Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
Mradi mkubwa wa usafirishaji umeme kutoka Iringa hadi Shinyanga katika msongo wa kilovolti 400 unaofadhiliwa na washirika mbalimbali wa maendeleo tayari umekamilika kwa 89% na unategemewa kukabidhiwa kwa Serikali ifikapo Septemba mwaka huu.
Hayo yalielezwa na Meneja Mradi anayesimamia ujenzi wa vituo vya kupoza umeme wa mradi huo, Mhandisi James Mtei alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma.
Mhandisi Mtei alisema kuwa mradi huo uliogharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 224 sawa na Shilingi bilioni 450 umejumuisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme umbali wa kilomita 670 na vituo vya kupoza umeme katika mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga.
Alisema kwa upande wa sehemu ya kutoka Iringa hadi Dodoma kilomita 225 imeshakamilika kwa asilimia 99 na kinachosubiriwa kwa sasa ni mkandarasi kulifahamisha rasmi Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwa kazi imemalizika ili kituo kianze kufanyiwa majaribio na kukabidhiwa kwa serikali mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Alifafanua kuwa sehemu nyingine za kutoka Dodoma hadi Singida na Singida hadi Shinyanga utekelezaji wake umefikia asilimia 89 ambapo mradi wote kwa ujumla unatarajiwa kukabidhiwa kwa serikali mapema Septemba mwaka huu.
Alisisitiza kuwa mara baada ya mradi wote kukamilika kama ilivyopangwa hali ya umeme katika mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida, Shinyanga na Kanda ya Ziwa kwa ujumla itaimarika sana.
Wakati huo huo Mhandisi Nishati Mkuu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Salum Inegeja aliongeza kuwa mradi huu ni sehemu ya mradi mkubwa wa kuunganisha gridi za Zambia, Tanzania na Kenya (ZTK).
Alisema kuwa katika mradi huo wa kikanda, Tanzania imeshatekeleza sehemu kubwa ya mradi huo kutoka Iringa hadi Singida na sehemu iliyobaki ya kutoka Singida hadi Namanga kupitia Arusha fedha zake kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) zilishapatikana ambapo kwa sasa taratibu za tathmini ya fidia kwa watu watakaopisha mradi huo zinaendelea.
Aliendelea kusema katika sehemu ya kutoka Mbeya hadi Tunduma upembuzi yakinifu unaendelea ambapo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Mhandisi Inegeja alisema kukamilika kwa mradi mbali na kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini, kutaiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu katika biashara ya umeme kupitia mifumo ya gridi za nchi jirani katika ukanda wa mashariki (Eastern African Power Pool -EAPP) na zilizopo katika ukanda wa kusini (Southern African Power Pool -SAPP).
Chanzo: Michuzi