Mkakati kuvuruga uagizaji mafuta waandaliwa

sir.JAPHET

JF-Expert Member
May 18, 2012
699
133
*Makampuni matatu makubwa yahusishwa
*Mbunge wa CCM ashiriki mchezo mchafu

MPANGO wa Serikali wa kudhibiti bei ya mafuta kupitia utaratibu wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja (bulk procurement) upo hatarini.

Hatua hiyo inatokana na makampuni makubwa matatu yanayojishughulisha na biashara ya mafuta nchini kuandaa mkakati wa kuvuruga mpango huo wa Serikali.

Kampuni zinazodaiwa kuendesha mkakati huo ni Puma Enegy, Oraxy Enegy na Gapco ambazo zinataka kuubadili mfumo huo ziweze kudhibiti soko la mafuta nchini.

Taarifa za ndani kutoka kwa wadau wa mafuta zimeweka wazi kuhusu mkakati huo na kuitaka Serikali kuwa makini na kampuni hizo kulinda bei ya mlaji.

Kampuni hizo zinadaiwa kuendesha mkakati wa siri unaolenga kumng’oa Mwenyekiti wa Bodi ya Petroleum Importation Coordinator (PIC) ambayo inasimamia zabuni za mafuta.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, Mwenyekiti wa bodi hiyo ambaye ni Mbunge wa Kwimba, Mansoor Shanif Hiran, anaonekana kikwazo kwa makampuni hayo.

Mkakati mwingine unaofanywa ni kutaka kubadili mwongozo uliounda utaratibu huo wa kuagiza mafuta kwa pamoja kuzifanya kampuni hizo ziwe na nguvu kinyume na sasa.

Bodi hiyo inayosimamia zabuni ya uagizaji wa mafuta kwa pamoja unaundwa kwa mujibu wa sheria na kuzihusisha kampuni za Puma, Orxy, MGS, Moil, Camel Oil na Gapco.

Kwa mujibu wa muundo ulioandaliwa na Serikali bodi ya zabuni (PIC) inaundwa na makampuni sita ya mafuta. Kampuni mbili kati ya hizo zina zaidi ya asilimia 10 ya soko lote la mafuta nchini.

Kampuni hizo mbili ni Puma Enegy na Orxy, wakati kampuni kampuni za kati ni MGS, Camel Oil na Gapco na kampuni ya Moil, ambayo ina mtaji chini ya asilimia 5, ambayo kisheria ndiyo inayotoa mwenyekiti.

Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM) anadaiwa kuratibu mkakati huo kutokana na kuwa na uhusiano na kampuni ya mafuta ya Puma.

Mwenyekiti wa bodi hiyo zabuni ambaye pia ni Mbunge wa Kwimba, Mansoor Shanif Hiran (CCM) anawakilisha wafanyabiashara wadogo wa mafuta akipitia Kampuni ya Moil.

Makampuni hayo matatu yanadaiwa kutaka kuzinyang’anya kazi ya kuagiza mafuta kampuni ndogo zinazoshinda katika tenda, jambo ambalo limekuwa likipingwa na mwenyekiti wa bodi.

Makampuni hayo yamekuwa yakiipiga vita kampuni ya Agusta Enegy ambayo imeshinda zabuni kwa vipindi vitatu mfululizo kwa kuwa waagizaji wa bei ya chini.

MTANZANIA imebaini kutokana na hali hiyo kampuni hizo kubwa zimekuwa zikifanya mawasiliano na baadhi ya wasambazaji na kufanya uchakachuaji mafuta kwa lengo la kutaka kuiondoa sokoni kampuni Agusta Enegy.

Hata hivyo, utaratibu ambao umekuwa ukielezwa na EWURA, unaeleza kuwa baada ya mafuta hayo kuingizwa nchini watalaamu wa maabara kutoka EWURA na TBS hufanya ukaguzi kabla ya mafuta kuingizwa katika depoti za wafanyabiashara.

“Meli inapoweka nanga bandarini, kabla mafuta hayajashushwa, wakaguzi kutoka TBS na EWURA wanakuja kupima mafuta.

“Wakijiridhisha kuwa mafuta ni mazuri wanatoa cheti cha kuruhusu mafuta yashushwe, wakibaini mafuta ni machafu wanazuia, huu ndiyo utaratibu.

“Sasa makampuni haya yanafanya mchezo mchafu, mafuta yakipelekwa katika depoti wanayachakachua yakifika kwa walaji wanalalamika EWURA ili kampuni iliyoagiza mafuta ionekane haifai inaleta mafuta machafu, hizi ni hila,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Kampuni ya Agusta Energy mara zote imekuwa ikishinda zabuni kutokana na bei yake kuwa ndogo wakati wao wanataka bei ya mafuta iwe kubwa.

“Sasa kumekuwa na hali ya mizengwe dhidi ya kampuni hii hasa kutokana na hizi kampuni kubwa kuona kuwa zinakosa maslahi.

“Wanataka kumtoa mwenyekiti wa bodi na kampuni ya Agusta waitoe sokoni ili makampuni haya yashike hatamu wapeane zamu ya kuagiza mafuta.”

Naye Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM) anayetuhumiwa kuongoza mkakati huo, alisema yeye hahusiki na jambo lolote linalohusu PIC.

“Nataka nikwambie kuwa sekta ya mafuta nchini kwetu imeingiliwa na ina matatizo sana na katika hili hata jana nilikuwa na Mwenyekiti wa PIC, Mansoor nilimueleza hili kwa kina.

“Fitna na majungu kila kukicha mwongozo huandaliwa na EWURA na si PIC. Siku zote nasema muundo wa chombo hiki ni sawa na NGO’s ya watu fulani.

“Hao wanaosema mimi naingilia mambo ya PIC hata kidogo sina maslahi nayo zaidi ya kushauri sekta nzima ya mafuta hasa kupitia Bunge letu tukufu,” alisema Mwijage.
 
Back
Top Bottom