Jaws
JF-Expert Member
- Jun 13, 2023
- 622
- 2,225
MPOPOMA - Mti usio na kazi
Wazaramo walipoona haufai kwa mbao, mkaa wala kwa kuni, wakaususa na kuuita mti usio na maana.
Popote ulipomea, haukuguswa wala kushambuliwa na wavunaji wa miti, kwa sababu hauna kazi. Na matokeo yake, umekuwa miongoni mwa miti mirefu hifadhini Pugu Kazimzumbwi..
Wataalamu baada ya tafiti, walibaini ni mti unaozalisha kiwango cha juu sana cha oxygen. Lakini wala haukubadilishwa jina. Bado huitwa kubwa jinga. Yaani jiti refu, zuri lililonyooka lakini kazi halina. Halifai kwa mbao wala kwa sanaa ya vinyago.
Baadhi ya watu hupenda kuwatania wenzao wanaohisi hawana athari chanya kwa jamii na kuwaita 'Mpopoma' au Popoma. Limekuwa jina lisilopendwa kwa wanaolijua na kutumiwa na wasiolijua, kunogesha masihara.
Nimeuwaza kwa kina 'Mpopoma' nimewawaza watu wanaokataa kwa nguvu na jitihada nyingi kuwa Mpopoma. Nakwenda mbali na kuona namna inafanya wengine kuigiza maisha ili wasiitwe Mpopoma..
Wapo ambao huishia kujiingiza katika biashara haramu ili kuiaminisha jamii yao kuwa wao sio, Mpopoma. Wapo ambao huuza nafsi zao na kujipoteza kabisa ili kujiaminisha wao na wapendwa wao kuwa wao ni watu wenye maana.
Je, Mpopoma ungefanya hayo ungekuwa na maisha marefu? Thamani yake kama chanzo cha hewa safi na muhimu kwa viumbe hai ingetambuliwa? Kwa kufanya kinyume na utu wako ni uthibitisho halisi kuwa wewe ni wa maana? Kwa kukiuka taratibu za ubinadamu ili kujipatia fedha, huko ndiko kuwa na maana?
Wacha nikutafakarishe sambamba na ufinyu wa uelewa wangu. Mungu aliumba kila kitu kwa makusudi kabisa. Mungu alimuweka kila mja mahali alipoona yeye kuwa yafaa. Dhima kuu ni kumtumikia na kùtumikiana. Katika dhima hiyo, hata kutokuwa na maana kwa majira fulani kuna maana yake.
Namaanisha, kutokuwa na uwezo wa kufanya mambo chanya ya kuonekana na kusaidia jamii yako kuna maana wakati mwingine. Utajifunza vipi ustahimilivu bila kubezwa? Utajifunza vipi uvumilivu bila kutindikiwa? Kuna wakati inabidi ubaki kuwa Mpopoma ili ujifunze kuwa na maana halisi na uwe darasa kwa wengine.
Kuna wakati inabidi ukae katika nafasi ya Mpopoma ili ung'amue kuwa, wanaokupenda watakuchagua, hata kama huna faida yoyote kwao. Watasimama na wewe hata kama hawajui kuwa unazalisha Oxygen.
Na wakati ukiwa Mpopoma, jitahidi angalau hali ya hewa unayozalisha iwe nzuri. Ni kweli, huna chochote cha kuongeza thamani ya kushikika mahali ulipo, usiwe chanzo cha makwazo, hasara na maumivu kwa wengine.
Huna kazi wala biashara, wewe ni kijana unaishi kwa ndugu au kwa wazazi; kuwa mtu wa faida. Fanya japo kazi za nyumbani. Jifunze ujuzi unaoweza kuufanya na ukawa na manufaa hapo nyumbani, epuka kuwa mzigo mzito. Epuka kuwa hasara moja kwa moja.
Hata kama ndo Mpopoma, zalisha japo hewa safi rafiki. Wengi wetu hupitia majira ya kutokuwa na faida ya wazi kwa wengine. Lakini angalau kuwa na faida kwako na katika mazingira binafsi.
Nakutakia wakati mwema.
✍ Eva Mrema
0742 6301 41