Mkasa: Majini Walivyoitesa Ndoa Yangu

Mkasa: Majini Walivyoitesa Ndoa Yangu

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Joined
Apr 29, 2016
Posts
20,746
Reaction score
25,637
SEHEMU YA KWANZA


Vincent yupo katika furaha baada ya kufunga ndoa na mpenzi wake wa siku nyingi aitwaye Vera, wapo kwenye fungate lao, ikiwa ni saa chache tu baada ya kutoka ukumbini. Wote wana furaha sana na Vice ana hamu sana ya kukutana na mkewe kimwili baada ya kuwa waaminifu kwa kipindi chote cha uchumba wao.

Ajabu ni kwamba, Vera hataki kumpa mumewe haki yake ya tendo la ndoa, jambo linalompa hasira Vincent na kutaka kumpiga. Katika hali ya kushangaza, mkono wake ukawa mzito na kurudi wenyewe. Ghafla Vera anapiga magoti chini na kuaomba msamaha.
Macho yake yanatoa machozi, lakini cha kushangaza zaidi, machozi yale siyo ya kawaida. Yalikuwa machozi ya damu, tena damu mbichi! Je, nini kitatokea? Fuatilia...

MACHO yalimtoka Vincent akiwa haamini kilichokuwa mbele yake. Mkewe wa ndoa kulia halikuwa tatizo, labda ilikuwa ni maumivu ya makosa ambayo alifanya kwa mumewe, lakini tatizo ni kule kulia machozi ya damu. Vincent akasimama kwa woga akizidi kutetemeka.
“Nisamehe mume wangu Vincent, nisamehe please, sitarudia tena, nakubali nimefanya makosa mume wangu,” Vera akasema huku akizidi kulia.
Katika hali ya maajabu, damu ikaanza kuchuruzika mashavuni mwake na baadaye kushuka hadi kwenye matiti. Anazidi kulia akisisitiza anaomba kusamehewa kwa kosa alilofanya.

“Vera, una nini?”
“Nisaheme Vice.”
“Ok, lakini mbona unatoa damu?”
“Damu?”
“Ndiyo damu.”
“Wapi?”
“Machoni.”

Vera akashtuka sana, papo hapo akayatupa macho kwenye matiti yake na kuona damu ikichuruzika kutoka machoni mwake. Punde damu ikatoweka, machozi ya kawaida yakaonekana!
“Mbona sikuelewi, iko wapi basi hiyo damu uliyokuwa unasema?” Vera akasema akionekana kushtushwa na kauli ya Vice.
“Ilikuwa hapo muda huu huu, lakini nashangaa imetoweka.”
“Imetoweka kivipi?”
“Sijui.”

“Unataka kusema kwamba nilikuwa nalia machozi ya damu? Na kama ndiyo inawezekana vipi sasa jamani Vice? Mbona unanishtua sana?”
“Sikushtui Vera, ni kweli!”
“Lakini yako wapi sasa?”
“Haya tuachane na hayo, labda ni macho yangu tu, lakini kwanini unanifanyia hivyo mpenzi wangu?”
“Vipi?”
“Unaninyima penzi?”
“Nina maana yangu, tena sababu za msingi sana, na unatakiwa kuelewa kila ninachokuambia, kwa leo haitawezekana, lakini kesho saa nne, nitakufurahisha.”

“Saa nne?”
“Ndiyo!”
“Asubuhi au usiku?”
“Asubuhi darling!”
“Poa, twende basi bafuni.”
“Sawa.”
Wakaongozana hadi bafuni kuoga, huko walifanya kila aina ya michezo ya kimahaba, lakini si tendo la ndoa. Baadaye wakarudi zao chumbani. Wakalala kwa mtindo wa kupendeza sana. Vincent alikuwa amelala kwa mgongo, Vera akiwa amelala kwa ubavu pembeni yake, kichwa chake akiwa amekilaza kifuani mwa Vincent.
Usingizi mnono!

***
Vicheko vile havikuwa vya kawaida kabisa, kwa dakika ishirini nzima, bado alikuwa amesimama akiwa na wasiwasi na mawazo mengi mbele ya umati ule mkubwa wa watu ambao hakuwafahamu! Hakujua kama ilikuwa mchana au usiku, maana ukumbi mzima ulikuwa unang’ara kwa taa kubwa za kupendeza.
Manukato ya kuvutia na harufu nzuri ya vyakula. Vicheko vinaendelea. Akiwa katika hali ile ya kuduwaa, kijana mmoja mnene, mrefu, anamfuata na kumpiga begani. Vincent akageuka katika hali ya kugutuka kidogo!

“Karibu sana kaka, katika ufalme wetu,” kijana yule akasema kwa sauti ya kitetemeshi kidogo, akimuonesha ishara kwamba amfuate.
Katika hali ambayo Vincent hakuitarajia, alijikuta akimfuata. Bila hiyari yake. Safari yao ikaishia chini kidogo ya meza kuu. Akaambiwa aketi, Vincent akatii agizo, akionekana bado ana wasiwasi mwingi sana.
Vicheko vikaendelea.

Punde, akashangaa kumuona mwanamke akiwa analetwa eneo lake akiongozwa na mabinti warembo sana. Juu ya mwanamke huyo aliyekuwa amefungwa kitambaa usoni asionekane, kulikuwa kunawaka moto, ukimfuata kila anapokwenda!
Mara akamfikia na kupewa ishara kwamba asimame. Akasimama. Akapewa ishara kwamba amfungue kile kitambaa usoni, kwa taratibu kabisa, bila hiyari yake akajikuta anafanya hivyo! Haaaaa! Alikuwa ni Vera ambaye aliacha tabasamu mwanana na kumkumbatia.

Akawa kama amenaswa na sumaku!
Hakuwa na hiyari na kitu chochote kile, Vera akaanza kumfanyia kila aina ya michezo anayoijua yeye. Vincent akiwa kimya akishangaa kila kitu. Alipoachiwa, akashangaa kumuona Vera akiwa mtu. Hata wale wasichana waliomsindikiza, wakawa utupu ghafla!
Akiwa bado anashangazwa na hali ile, Vera na wale wapambe wake, wakaanza kubadilika taratibu, macho yao yakawa yanatazama kwa juu, huku meno yao yakianza kutoka kama ngiri. Vincet akataka kupiga kelele.
Lakini hakuweza!
Je, ni wapi hapo na nini kitatokea?
MAPIGO ya moyo wa Vincent yakabadilika kadri nukta moja ilipozidi kwenda, akiwa yupo katika mshangao wa hali ya juu. Kwanini Vera wake amebadilika, kwanini amekuwa mtupu? Kwanini ametoka meno kama ngiri?
Kwanini amebadilika?
Kuna nini?

Ulikuwa mfululizo wa maswali lakini yasiyo na majibu. Aliposhindwa kupiga kelele, akataka kuanza kulia, lakini kwa bahati mbaya sana, machozi nayo yakagoma kutoka. Hakuweza kufanya kitu chochote. Akabaki anashangazwa na jinsi Vera na wenzake walivyobadilika.

Mara ukumbi mzima ukalipuka kwa makofi na vigelegele! Vincent akazidi kushangaa. Akiwa katika mshangao ule, kijana mmoja mtanashati sana, akatokea katikati ya umati wa watu na kusogea eneo walilokuwa wamesimama wale wasichana akiwemo Vera na Vincent. Akawapiga wale wasichana mgongoni, mara wakaonekana wamevaa nguo zao!

Vincent akazidi kupigwa na butwaa kuliko awali.
“Safi sana...” yule kijana akasema kisha akawapiga tena.

Mara wakabadilika, meno na macho yao kurudi katika hali ya kawaida. Vicheko vikasikika tena. Mara akasikia mlio wa king’ora kikali. Watu wote mle ukumbini wakapiga magoti. Mara akasikia muungurumo mkali, upepo na kelele zisizoeleweka. Ghafla likatokea jitu ambalo lilitisha sana hakika.

Lile jitu likapiga kofi mara moja. Wale watu wote wakakaa. Bado Vincent anashangazwa na sehemu aliyopo, matukio yanayotokea yanayosisimua, kushtusha na kuogofya huku akiwa bado hana la kufanya. Kwa mbali zilianza kumuingia hisia kwamba alikuwa kwenye ufalme wa majini!

Wazo hilo lilimwingia, lakini akalikataa. Haikuwa rahisi sana kukubaliana na wazo hilo hasa kutokana na ukweli kwamba hakuwa na kumbukumbu yoyote kama alianza safari ya kwenda huko. Lakini mara moja, akawaza huenda alikuwa katika ndoto ya kutisha!
Ndoto?

Mara zote ndoto huwezi kujua na wala huwezi kuifananisha ndoto na ndoto, sasa iweje kwake? Alikuwa katika wakati mgumu sana wa kujiuliza maswali na kujijibu mwenyewe. Akiwa katika mfululizo ule wa maswali, lile jitu la kutisha, likapiga makofi tena, mara akabadilika na kuwa binadamu wa kawaida, akiwa amevalia suti nyeusi.
Akapiga hatua za taratibu mpaka alipokuwa amesimama Vincent. Akampa mkono, bila hiyari yake, mkono wake ukaenda kwa yule mtu.

“Karibu sana nyumbani, karibu...” akamwambia, Vincent akizidi kutetemeka kwa woga.
“Ahsante sana, ahsante...” bila kutarajia kinywa chake kilifunguka na kutoa maneno hayo.
Hata yeye alishangaa kusikia sauti yake akiwa hana nia ya kuyataamka.

“Tunashukuru sana kwa kututembelea, sijui niseme nini juu ya shukrani zetu, lakini labda niseme ahsante sana. Umekuwa ukitupatia chakula mara nyingi sana, hata tukiwa tumekaukiwa kabisa, wewe umekuwa mkombozi wetu. Ahsante sana Vincent mwanangu...” yule mtu wa maajabu akasema akitabasamu.

Yalikuwa maneno mazito ya kuchanganya kidogo. Hakujua ni chakula kipi hasa ambacho alikitoa kwa yule mtu.
“Kwa bahati mbaya sana, nia yako haiwezi kutimia, lakini tutakupa zawadi nyingine. Tunafahamu kuwa nia yako ilikuwa ni kumuoa binti yetu Vera, lakini hilo halitawezekana!”

“Haitawezekana?” Vincent akang’aka, sasa kwa hiyari yake mwenyewe.
“Ndiyo, hutaweza kumuoa Vera. Hata kama tukikuruhusu, mtashindwana. Ni heri kama unataka kuishi na jamii yetu, tukupatie mwanamke mwingine, tena uishi huku!”
“Huku ni wapi?”

“Utajua baadaye, lakini labda nitangaze kuwa, tangu sasa nimefungua rasmi sherehe hii...Vincent, sherehe hii ni kwa ajili ya kukupongeza...nitakupa ofa ya kulala na Vera kwa siku moja tu na utakuwa hapa kwa siku mbili halafu baada ya hapo utarudishwa kwenu, uendelee na shuguli zako kama kawaida, ambazo zitakuwa na mafanikio makubwa sana,” akasema makofi yakipigwa.
Vincent hakujibu kitu!

Ikatolewa amri kuwa watu wote wafumbe macho, wakafumba. Walipoambiwa wafumbue, Vincent akashangaa akiwa tayari ameshaketi kwenye kiti cha kupendeza, Vera na wapambe wake wakiwa karibu yake. Vyakula vya kila aina mezani. Kwakuwa alikuwa anahisi njaa sana, hakuona sababu ya kujivunga. Akala nao kwa pamoja, huku muziki ambao mpaka sasa hawezi kuuelezea, ukisikika!

Hakuona sababu za kushtuka tena wala kushangaa, maana alishaona kwamba sehemu ile ni ya maajabu tu! Akaamua kuyaacha mambo yaende yenyewe, kama ni ndoto iishe yenyewe na kama ni kweli basi uendelee mpaka mambo yatakavyokuwa vinginevyo.

Katikati ya chakula, akashangaa wahudumu wakipitisha vinywaji, kwa macho ilionekana kama ni maji ya matunda. Akamiminiwa kwenye glasi na kupeleka kinywani moja kwa moja. Akagutushwa na rangi za midomo ya Vera na rafiki zake, ilikuwa myekundu kabisa, alipowachunguza vizuri, akagundua ilikuwa ni damu!
Alipoangalia glasi yake, ilikuwa ni damu!

“Juisi ya damu, hapana siwezi kunywa!” Vincent akasema.
“Acha ujinga, baba akisikia atakuua, kunywa...” Vera akamnong’oneza Vincent ambaye aliamua kunywa japo kwa shingo upande.

Baada ya chakula, yule baba akamfuata na kumpatia kipande cha kitambaa chekundu, akimwambia; “Huu ndiyo utajiri wako, ndiyo zawadi pekee ambayo tunakupatia kwa kazi uliyotufanyia....sasa mnaweza kwenda kupumzika na Vera, kesho asubuhi utarudishwa kwenu. Nata ujue kwamba, uko kwenye ufalme wa giza, sisi ni majini na mimi ndiye mkuu wao, binti yangu alikupenda sana, na mimi nikamwagiza awe na wewe kwa muda, lakini ahakikishe tunapata chakula, muda wenyewe umeshaisha.”

Ukumbi mzima ukalipuka kwa makofi, mbinja na vigelegele. Mara Vera akasimama, katika hali ya maajabu sana, Vincent naye akajikuta amesimama na kumshika Vera mkono, katika maajabu yale yale, akashanga akitembea tena kwa kumwongoza Vera kuelekea lango kuu la kutokea. Makofi yakiendelea.

Vincent akashangaa akihisi kichwa chake kuwa kizito kidogo, mara akahisi kama furaha fulani hivi moyoni. Wakiwa wanatokeza kwenye lango kuu, gari la kifahari likafunguka milango. Vincent ndiye aliyempakiza Vera garini. Safari ikaanza.

Haikuwa safari ndefu sana, kwani dakika kumi tu baadaye waliingia kwenye geti kubwa la kifahari, mlangoni kukiwa na walinzi. Vera akamwongoza mpaka chumbani. Wakavua nguo zote na kuwa watupu! Wakaenda bafuni kuoga, waliporudi wakaanza michezo ya kimahaba. Haukupita muda mrefu sana, walikuwa wameshahamia katika ulimwengu mpya wa kupendeza. Ulimwengu wa mahaba.

***
Kwa dakika tano sana anaendelea kukazia macho darini, ni kama alikuwa amepigwa bumbuwazi, kwani hakuelewa chochote kilichokuwa kikiendelea. Alipotingisha kichwa kwa nguvu, akagundua wazi kwamba alikuwa hotelini, akafungua pazia na kuangalia nje, akaoga jua changa la asubuhi likipendezesha Jiji la Dar es Salaam.

Akayarudisha macho yake kitandani, Vera alikuwa amelala usingizi kabisa. Vincent akashtuka sana. Hapo akahisi kwamba alikuwa kwenye ndoto mbaya ya kutisha. Akamtingisha Vera na kumtaka aamke, akashutuka.
“Vipi Vincent, mbona unanishtua hivyo mpenzi wangu?” Vera akasema akimwangalia Vincent kwa jicho la uchovu.
“Amka...hukumbuki ahadi yetu?” Vincent akasema akipuuza matukio yote aliyoyaona usingizini.

“Ahadi gani?”
“Uliniahidi nini jana?”
“Ok! Angalia saa ukutani, ni saa ngapi saa hizi?”
“Saa 4:45 asubuhi!”

“Na muda mfupi uliopita tulikuwa tunafanya nini? Mbona Vincent una vituko hivyo, hujafanya mapenzi na mimi mume wangu? Kwanza nimekupeleka mpaka kwetu, tumekaa siku mbili nzima na tumeondoka na gari pamoja, tukaenda chumbani...” Vera akasema huku uso wake ukijenga makunyanzi makubwa.

“Vera una nini?” Vincent akasema akiamka na kuvaa haraka.
Akashuka ngazi haraka na kwenda barabarani ambapo alichukua taxi, safari yake ilikuwa moja kwa moja Kanisani. Akaenda ofisini kwa Mchungaji, lengo lake likiwa moja tu, kuvunja ndoa yake na Vera. Alipofika kwenye mlango wa ofisi ya Mchungaji, Vincent akagonga akiwa anatweta kwa hofu.

“Yes, come inn!” Mchungaji akasema.
Vincent akaingia!
Alichokutana nacho ofisini kwa Mchungaji, ilikuwa nusu azimie. Mchungaji alikuwa anaongea na Vera ambaye alikuwa akilia muda wote. Akashangaa sana, Vera alimuacha hotelini.
Amefikaje?

“Noooo Pastor, nooooo.....” Vincent akasema akitoka nje mbio.
Je, nini kitatokea? Endelea kufuatilia simulizi hii ya kusisimua
 
SEHEMU YA 02


Baada ya kushtushwa na matukio ya ajabu. Vincent anaamua kwenda kwa Mchungaji, lakini cha ajabu, anamkuta Vera akiongea huku akilia. Vincent akatoka mbio kwa woga. SASA Endelea...
Mchungaji alipigwa na butwaa, ni muda mfupi uliopita Vera alifika ofisini kwake akieleza matatizo ya mumewe Vincent, tena wakiwa na saa chache tu baada ya kufunga ndoa yao kanisani. Ndiyo, walikuwa na saa chache tu!
Saa 72 tu!
Mchungaji akasimama haraka na kutoka nje, akiangaza macho huku na kule, akamwona Vincent akikimbia. Mchungaji akaamua kumkimbiza huku akimuita jina lake.

“Vincent...Vincent...simama we’ kijana!” Mchungaji aliita akimkimbiza Vincent.
Mara Vice akasimama na kumwangalia Mchungaji huku akionekana kutweta kwa hofu. Macho yake yalikuwa yanazungumza vizuri sana, yakitoa ujumbe mzito, kwamba ndoa ile ilikuwa imemshinda.
Ndoa ilikuwa ndoano. Lakini Mchugaji alipata shida sana kichwani mwake, maana Vera naye alikuwa akilalamikia ndoa ile ile!

“Subiri kijana wangu, hapa upo katika mikono salama...nyumbani mwa Bwana! Unajua Mungu ana baraka tele, ambazo zipo kwa ajili yetu....mimi na wewe. Kwanini unakuwa na hofu? Kwanini hutaki kumtegemea yeye?
“Hata hivyo, ipo amri kuu tuliyoachiwa na Yesu Kristo. Alisema tupendane. Huna sababu ya kumchukia mkeo Vera. Kinachoonekana hapa, ni nguvu za shetani ndiyo zinataka kuwaharibu. Lakini kwakuwa tayari upo kwake yeye asiyeshindwa, hupaswi kuogopa tena,” alisema Mchungaji akimwangalia Vincent usoni.

“Nakuelewa Mchungaji lakini si kwa Vera.”
“Unamaanisha nini?”
“Vera si binadamu na kama ni binadamu, basi anatumiwa na shetani!”
“Sijakuelewa bado.”
“Sitaki kuishi na Vera! Tafadhali vunja ndoa yangu na Vera Mchungaji, sitaki tena kuishi naye.”
“Vincent mwanangu, ndoa ni agano, tena ni agano la milele. Halafu imeunganishwa na Mungu mwenyewe, hakuna binadamu yeyote ambaye anaweza kutengua, labda kwa suala la zinaa.”

“Lakini hii itavunjwa!” Vincent akasema kwa jazba.
“Hatuwezi, taratibu za kanisa hazituongozi hivyo, ukiachilia mbali kanisa, lakini hata maandiko hayatuagizi hivyo, ni vyema tukaheshimu haya maagizo.”
“Kwahiyo Mchungaji, kwa sababu imeagizwa hivyo, ndiyo mimi niishi na jini?”
“Si tabia njema kumuita binadamu mwenzako jini, rekebisha usemi wako.”
“Ni jini Mchungaji, kwanini nirekebishe?” Vincent akasema akionekana kuwa na mashaka na woga sana.

“Ok, sijui sababu za wewe kusema hivyo, ingawa nimekuambia si utaratibu mzuri. Hebu twende ofisini tukazungumze na Vera mwenyewe akisikia.”
“Hapana siwezi Mchungaji, naomba tuzungumze sehemu yoyote ile, lakini si ofisini na Vera asiwepo.”
“Hebu twende huku,” Mchungaji akamshika mkono wakielekea bustanini.
Wakaketi kwenye viti vya plastiki, kwa mtindo wa kutazamana.
“Enheee Vincent, hebu nieleze kwanini unamwita mwenzako jini?” Mchungaji akamwuliza, akimkazia macho.

“....ni habari ndefu Mchungaji, unajua leo ni siku ya tatu tangu tumefunga ndoa yetu....yaani ni saa 72 tu zimepita, lakini sijawahi kukutana kimwili na mke wangu na kama unavyojua, hatukuwahi kukutana kabisa kabla, kama maandiko yanavyoelekeza.
“Kila ninapomwambia, mwenzangu anakataa. Lakini pia, naamini unajua kuwa leo ni Jumatano, nimejua hivyo baada ya kuangalia kalenda ya kwenye saa yangu na magazetini asubuhi hii. Bila shaka nipo sahihi?”
“Ndiyo, upo sahihi kabisa, leo ni Jumatano, lakini kwanini umesema umejua baada ya kusoma magazetini?”

“Swali zuri sana Mchungaji. Jumamosi baada ya kufunga ndoa, tulikwenda ukumbini kufanya sherehe yetu na baadaye usiku sana, tulikwenda kwenye Hoteli iliyoandaliwa kwa ajili ya fungate letu. Huwezi kuamini, tangu nilipolala Jumamosi usiku kuamkia Jumapili, ndiyo nimeamka leo!” Vincent akasema.

“What? Ulilala usingizi wa aina gani huo? Na Vera naye?”
“Tuliamka naye sawa, tena mimi nilitangulia, nikamwamsha na kumuomba tendo la ndoa, bado alikataa, akasema tulishafanya muda mfupi uliopita, lakini nilipoangalia kwenye simu yangu, nikagundua ni Jumatano, nikashtuka sana na kuamua kuja huku Kanisani, chumbani nikiwa nimemwacha Vera, lakini cha ajabu, huku nako nimemkuta.”
“Hebu ngoja kwanza, umesema mlilala kwa siku tatu, kivipi?” Mchungaji akauliza akijiweka sawa kitini.

“Pastor, nikiwa usingizini, niliota ndoto ya ajabu sana, nikiwa katika sehemu nisiyoijua, kukiwa na viumbe wa ajabu na Vera mwenyewe. Nashawishika kusema kwamba ule ni mji wa majini, maana kulikuwa na kila alama.
“Lakini nilishtuka zaidi nilipoambiwa kwamba ile ilikuwa sherehe ya kunipongeza kwa kuwapelekea chakula. Sijui ni nini na kwanini mambo haya yanatokea....” Vincent akasema akianza kulengwa-lengwa na machozi.
“Unaweza kukumbuka matukio yote yaliyotokea huko?” Mchungaji akauliza.
“Yes Pastor!”
“Hebu nisimulie....”
Vincent akakaa vizuri na kuanza kumsimulia Mchungaji kila kitu. Mara kadhaa Mchungaji alionekana kusisimkwa na matukio yale, alipomaliza kusimulia, Mchungaji akamwambia afumbe macho, akaomba!

“Amen!” Vincent akaitikia baada ya sala kumalizika.
“Sikia nikuambie Vincent, Mungu hajawahi kushindwa, hashindwi na hatashindwa kamwe. Hili ni jambo dogo sana kwake, ambalo anaweza kulishughulikia na kila kitu kikawa sawa, ukaishi na mkeo kwa amani na upendo. Hebu niambie, mlikutana wapi kwa mara ya kwanza na Vera?”
“Ni habari ndefu pia Pastor, lakini nitakusimulia....”

Vincent ameshamweleza Mchungaji kila kitu kilichotokea na kwanini anataka ndoa yake yenye umri wa saa 72 tu, ivunjwe! Mchungaji akamtaka aeleze jinsi alivyokutana na Vera. Je, Vincent atasimulia nini? Wadau, hadithi ndiyo kwanza inaanza. Fuatilia...

Ilikuwa ni Jumatano, katikati ya wiki, eneo la Kanisa la Kilutheri, Usharika wa Azania Front, likiwa tulivu kabisa. Ni kawaida ya utulivu wa siku hiyo, hasa kutokana na ukweli kwamba huwa hakuna pilika-pilika nyingi katikati ya wiki. Ratiba ya siku hiyo ni Masomo ya Biblia jioni yake na shughuli za kawaida za Usharika.
Hata hivyo, kelele za magari yakipita pembeni mwa Kanisa hilo ni za kawaida sana kusikika, lakini siku hiyo Mchungaji Ngarango hakusikia, akili yake yote ilikuwa kwa Vincent ambaye alionekana kuwa na ushuhuda mzito sana.

Macho ya Mchungaji Ngarango yalikuwa yametulia vyema usoni mwa kijana huyu anayeonekana kuwa na majonzi sana ndani ya moyo wake. Hana amani. Hatamani tena ndoa. Hana furaha. Anaonekana ana huzuni na simanzi tele. Macho aliyokuwa akitazama siku tatu zilizopita wakati akifungishwa ndoa, yamekuwa tofauti kabisa na leo.
Leo ana macho mekundu, anayeonekana kukosa usingizi na kuwa na mawazo mengi sana kichwani mwake. Hitaji pekee lilikuwa kanisani, akiamini Watumishi wa Mungu wangekuwa na kitu cha kumsaidia.
“Vincent...” hatimaye Mchungaji akamwita.
“Yes Pastor!”

“Tafadhali, nisimulie. Nataka kukusaidia hili jambo, unajua katika macho ya Kimataifa ni jambo kubwa sana, lakini kwake yeye aliyetutuma kufanya kazi yake, ni kitu kidogo sana ambacho kinaweza kusambaratika kwa sekunde moja tu. Nipe stori yenu vizuri.”
“Sawa Mchungaji, acha nikusimulie...” akasema Vincent akitazama juu, akionekana kuvuta kumbukumbu zake vyema.

*****
Julai 27, 2003, Mbeya.
Alijaribu kufumbua macho yake kwa mara ya tatu sasa lakini anashindwa. Alihisi mwili wake unakuwa kama mzigo, lakini baridi kali iliyokuwa asubuhi hiyo, ilimfanya azidi kujisikia mchovu zaidi. Usingizi ulikataa kabisa kumtoka. Akavuta shuka vyema na kujifunika hadi kichwani. Akaendelea kulala.
Dakika tatu mbele, akakurupuka kitandani kwa kugutuka kidogo. Akaketi. Akapiga miayo mfululizo, kisha akavuta tena shuka baada ya kuhisi baridi kali. Ni kweli kulikuwa na baridi sana. Si ajabu kwa Jiji la Mbeya kuwa na baridi ya aina ile. Ilikuwa ni kawaida kabisa.
Akayatupa macho yake ukutani, ambapo yalikutana na saa, akakodoa macho vyema. Akaweza kuuona mshale mkubwa ukiwa kwenye nane na mdogo ukiwa katikati ya nane na saba! Ilikuwa ni saa 1:40 za asubuhi.

Saa mbili kaso-robo!
Huyu ni Vincent Bryson Minja, ambaye amekuwa akijulikana zaidi kwa jina la Vincent Minja, kijana mtanashati mwenye kuvutia kwa kila idara, ambaye kiasili ni mzaliwa wa Mkoa wa Kilimanjaro, akiwa Mchaga wa Marangu. Anatingisha kichwa akionekana kujilaumu kwa kuchelewa kuamka...
“Oh! Nimechelewa sana kuamka, nimechelewa...” akasema akijilazimisha kuamka na kuchukua taulo lake na kujifunga kiunoni.
Akapiga hatua za kivivu akilaumu asubuhi hiyo kufika, akafungua pazia na kuchungulia nje. Watu walikuwa katika pilikapika zao za kila siku kama kawaida.

“Mbeya bwana, unaweza kudanganyika na huu ukungu ukajua bado alfajiri kumbe kumekucha, acha nikimbie bafuni halafu nianze mizunguko yangu, halafu kesho lazima nirudi Dar, labda kama Mwakilasa ataniyeyusha na ule mzigo wangu.
“Halafu amebaki yeye tu, ndiye anayesumbua na fedha kipindi hiki sijui kwanini? Anyway acha nioge kwanza, halafu nikaonane naye, lakini naamini leo atanipa...akinipa tu, kesho narudi Dar. Hata asiponipa, bado itabidi niende Dar halafu atanibenikia,” akazidi kuwaza, akielekea bafuni.

Hakutumia muda mwingi sana huko, akawa ameshamaliza na kutoka akiwa tayari ameshajikausha maji yote mwilini. Akatoka kivivu akiwa bado hajakubali sawasawa kwamba kulikuwa kumekucha. Akatoa suruali ya kitambaa ya rangi nyeusi na kuvaa, baada ya hapo akachukua fulana ya kubana shingo akavaa na kuchomekea ndani ya suruali yake.
Akaketi kitandani kisha akavaa soksi zake na kuingiza miguu ndani ya viatu maridadi. Akasimama na kujongea kabatini, akatoa koti la ngozi lenye rangi ya damu ya mzee! Akavaa na kusogea kilipo kioo. Akamwangalia kwa makini sana mtu aliyekuwa akionekana kwenye kioo.
Alikuwa amependeza sana. Alikuwa na nywele fupi, nyeusi zilizonyolewa sawaswa zikiwa zimelingana zote. Ndevu zilizochongwa vizuri na kuzidisha umaridadi wake, kifua cha mazoezi na kiuno cha kiume! Alikuwa amependeza sana.

“Mh! Jamaa kapendeza sana,” akasema mwenyewe kwa sauti akicheka.
Alikuwa yeye!
Taswira yake ndani ya kioo!
Akachukua manukato na kujipulizia. Akajirudisha tena kwenye kioo kile, akakikonyeza na kucheka, kisha akarudi kweye kochi na kuchukua kompyuta yake ya mkononi, akaiwasha na kuonekana kukagua baadhi ya mafaili yaliyomo ndani yake. Kisha kwa haraka sana, kama ambaye hakukusudia kufanya hivyo, akachukua mkonga wa simu iliyokuwa mezani, akapiga Mapokezi.

Haikuita muda mrefu, sauti nyororo ikasikika...
“Almas Hotel, Mapokezi nikusaidie tafadhali...”
“Yes, nimepiga hapo,” sauti nzito ya kiume, iliyopangika vyema ikasikika kupitia ngoma za dada wa Mapokezi.
“Nikusaidie tafadhali.”
“Nipo room no. 206, ghorofa ya tatu, nahitaji breackfast chumbani kwangu!”
“Sawa kaka, kawaida huwa tunatoa ofa ya maziwa, rangi, maji ya matunda, slesi za mkate, matunda, mayai mawili ya kukaanga au kuchemsha na maji ya kunywa. Sijui utapenda nini au utaagiza vingine vya gharama yako...!”

“Nahitaji chai ya rangi, slesi na juice inatosha!”
“Ok! Maji ya kunywa hutahitaji?”
“Nadhani ninavyotaka nimekwishakuambia!”
“Ok! Kaka, usijali.”
“Baada ya muda gani?”
“Vyote ulivyotaja vipo tayari, dakika mbili zijazo, Mhudumu atakuwa chumbani kwako.”
“Ahsante sana.”
“Karibu.”
“Nashukuru!”

Dakika mbili baadaye, alipelekewa kifungua kinywa, akanywa chai yake haraka, kisha juice na kujiandaa kutoka. Nukta chache baadaye alikuwa kwenye ngazi akishuka chini. Akiwa ghorofa ya pili, akakumbuka simu yake aliyoisahau. Akarudi haraka na kuichukua. Akawasha.
Akaanza kushuka chini kwa kasi ile ile, simu ikaanza kulalamika. Kwanza alipowasha tu, meseji kama sita hivi zikaingia kwa wakati mmoja. Hakujali. Akaendelea kushuka, alipofika chini, akakabidhi funguo Mapokezi na kutoka nje ya Hoteli ile, akaingia kwenye taxi moja iliyokuwa pale kijiweni.
“Wapi bro?”
“Mwanjelwa!”
“Elfu tatu!”
“Endesha gari kaka.”

Gari likiwa kwenye mwendo, Vincent akaanza kufungua zile meseji kwenye simu yake. Akashtuka sana. Hakuwa na taarifa kabisa na zile meseji, zilikuwa ni meseji za kumpongeza kwa kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa. Akatabasamu!
“Kumbe leo birthday yangu?!” Akasema kwa sauti akitabasamu.

Akaendelea kusoma zile meseji nyingine, mpaka alipofikia iliyomfurahisha vizuri. Ilimfurahisha kwa sababu mbili; Kwanza ilitoka kwa mtu ambaye hakutegemea kama angekuwa makini na siku yake muhimu kama hiyo, lakini pia ujumbe wenyewe! Ilikuwa imeandikwa hivi;
I’m so blessed 2 have a friend like u
This comes with many
Loving thoughts & warm wishes
I send 2 u...
May ur day be filled with laughter and on this special day may the finest things.
In life always come ur way
Happy birthday!

Ujumbe huo ulitoka kwa Genoveva, mwanamke ambaye siku zote aliota awe wake, lakini Geneveva, alisisitiza wabaki kuwa marafiki tu, kwakuwa hajisikii kumpenda kimapenzi. Alikuwa na maumivu siku zote, lakini siku hiyo akatabasamu. Alifurahi sana kupata ujumbe kutoka kwa Genoveva tena katika siku yake muhimu kama hiyo.
Siku ya kuzaliwa!
Akatabasamu tena!

“Ngoja nimpigie,” akawaza Vincent moyo wake ukienda mbio kwa furaha.
Aliwaza huenda ombi lake la siku nyingi lingekubaliwa. Haraka akabonyeza kitufe cha kijani, kuruhusu simu itoke, majibu aliyopewa kwenye simu yake yalimnyong’onyesha!
“Simu yako haina salio la kutosha kupiga simu, tafadhali ongeza fedha kwanza kabla ya kujaribu kupiga simu nyingine....” akaikata haraka akionekana kuwa na hasira.
“Nishushe hapo,” akamwambia dereva bila hiyari yake, alikuwa bado hajafika.

Je, nini kitatokea? Genoveva ni nani na ameingia vipi kwenye stori ya Vincent alivyokutana na Vera?
 
SEHEMU YA 03


Vincent akiwa kwenye taxi akielekea Mwanjelwa, anasoma meseji nyingi kwenye simu yake ambazo zinampongeza kuadhimisha miaka kadhaa ya siku yake ya kuzaliwa.
Lakini sms ya Genoveva inamfurahisha zaidi, Genoveva mwanamke ambaye anautesa moyo wake siku zote. Haraka akabonyeza kifute cha kijani ili kumpigia, lakini akajibiwa simu yake haikuwa na salio. Akamuamrisha dereva asimamishe gari haraka. Endelea...

Aliona kama bahati ya kipekee, kupokea meseji ya Genoveva ikimpongeza katika siku yake ya kuzaliwa. Lakini alipata kazi kubwa sana kukumbuka kama aliwahi kumwambia juu ya siku yake hiyo muhimu.
Hata kama alimwambia, anajaribu kutazama umuhimu wa siku hiyo kwa Genoveva ambaye siku zote alisisitiza wabaki kuwa marafiki tu!
Bado anahema kwa kasi, akimtazama dereva kwa hasira ambaye hakuonekana kuwa na dalili za kutii agizo lake.

“Oyaa bro, hujanisikia au?”
“Nimekusikia.”
“Sasa mbona husimami?”
“Eneo baya hili kaka, subiri kidogo hadi hapo mbele, vipi Mwanjelwa huendi tena?”
“Nataka kuchukua vocha kwanza.”
“Lakini mbona hata hapo utakaposhukia utapata? Isitoshe si mbali sana, kutoka hapa, ni kama dakika mbili tu, tutakuwa tumefika.”
“Mimi si mgeni hapa jijini, naijua Mbeya vizuri sana, hata ninapoenda pia napajua, lakini nataka kushuka hapa, kwanini hutaki?”
“Ok! Naegesha hapo mbele,” akasema dereva akionekana kukubaliana na Vincent.

Akashuka haraka na kulipa pesa kwa dereva kisha akapiga hatua za haraka akielekea dukani. Akanunua vocha ya Mtandao wa Ellycom, akaondoka zake. Akatafuta sehemu iliyotulia na kuanza kuingiza ile vocha kwenye simu yake.
Kwa zaidi ya mara tatu sasa amekuwa akiingiza, lakini jibu analorudishiwa ni kwamba namba zimetumika!
Akajaribu tena, jibu lilikuwa lile lile! Akarudi haraka kwenye lile duka alilonunua ile vocha.
“Ebwana vipi, mbona hii vocha kila ninapoingiza naambiwa imetumika?”
“Umeingiza vizuri ndugu?”
“Ndiyo!”
“Hebu lete...” yule muuza duka akamwambia na kuchukua ile vocha pamoja na simu.

Naye akajaribu kuingiza, lakini akashindwa, alipouliza salio kwenye simu, likaonesha hakukuwa na fedha! Akapigwa na butwaa, akabaki kumtazama Vincent ambaye alianza kukasirika akidhani kwamba alikuwa na nia ya kumtapeli.
“Hata hapa inaonekana imekwishatumika.”
“Imetumika wapi sasa, kama simu yenyewe ndiyo inaonesha haina salio?”
“Kwani hii vocha nimekuuzia ikiwa imefutwa?”
“Hapana.”

“Sasa kwanini unanilaumu?”
“Nipe simu yangu!” Vincent akasema kwa hasira.
Akapewa.
Akaondoka zake, akiwa na vocha yake mkononi, lakini mara akapata wazo, wazo ambalo kwa hakika lingekuwa suluhu la tatizo lake; Alitakiwa kupiga namba za Huduma kwa Wateja ili awaeleze tatizo hilo. Ndivyo alivyofanya.
“Ellycom Customer Care, naomba kukusaidia tafadhali,” ilikuwa sauti laini ya msichana mwenye simu.
“Yeah, nimepiga hapo, nahitaji msaada wenu tafadhali.”
“Jina langu naitwa Vera, nitajie jina lako, namba yako ya simu na shida yako tafadhali,” sauti ile laini ilizidi kumpa mateso ya ghafla Vincent.

“Naitwa Vincent Minja, namba yangu ni 0543 12333312, napiga simu kutoka Mbeya...tatizo langu ni kwamba, nimenunua vocha muda mfupi uliopita, lakini nilipojaribu kuingiza, nikaambiwa imetumika, ndiyo maana nimewapigia!”
“Ni ya shilingi ngapi?”
“Elfu kumi!”
“Unayo hiyo vocha hapo?”
“Ndiyo!”
“Nitajie namba zake!”

Vincent akataja zile namba. Baada ya muda mfupi, yule dada aliyejitambulisha kwa jina la Vera, akamwambia kulikuwa na matatizo ya kiufundi siku hiyo, ndiyo maana ikaonekana vocha imeshatumika, lakini akamhakikishia vocha hiyo ingekuwa imeshaingia ndani ya saa 3!
“Ok! Nashukuru sana.”
“Nawe pia, nakutakia siku njema Vincent, endelea kutumia Ellycom!”
“Ahsante.”

Baada ya kukata ile simu, akaanza kuhisi kitu tofauti ndani ya moyo wake, alihisi kama unakuwa mzito na kuanza kushawishiwa sana na ile sauti ya yule dada.
“Kama ni maajabu, haya yatakuwa ya kwanza, eti naanza kumpenda. Hivi nimechanganyikiwa? Nawezaje kumpenda mtu ambaye sijawahi kumuona? Halafu ni kama uchizi, maana siwezi kuonana naye....kwanza hata mawasiliano naye sina, sasa si maajabu haya jamani?!” Akasema akicheka kwa sauti ya chini.

Akaamua kwenda kununua vocha nyingine, akisubiri ile nyingine iingie baadaye. Akiwa sehemu tulivu kabisa, akijiandaa kumpigia Geneveva, mwanamke aliyeuteka moyo wake, simu yake ikaita, alipoangalia kwenye kioo cha simu yake, akakutana na jina ‘My Dady’. Alikuwa ni baba yake mzazi, mzee Minja!
Akapokea.
“Uko wapi mwanangu Vice?” Lilikuwa swali la kwanza baba yake kumuuliza mara baada ya kupokea simu.

Haikuwa utaratibu wa baba yake, siku zote alianza na salamu na utani kidogo, kwani baba yake alimfanya kama rafiki yake wa karibu, lakini sauti yake nayo ilimpa picha fulani, kwamba kulikuwa na matatizo.
“Mbeya baba.”
“Wewe ni mwanaume mwanangu, tafadhali pokea taarifa hizi za masikitiko kama zilivyo, tuliza moyo wako na uwe na subira, mdogo wako Andrew hatunaye tena duniani...” mzee Minja alitamka simuni kwa tabu akijitahidi kuficha simanzi yake.
“What?!! No dady, noooooo....” Vincent akaropoka.
Haikuwa rahisi kupokea taarifa zile mbaya za kifo cha mdogo wake mpendwa.

Ni muda mfupi tu, alitoka kusoma ujumbe wake wa pongezi ya siku yake ya kuzaliwa, sasa anaambiwa amekufa? Ilikuwa vigumu sana kuamini!
Vigumu mno!
Machozi machoni mwa Vincent yakaanza kumiminika kama maji! Hakutaka kukubaliana na ukweli ule.
ALIJITAHIDI sana kujikaza, lakini alishindwa, alikuwa katika hali mbaya sana. Ni muda mfupi tu, mdogo wake alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi katika simu yake akimpongeza kwa kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa, mara hii anapokea simu kwamba amekufa?
Hilo liligoma kabisa kuingia kichwani mwake, akawa kama aliyechanganyikiwa. Simu ipo sikioni, ameishikilia vizuri kwa mkono wake, lakini hawezi kuzungumza chochote.

Moyo wake ukazizima!
Ukapiga kambi kwa mshtuko!
“Vice mwanangu!” Baba yake akaita.
“Dady...Andrew kanitumia meseji muda mfupi uliopita, please kama unapima mapenzi yangu kwa mdogo wangu, naomba utafute njia nyingine,” alisema Vice, akiwa haamini kabisa alichokuwa akikisikia kutoka simuni.

“Wewe ni mwanangu mpenzi, rafiki yangu namba moja, siku zote nimekulea hivyo. Nakiri kwamba nimekuwa nikitaniana na wewe kwa mambo mengi, lakini si hili la ndugu yako kufa. Andrew hayupo tena nasi.”
“Nini tatizo?”
“Mwanangu hata sisi tunashangaa....imekuwa ghafla sana.”
“Nimekuelewa baba, najua ni ghafla. Nini kimesababisha kifo chake ghafla kiasi hicho?”
“Ngoja nikuambie...”

******
Alidamka asubuhi kuliko siku zote, akionekana mwenye furaha sana. Alianza kufanya usafi kwenye zizi la ng’ombe, akawapa na chakula.
Akaingia kwenye banda la kuku, akafanya usafi na kuwapa pumba, akachukua fyekeo na kufyeka ukoka vyema, akamwagilia maua maji na kufanya mandhari ya nyumbani kwao kuwa mazuri na ya kuvutia sana.
Alimaliza kazi zote za nyumbani saa 1:00 za asubuhi. Akarudi chumbani kwake, akajifunga taulo na kuingia bafuni. Akiwa anavaa akijiandaa kutoka kwa mihangaiko yake ya siku hiyo, akakumbuka kitu...

“Mh! Leo ni birthday ya brother Vincent, natakiwa kufanya kitu...ngoja nimtumia angalau meseji ya pongezi,” akawaza akiiendea simu yake.
Huyu ni Andrew, mdogo wake na Vincent, ambaye walikuwa wanafuatana. Walipendana kuliko watoto mapacha. Andrew akatoka taratibu akitabasamu, huku vidole vyake vikiandika ujumbe mfupi. Akaingia sebuleni na kuketi mezani. Mara mama yake akatokea.
“Shikamoo mama!”
“Marhaba mwanangu, vipi baba umeamka salama?”
“Salama mama, nataka kwenda Taveta mara moja.”

“Mbona kama umechelewa kuamka leo?”
“Nimechelewa? Mama bwana, hebu toka nje, ndiyo utajua kama nimechelewa kuamka au nimewahi.”
“Una maana gani?”
“Si utoke mai (mama) jamani?”
“Haya, ngoja nione.”
Mama yake akatoka nje, akastaajabu jinsi mazingira yalivyokuwa katika hali ya kuvutia. Hakuhitaji mtu yoyote kumwambia kwamba aliyefanya usafi ule alikuwa ni Andrew. Alimjua mwanaye vizuri sana kwa jinsi anavyopenda mazingira.

“Ndiyo maana nakupenda Andrew mwanangu, unajua naona faida ya wewe kubaki hapa nyumbani, kaka zako wote wamekimbilia huko mijini, lakini wewe uko hapa. Hongera sana mwanangu.”
“Usijali mama, ni wajibu wangu kuwafanya wenye furaha. Acha nikimbie mama, nisije kuchelewa!”
“Chai?!”
“Nitakunywa njiani mama, time...” akasema Andrew akitengeneza tabasamu pana.

“Kwanini mwanangu? Nachemsha maji na mayai yako mawili mara moja, upashe utumbo kidogo!”
“Ahsante kwa kunijali mama, lakini naomba uniruhusu niondoke, hata jioni nitakula tu mama.”
“Nikupikie nini?”
“Ukipika machalari (ndizi nyama) nitafurahi zaidi, halafu utumbo uwe mwingi!”
“Sawa baba, nitakupikia mwanangu. Ufike salama na kazi njema pia.”

“Ahsante sana mama nawe ubaki salama.”
Wakashikana mikono na kuagana. Andrew akaingia garini na kuondoka taratibu. Ni kijana mpole, mwenye upendo kwa wazazi wake, na hii ndiyo sababu iliyomfanya akatae kwenda kutafuta maisha mijini, akitaka kuwasaidia wazazi wake Marangu.
Akiwa njiani, kuelekea Taveta, akipita Marangu Mtoni, ghafla akahisi kichwa kuanza kumgonga. Aliamini ni maumivu ya kawaida ambayo yangeisha baada ya muda mfupi.

Lakini haikuwa hivyo, kila muda ulivyosonga ndivyo kichwa kilivyozidi kugonga. Baadaye akahiyari kuegesha gari pembeni. Akashuka na kwenda kwenye duka kununua dawa za kutuliza maumivu ya kichwa. Akanywa. Akahisi kikitulia kidogo.
Akarudi kwenye gari na kuendelea na safari yake, alipofika Himo, kwenye makutano ya barabara zinazoelekea Holili na Moshi akakata kushoto akiifuata barabara inayoelekea Holili. Baada ya mwendo kidogo, akaanza kuhisi tena maumivu makali ya kichwa. Mara ghafla, akamuona mwanamke mrembo mbele yake, akiwa mtupu huku akimtisha na kisu!

Akahisi ni jinamizi, lakini punde akaona ukungu umetanda mbele kwenye kioo cha gari, ghafla akasikia kizunguzungu kikali, kilichofuata baada ya hapo ni mlio mkubwa wa puuuuu!
Ilikuwa ajali mbaya sana! Gari la Andrew liligongana na gari kubwa ya mizigo aina ya Scania lililokuwa likitokea Kenya.
Andrew akafariki pale pale!

***
Muda ulikuwa umeshakwenda sana, lakini ilikuwa lazima aanze safari ya kwenda Marangu, Moshi kwa ajili ya taratibu za mazishi ya mdogo wake. Magari yote ya Arusha na Dar es Salaam, yalikuwa yameshakwenda!
Umuhimu wa safari hiyo, ukamfanya asafiri kwa kuunga-unga hadi Morogoro ambako alifanikiwa kupata basi la kwenda Dar alipofika usiku sana.
Akawasiliana na marafiki zake wote na kuwajulisha kuhusu msiba ule mzito kwake. Hakusita kumjulisha pia Genoveva ambaye aliumia sana.
“Jamani pole sana Vincent, amini ni kazi ya Mungu!”
“Nashukuru Genoveva.”

“Kuzikwa?”
“Hadi niende nyumbani kesho.”
“Pole sana, safari njema.”
“Nashukuru.”
Hata kama angeamua kubaki Mbeya, asubuhi yake angeweza kupata usafiri kwenda Moshi, lakini aliamua kwenda Dar kwa ajili ya kukamilisha taratibu muhimu kabla ya kwenda Moshi.
Saa nane za usiku, akiwa mchovu sana, akijaribu kusaka usingizi kwa tabu, aligutushwa na simu yake iliyokuwa ikiita. Akatazama kwenye kioo cha simu, hakuona jina. Zilikuwa namba za Mtandao wa Ellycom, akasita kidogo, lakini akapokea...
“Pole sana Vincent...” ilikuwa sauti ya taratibu sana ya mwanamke kwenye simu.

“Nani?” Vice akauliza kabla ya kupokea pole.
“Vera!” Sauti ile ikajibu, ikionekana kutoka kwa kujilazimisha kidogo.
“Vera?!” Vice akauliza.
“Ndiyo Vera!”
Vera ni nani hasa? Kwanini anampigia simu muda ule na amejuaje kuwa amefiwa? Vera....bado ubongo wake haukutaka kufunguka na kukumbuka alikuwa ni nani.
“Umesema unaitwa Vera?”
“Ndiyo!”
“Unajua unaongea na nani?”

“Yeah! Najua...”
“Ni nani?”
“Vincent Minja!”
“Sikiliza sister, ni usiku sana sasa hizi, halafu nina matatizo, sihitaji kuichosha sana akili yangu. hebu niambie, wewe ni nani hasa?”
“Vera wa Ellycom!”
Moyo wa Vincent ukalipuka!
Vera!

Akakumbuka kuwa ni yule aliyeongea naye asubuhi wakati alipopiga kwenye Kitengo cha Huduma kwa Mteja ya Kampuni ya Ellycom.
“Sasa umejuaje kama....hallow, hallow...” hakuchukua muda mrefu kugundua kuwa alikuwa akiongea kwenye simu iliyokatwa!
Alipompigia tena, alikuwa hapatikani! Vera alijuaje kama Vincent alikuwa amefiwa? Hilo likabaki kuwa swali lenye mateso makubwa moyoni mwake!
Wasiwasi moyoni!

Je, nini kitatokea?
 
SEHEMU YA 04


Vincent ameingia Dar usiku sana akitokea Mbeya kwa usafiri wa kuunga-unga. Alichokifanya ni kuwasiliana na ndugu zake na marafiki wote na kuwaeleza juu ya safari yake ya kwenda Marangu kwenye mazishi siku inayofuata.
Akampigia Genoveva mwanamke ambaye kwake alikuwa kila kitu, ingawa alikuwa akizungusha sana. Alipomaliza kuongea na Genoveva, akapokea simu ya Vera, ambaye alimpa pole, baada ya hapo akakata simu. Je, nini kitatokea? Fuatilia...

VINCENT alipata wakati mgumu sana, maswali mengi yakajaa kichwani mwake, akiwaza ni kwa jinsi gani Vera alijua kwamba alikuwa amefiwa. Lakini lingine ni kwa namna gani alipata namba zake.
Baada ya muda, akagundua kwamba, namba anaweza kuwa amezipata baada ya kumpigia simu ile asubuhi, lakini vipi ajue kuwa alikuwa amefiwa?
Akazidi kuwaza bila kupata majibu ya moja kwa moja. Alipojaribu kumpigia kwa mara nyingine tena, bado hakupatikana.
“Kuna nini kinaendelea?” Vincent akawaza bila kupata majibu.
Akajilazimisha kulala, baadaye akalala japo kwa taabu kidogo. Akaishilia usingizini.

***
Saa 11:00 za alfajiri, Vincent tayari alikuwa ameshafika katika Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani, Ubungo jijini Dar es Salaam. Akakata tiketi katika basi la Meridian, ambalo linafanya safari zake kutoka Dar kwenda Rombo.
Ilipohitimu saa 12:00 za asubuhi, basi likaanza safari. Njia nzima Vincent alikuwa na mawazo, lakini kubwa zaidi ni aina ya kifo cha mdogo wake, ilikuwa ghafla sana, ilikuwa mapema sana kwa Andrew kufa. Alikuwa na simanzi tele moyoni mwake.
Mchana wakiwa katika Hoteli ya Liverpool, Mombo kwa ajili ya chakula cha mchana, simu yake ikaita, alipotupia macho, akakutana na namba za Vera. Haraka akapokea...

“Vipi, salama?” Vera akamsalimia.
“Si salama sana, nina matatizo.”
“Pole.”
“Ahsante, mbona jana ulinikatia simu?”
“No! Simu yangu iliisha chaji!”
“Umejuaje kama nimefiwa dada Vera?”
“Umefiwa?”
“Ndiyo, nimefiwa na mdogo wangu!”
“Sijui, pole sana mwaya...”
“Mbona sikuelewi?”
“Kivipi?”
“Jana uliponipa pole si ilikuwa ya msiba au?”

“Hapana...nilikuwa nakupa pole kwa kazi za kutwa nzima, sasa mambo ya msiba ningejuaje?”
“Ok! Ndiyo hivi nimefiwa na mdogo wangu na hivi nipo Mombo naenda nyumbani Marangu kwa ajili ya mazishi,” Vincent akasema.
“Pole sana, safari njema pia.”
“Ahsante Vera.”
Wakakata simu zao.
Kwa Vincent bado alikuwa na maswali kichwani mwake, kwanini aliamua kumpigia simu, wakati hawafahamiani? Hilo akaliweka pembeni, akamalizia chakula chake kisha akarudi garini. Muda mfupi baadaye wakaendelea na safari.

***
Alishuka kituoni saa 8:00 mchana akiwa mchovu sana, akapiga hatua za taratibu kwa unyonge sana kwenda nyumbani kwao. Akiwa hatua chache tu, kabla hajaingia kwenye eneo la nyumba yao, akasikia muziki wa maombolezo ukilia kwa mbali, hisia kali zikamshika, machozi yakaanza kumtoka.
Akafika nyumbani, uso wake ukiwa umechakazwa kwa machozi, akapokelewa na wadogo zake ambao walianza kuangua kilio upya! Mama yake alipomuona, akachanganyikiwa zaidi, akaanza kulia upya hadi akazimia.

Ilikuwa lazima azimie, maana mama yake alikuwa anajua jinsi gani watoto wake Andrew na Vincent walivyokuwa wanapendana! Akinamama wakaanza kumpepea na kumwagia maji, robo saa baadaye akazinduka!
Siku iliyofuata watu walikusanyika nyumbani kwa mzee Minja kwa mazishi ya Andrew. Lilikuwa pigo kubwa sana kwa familia. Jeneza lenye mwili wa Andrew likabebwa mpaka kwenye kaburi lake, mbele kidogo ya nyumba yao, kulipokuwa na makaburi maalum ya ukoo! Baada ya maombi, mwili wake ukateremshwa kaburini!
Ndugu wakapita, wakitupia mchanga. Machozi yakatawala eneo zima, baadaye majirani nao wakatupia mchanga, kisha vijana wakapishwa kwa ajili ya kufukia. Punde, likaonekana tuta kubwa, ndani yake alikuwa amelala Andrew!
Katika nyumba ya milele.

***
Baada ya maziko, kikao cha ukoo kilikaa, tanga ikavunjwa na watu kuruhusiwa kurudi kwenye makazi yao kuendelea na shughuli zao za kila siku. Vincent akaomba kwenda na mdogo wake wa kike Mariana, akiahidi kumpa kazi ofisini kwake.
“Unajua mama, mara nyingi nasafiri, ndiyo maana naona ni bora niende na Mariana. Atanisaidia sana, maana watu wengine hawafanyi kwa moyo kama kazi yao, wanajua wameajiriwa tu,” alisema Vincent.
“Sawa baba, hakuna tatizo katika hilo, mnaweza kwenda,” baba yake akasema.
“Ahsante sana, nyie mbaki salama wazazi wangu.”
“Mbona unaaga mapema hivyo, si mnaenda kesho?” Mama yake akadakia.
“Oh! Kuchanganyikiwa huko...nimeshaanza kuona kama ndiyo tunaondoka!”
Wote wakacheka.

***
Walifika Dar usiku, kwasababu walichelewa kidogo kuondoka Marangu. Kwakuwa muda ulikuwa umeenda, hawakupata gari la moja kwa moja, kwahiyo wakalazimika kupanda basi mpaka Njia Panda, ambapo alipanda basi la kwenda Dar saa tano asubuhi!
Wakachukua taxi iliyowapeleka nyumbani kwa Vincent, Kinondoni. Hawakufanya kitu chochote zaidi ya kulala. Vincent akiwa usingizini, akakurupushwa na mlio wa simu. Alipoitazama, akakutana na jina la Vera. Akapokea...
“Samahani kwa kukupigia usiku Vincent, kuna kitu nataka kukuambia,” sauti ya Vera ikasikika ikiwa imejaa kitetemeshi.
“Ni nini Vera?”
“Niahidi hutakataa?”
“Sema kwanza ni nini?”
“Niahidi kwanza.”

ILIKUWA ni usiku sana, Vincent akiwa amepotelea usingizini kabisa, alishtuka sana, lakini alishangazwa na kauli ya Vera ambayo aling’ang’ania kwamba hawezi kuzungumza mpaka atakapomhakikishia kukubaliana na jambo lake.
“Lakini Vera, mbona unakuwa hivyo?”
“Vipi?”
“Mambo yako siyaelewi-elewi!”
“Kivipi?”
“Kwanza saa hizi ni usiku sana, kwanini umenipigia muda huu?”
“Ndiyo muda mzuri!”
“Muda mzuri? Unamaanisha nini?”

“Ndiyo muda ambao nimetulia kidogo!”
“Kwahiyo wewe hulali?”
“Nalala, ila nipo kazini, nimeingia usiku.”
“Lakini nimechoka sana, halafu ndiyo nimeingia usiku huu.”
“Kutoka?”
“Vera hujui kuwa nimetoka Marangu kwenye mazishi?”
“Ok! Sawa, nimekuelewa vizuri sana.”
“Enhee, ulikuwa unasemaje?”
“Nitakuambia, mbona una haraka sana?”
“Nataka kujua....”
“Lakini utakubali?”

“Vera ni vyema ukaniambia kwanza.”
“Ok! Sikia...nataka kukutana na wewe, unajua tumekuwa tukiwasiliana kwa simu tu, lakini hatufahamiani. Nahisi huu ni muda mzuri kwetu kukutana na kufahamiana zaidi.”
“Hilo tu au kuna lingine?”
“Ni hilo tu!”
“Lini?”
“Week-end hii.”
“Sawa.”
“Usiku mwema.”
“Nawe pia.”
Wakakata simu zao.

Vincent alibaki na maswali mengi kichwani mwake. Kwanza alishindwa kuelewa ni kwanini Vera alipenda kumpigia simu usiku, lakini pia akashangazwa na jinsi anavyohitaji ukaribu naye!
Akapuuzia, akaamua kuzima simu kabisa na kulala.

***
Ofisi ilikuwa kimya, kwenye kiti kikubwa cha kuzunguka alikuwa ameketi Vincent aliyekuwa kimya huku akiwatembezea macho watu wote waliokuwa ofisini kwake asubuhi hiyo.
Walikuwa jumla ya watu wanne, Matilda, Nice, Julius na Mariana, mdogo wake. Kilikuwa kikao cha utambulisho.
“Namshukuru Mungu, nimerejea salama na tumemaliza maziko salama...nawashukuru pia kwa kuwa karibu na mimi kwa muda wote niliokuwa kwenye matatizo. Nasema ahsanteni sana,” alisema Vincent akitabasamu.

“Pole sana bosi,” Nice, Sekretari wake alisema.
“Ahsante sana Nice.”
“Nimefurahishwa na utendaji wenu katika kipindi chote nilipokuwa sipo, nimepitia mafaili hapa, japo kwa juu juu, lakini inaonekana ni jinsi gani mnavyoweza kujiendesha wenyewe hata nikiwa sipo. Nimependezwa sana na hilo.”
Wote wakatingisha vichwa kumaanisha kwamba wameelewa.
“Huyu hapa, anaitwa Mariana...” akasema akimwangalia dada yake.
“She is my sister, tutakuwa naye hapa kuanzia leo, naombeni sana mumpe kila aina ya ushirikiano!”
“Usijali bosi, karibu sana dada Mariana,” Julius akasema akitabamu.

“Ahsante sana kaka, nashukuru.”
“Yes, Mariana, kutana na wafanyakazi wenzangu. Huyu hapa ni Julius, ndiye Afisa Masoko wetu, pale ni Nice, Katibu Muhtasi na Matilda ambaye ndiye Afisa Uhusiano, wengine utaendelea kufahamiana nao taratibu, lakini hawa ndiyo kama kampuni yenyewe maana ndiyo wasaidizi wangu wa karibu,” akasema akimtazama dada yake.
“Nashukuru sana bosi,” Mariana akasema akitabasamu.
“Thank you Mariana, nimefurahi sana kuniita bosi, maana niliwaza ungeniita kaka, lazima utofautishe nyumbani na kazini, vizuri sana.”
Wakatabasamu wote.

“Jamani, Mariana ni msomi, ana degree ya Business Administration, nina imani kwa elimu yake na ushirikiano wenu, atakuwa bora zaidi katika kutimiza majukumu yake.
“Kwasasa hatakuwa na nafasi yoyote, ataendelea kupata ujuzi kwanza, kabla ya kumpangia kazi yake, nawatakieni asubuhi njema na kazi njema pia,” akasema Vincent akiwa amechangamka sana.
Wote wakatawanyika. Ofisini wakabaki Mariana na Vincent.
“Inaonekana unafanya kazi nao vizuri sana,” Mariana akamwambia kaka yake.
“Ndiyo, kwani vipi?”
“Nimeona tu.”
“Vizuri, kwahiyo Mariana kama tulivyozungumza, lengo langu hasa ni kukufanya Meneja Mkuu wa hapa, ili uweze kusimamia vizuri Kampuni, lakini kwasasa endelea kusoma mazingira kwanza, sitaki kufanya haraka kuhusu hilo!”
“Sawa kaka....” Mariana akakatisha kauli yake.

“Mariana...”
“Sawa bosi!”
Wakacheka sana.
“Acha niendelee kukagua hizi ripoti, we’ nenda ofisini kwako, jitahidi kujifunza na kuzoea mazingira kadri uwezavyo!”
“Sawa bosi.”
“Ok, kazi njema Mariana.”
“Thanks.”
Mariana akaondoka na kumwacha Vincent mwenyewe akiendelea kupitia kazi mbalimbali kwenye mafaili. Kampuni ya Vincent ilijulikana kwa jina la Vinja Company Ltd, ambayo ilihusika na uagizaji na usambazaji wa majora ya vitambaa.
Ofisi yake ilikuwa Kariakoo, akiwa na wafanyakazi wachache, lakini mwenyewe akihangaika mikoani kusaka oda katika maduka mbalimbali. Ni kazi ambayo aliipenda na aliamini siku moja angekuwa na maendeleo makubwa kutokana na kazi hiyo. Hiyo ndiyo ilikuwa ndoto yake ya siku zote.

***
Pamoja na kumiliki kampuni yake, kuwa na gari la kutembelea pamoja na nyumba aliyojenga kwa pesa yake mwenyewe eneo la Kinondoni, jijini Dar es Salaam, hakuwa na mke. Tayari alikuwa ameshafikisha umri wa miaka 30, lakini hakuwa na mke wala mchumba.
Hilo liliwashangaza wengi. Hata Mariana, dada yake, naye alishangazwa na hali hiyo, kichwani mwake kulijengeka kitu tofauti, kwamba yawezekana kaka yake alikuwa na matatizo ya nguvu za kiume.

Usiku huu, wakiwa mezani wakipata chakula cha usiku, Mariana alijikuta akitamani sana kujua kama kaka yake ana tatizo lolote, ilimchukua muda kidogo kumuuliza, lakini baadaye akaona ni vyema kuuliza kuliko kukaa kimya.
“Kaka Vincent!”
“Yes sister,” Vincent aliitika akisita kidogo kula na kumwangalia dada yake usoni.
“Kuna kitu kinanitatizo kidogo, nataka kukuuliza.”
“Uliza tu, ni nini hicho?”
“Usinifikirie vibaya lakini, nina sababu za kukuuliza.”
“Sawa, uliza tu.”

“...unajua nina wiki sasa nipo na wewe hapa nyumbani, lakini sijaona wifi akija hata siku moja, vipi au kasafiri?” Mariana akauliza akionekana kuwa na woga kidogo.
“Kwanini umeniuliza swali hilo mdogo wangu?”
“Hapana, sina nia mbaya, natamani kumjua wifi yangu.”
“Mariana, wifi yako hayupo.”
“Hayupo kasafiri au huna?”
“Kwasasa sina.”
“Umri wote huo kaka, kwanini sasa?”
“Sina tu, lakini yupo msichana ninayempenda, nimeshamweleza ukweli wa hisia zangu, lakini bado ananizungusha.”

“Anaitwa nani?”
“Genoveva.”
“Amekukatalia kabisa?”
“Kabisa.”
“Sikia, fanya uwezavyo, umwalike nyumbani, nitambulishe kwake, halafu kazi inayobakia uniachie mimi...”
“Kweli Mariana?”
“Si umesema unampenda?”
“Sana.”
“Una uhakika?”
“Ndiyo!”
“Fanya hivyo.”

“Ok!”
Mariana aliuliza swali la msingi sana na pengine alikuwa na haki ya kuuliza vile, lakini Vincent alilipokea kwa namna tofauti. Alihisi mdogo wake alianza kumhisi vibaya. Kwamba pengine alikuwa na wazo kuwa yeye hajakamilika!
Kichwa kikamuuma.
ItaendeleA
 
Safi sana...

Mariana anahisi kaka yake siyo riziki...

Ngoja tuone... Vera ni jini...


Cc: mahondaw
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom