Stars, Cranes nusu fainali Tusker leo
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 9th December 2010 @ 23:59
Kikosi cha Kilimanjaro Stars
LEO ni leo kwa timu ya Taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' wakati itakaposhuka Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kumenyana na Uganda 'The Cranes' mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji.
Kilimanjaro Stars imefuzu hatua hiyo, baada ya juzi kuifunga Rwanda bao 1-0 katika mchezo wa robo fainali lililofungwa na Shadrck Nsajigwa, wakati Uganda yenyewe iliifunga Zanzibar kwa penalti 5-3 katika robo fainali juzi.
Ni mchezo ambao unakutanisha wachezaji wanaofahamiana na wanaokutana mara kwa mara iwe katika ligi hapa nchini ama michuano ya kimataifa.
Uganda inaye beki mahiri anayechezea Simba ya Dar es Salaam, Joseph Owino pamoja na washambuliaji wengine wawili pia wanaochezea Simba ambao ni Emmanuel Okwi na Patrick Ochan.
Pia Waganda wanaye mshambuliaji Robert Ssentongo ambaye amesajiliwa na African Lyon ya Dar es Salaam inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, ingawa msimu huu ameshindwa kujiunga na wenzake katika duru la kwanza la ligi hiyo.
Licha ya kusajiliwa na African Lyon, lakini Mei mwaka huu Ssentongo alichezea Simba katika michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati 'Kombe la Kagame' iliyofanyika Kigali, Rwanda.
Pia Waganda wanaye mshambuliaji Steven Bengo ambaye msimu uliopita alichezea Yanga ingawa hakung'ara na Danny Wagaluka ambaye alichezea Azam pia ya Dar es Salaam.
Kwa hiyo hao ni wachezaji ambao wanajulikana vyema uchezaji wao hapa nchini, ukali na udhaifu wao wote unafahamika.
Lakini pia wapo wachezaji ambao si wageni kucheza na timu ya Tanzania iwe Taifa Stars ama Kilimanjaro Stars, ambao ni Andy Mwesigwa, Mike Sserumaga, Kasule Owen na Mude Mussa, hivyo kwa lugha iliyo rahisi ni kuwa wachezaji wote wanajuana vilivyo.
Ni wazi beki ya Stars chini ya Kelvin Yondani, Juma Nyoso pamoja na Shadrack Nsajigwa watakuwa wanajua nini wanachokifanya kuwakabili Okwi, Ochan na Ssentongo.
Hali hiyo pia haitamsumbua washambuliaji wa Kilimanjaro Stars, Mrisho Ngasa na Nurdin Bakari ambao wanafahamu fika namna ya kumtambuka Owino, kwani si mara ya kwanza kukutana naye.
Ni mchezo wenye changamoto kubwa, ambao Kilimanjaro Stars inakumbana nao kwani Uganda licha ya kuwa ndiyo bingwa mtetezi, lakini pia imeonesha uwezo mkubwa kwenye mashindano hayo na si timu ya kubezwa hata kidogo zaidi ya kuwa ya kupigiwa mfano.
Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Mdenmark Jan Poulsen bila shaka atakuwa amefanyia kazi makosa kadhaa ambayo yalijitokeza kwenye michezo iliyopita, ambapo hadi sasa ukuta wa Stars umeruhusu bao moja katika michezo minne iliyocheza.
Uganda inafundishwa na kocha Robert Williamson ‘Boby' kutoka Scotland, ambaye karibu kila mechi timu yake imekuwa ikiimarika, hivyo ni wazi mchezo wa leo utakuwa na ushindani wa hali ya juu.
Nusu fainali nyingine leo itakuwa kati ya Ethiopia na Ivory Coast ambayo inatarajiwa kuwa ya vuta nikuvute.