SERIKALI imemuongezea muda wa mkataba wa miaka miwili Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Clement Mshana, aliyetimiza miaka 60 ya kustaafu kwa mujibu wa sheria, Machi mwaka huu.
Habari zilizotufikia Tanzania Daima hivi karibuni, zimepasha kuwa uamuzi huo umefikiwa rasmi, ingawa awali kulikuwepo na hali ya utatanishi kuhusu mkataba huo kutokana na kuwepo kwa lawama nyingi dhidi ya udhaifu wa uongozi wa TBC.
Mmoja wa wafanyakazi wa TBC ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu si msemaji wa shirika hilo, alisema kwa kipindi cha miezi kadhaa ya huko nyuma, Mshana alikuwa akionyesha wasiwasi mwingi kuhusu kuondoka kwake hadi pale ilipothibitika kwamba ataongezewa muda.
Hatua hiyo ya serikali kumuongezea muda Mshana, imechangiwa na hali ya joto la kisiasa lililoanza hivi sasa nchini na ambayo inatarajiwa kuendelea kupanda zaidi hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwakani.
Ofisa mmoja wa juu katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, ambaye naye hakutaka jina lake litajwe, alisema kuwa Mshana amepata bahati hiyo kutokana na watu waliokuwa wakimchagua asilimia kubwa wanafahamiana naye.
Ili kuonyesha kwamba Mshana alikuwa ametimiza miaka ya kustaafu, alifanya sherehe ya kumbukumbu ya kutimiza miaka 60 katika Makao Makuu ya TBC, Nyerere Road na kuhudhuriwa na kikundi kidogo cha wafanyakazi wa karibu na mkurugenzi huyo aliyekata keki maalumu ya kutimiza miaka hiyo.
Chanzo kingine kilisema kuwa kwa kutambua ukomo wake, siku chache alifanya sherehe ya kuwaaga wajumbe wa bodi kwa kumaliza kipindi chake cha mwaka mmoja na nusu.
Wafanyakazi kadhaa wa TBC walioulizwa kuhusiana na hatua hii ya kumuongezea Mshana muda, wameelezea kushitushwa kwao na uamuzi huo kutokana na kwamba tangu aingie madarakani mwaka 2011, shirika limekuwa likilegalega.
Jitihada za Tanzania Daima, kumtafuta Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara, kuelezea jambo hilo ziligonga mwamba baada ya simu yake kuita bila kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe hakujibu.