Mipasho haifai muziki wa Injili

Mipasho haifai muziki wa Injili

Mzalendo_Mkweli

JF-Expert Member
Joined
Jan 30, 2012
Posts
2,067
Reaction score
1,328
STAILI, vionjo na mfumo mzima wa muziki umekuwa ukibadilika kila siku kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo hali ya kwenda na wakati.
Mabadiliko haya kwa upande mwingine yamekuwa sababu ya changamoto ambazo nyingine zimeboresha mfumo mzima wa muziki kwa kunogesha, lakini pia yameharibu.
Lakini haya yote ni kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambayo yameikumba dunia.
Ingawa mabadiliko haya yalikwisha kutabiriwa katika vitabu vitakatifu, lakini kwa kuwa tumekosa maarifa na macho ya rohoni, ni vigumu kufahamu au kutambua na tumeendelea kuona kwamba ni mambo ya kawaida.
Nimeanzia mbali kwa kuhusisha na kugusia masuala ya kiimani zaidi na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, lakini uchambuzi wangu wa leo utazungumzia suala la waimbaji wa nyimbo za Injili kugeuza nyimbo hizo uwanja wa mipasho na mbwembwe za kutuonyesha kuwa wao ni mabingwa wa kukata viuno.
Ninasema haya kwa sababu sasa hivi karibu waimbaji wengi wa nyimbo za Injili tungo zao ni za kulalamika na kupigana vijembe, je, ndiyo huduma mliyoitiwa?
Wengine wamepoteza ramani kabisa na kusahau talanta za uimbaji walizopewa kwa kuanza kuimba nyimbo za dunia ambazo hazina maonyo yoyote, hazina hata mistari ya maandiko ya kuonyana lakini bado wanajiita waimbaji wa muziki wa Injili.

Hivi hatujiulizi ni kwanini wengine waliokuwa wakiimba nyimbo za duniani wamehamia kwenye nyimbo za Injili na wanaimba nyimbo zinazomtukuza Mungu kwa kumaanisha na wamefanya vizuri, wamefanyika baraka na uponyaji kwa wengine kupitia tungo zao za muda mfupi na kuwaacha nyuma wale wakongwe ambao wengine hivi sasa wamediriki kuwa waimbaji kwenye kampeni mbalimbali, hasa za kisiasa huku wakipata kashfa mbaya za kuupaka matope muziki wa Injili?
Je, mnakumbuka kwamba tulipatana dinari?
Sote tunafahamu kwamba nyimbo za Injili zipo kwa ajili ya kufundisha na kuonya mienendo isiyompendeza Mungu kama wanadamu, lakini pia kutuhubiria.
Lakini leo hii dhana ya muziki wa Injili imeanza kupotea kabisa kutokana na baadhi ya tungo kujaa vionjo vya mipasho ambavyo huwemo katika muziki wa kidunia.
Kwa mtazamo wangu, ujumbe wa neno la Mungu kufikishwa kwa staili ya mipasho, haipendezi na haiwezi kumbadili mtu kwani huwa kama mshale.
Unaweza kujiuliza, nini maana ya kusema kama mshale? Ni ule moyo ambao muda wote umejaa vijembe, visasi na manen0 yasiyofaa kwa ajili ya kukera nafsi ya mwingine.
Utakuta mwimbaji wa nyimbo za Injili mwanzo hadi mwisho wa tungo ni kulalamika na kumfumbia mtu mafumbo, jambo ambalo hata Mungu hapendi, lakini pia hakuna hata sehemu moja anapotajwa Mungu. Je, mtasema bado mnahubiri kwa njia ya nyimbo?
Kibaya zaidi, mnalalamika, ooh! Soko la muziki wa Injili limevamiwa, hatuuzi…mtauza nini wakati mnaimba mafyongo?
Tungo zenu hazina ujumbe ambao utanishawishi ninunue au nipende nyimbo zenu ili hata nikiwa nasikiliza napokea upak0, uponyaji na kupata faraja ya moyo, kwa kuwa mwimbaji alituliza akili akanena na Roho Mtakatifu akamwongoza aimbe nyimbo za aina fulani kwa utukufu wa Mungu.
Leo hii waimbaji wengi wa muziki wa Injili kilichobaki ni ustadi katika kucheza na kuzungusha viuno.
Yote haya yanakuja kutokana na kuimba kwa mazoea, hatumpi Roho Mtakatifu nafasi, hatusali, hatupati maono kuhusu ni nyimbo gani za kuimba.
Lazima tukubali kwamba hilo ni tatizo na lazima tubadilike katika hilo ili yale ambayo yamekusudiwa na Mungu yatimie.
Kwa upande mwingine, ninakubaliana na ninyi kwamba hamwezi kuimba nyimbo za aina moja kwa sababu zinawachosha wasikilizaji lakini kila jambo lina kiasi kama maandiko matakatifu yanenavyo.
Mbali ya yote, mnaweza kusema mbona mfalme Daudi alicheza hadi nguo zikaanguka, iweje utushambulie hivyo?
Siwashambulii, lakini pia ningependa kuwaasa kwamba ni vema mkatambua thamani ya huduma yenu, si busara kwa mwimbaji wa nyimbo za Injili akawa na albamu iliyobeba nyimbo ambazo hazimpi Mungu utukufu.
Kwa mtazamo wangu, ni vema waimbaji wa nyimbo za Injili mkajitambua, mkabadilisha namna ya uimbaji ili huduma na ujumbe mliokusudia ufike kwa jinsi ilivyokusudiwa, pia kwa kufanya hivyo mtaepuka kudharauliwa na wapenzi wa nyimbo zenu na kurudisha imani iliyopotea.
Lakini, waimbaji wa muziki wa Injili wanapaswa kuwa mfano bora wa kuigwa na wengine, si tu jamii bali hata wasanii wa muziki wa kidunia.
Kitendo cha baadhi ya waimbaji wa muziki wa Injili kuanza kupotoka na kutunga nyimbo zenye mipasho, itawafanya watu washindwe kutambua nini tofauti na muziki wa Injili na ule wa kidunia.

Source : http://www.freemedia.co.tz/daima/mipasho-haifai-muziki-wa-injili/
 
Back
Top Bottom