekabiliwa na kesi ya kutumia vibaya madaraka yake.
Mramba na mwenzake, Daniel Yona, wanashtakiwa katika kesi ya jinai namba 1,200 ya mwaka huu ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7.
Akizungumza katika moja ya mikutano ya hadhara inayofanywa na mbunge wa Moshi Mjini, Philemoni Ndesamburo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Manispaa ya Moshi, Japhary Michael, alisema inajipanga kuhakikisha wananchi wa jimbo hilo, wanapata mwakilishi atakayewaletea maendeleo.
Michael alisema, CHADEMA hivi sasa kinafanya mikutano ya hadhara ili kutoa mwongozo kwa wananchi wapi chama kilipo na wapi kinaelekea na hivi karibuni kampeni viongozi wa kitaifa wanaoendesha Operesheni Sangara, watatua katika jimbo hilo kuwafahamisha wananchi mustakabali wa cha taifa.
Alisema kampeni hizo zitafanyika ili kukiiimarisha chama kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwaka 2010.
Kama chama tunajiandaa kuelekeza nguvu jimbo la Rombo
ni wazi ni miongoni mwa majimbo tutakayoyatwaa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, alisema Michael.
Wapinzani ambao tuliambiwa wendawazimu
ambao tumefichua ubadhirifu wa fedha za umma kwa baadhi ya viongozi wa serikali, matunda yake ndio hayo ya kufikishwa mahakamani kwa vigogo hao, aliongeza Michael. Akizungumza kuhusu kuhamishwa kwa soko la Kiborloni, Michael alisema anasikitishwa na kitendo cha manispaa ya Moshi kubadili uwanja wa mpira wa jamhuri kuwa soko.
Wamehamisha soko la kiborloni kwa sababu za kisiasa., wasijali wananchi wa manispaa watateseka kwa kiasi ganialisema. CHADEMA mkoani Kilimanjaro, kinaendelea na mikutano ya hadhara ambapo hadi sasa wanachama kutoka CCM zaidi ya 800 katika kata za Majengo, Mji Mpya, Kiborloni na Rau, wamejiunga na CHADEMA.