Real yajipanga kuimaliza Barca leo Send to a friend Monday, 02 May 2011 20:02
MADRID, Hispania
LICHA ya kukabiliwa na mtihani mgumu dhidi ya Barcelona leo kwenye Uwanja wa Nou Camp, Real Madrid inajipa matumaini kuwa ina mbinu sahihi za kupata ushindi na kukuta tiketi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Real imetangaza kuwa itatumia kumbukumbu zile zile za mafanikio ya miaka ya nyuma na kufuta matokeo ya mabao 2-0 na kuiondoa Barcelona.
Mtandao wa klabu hiyo, Jumapili ulichapisha picha ya wachezaji wa klabu hiyo wakishangilia ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Nou Camp mwaka 2002 waliposonga mbele na kutwaa taji la tisa la michuano hiyo ya Ulaya.
Wachezaji wa zama hizo, Zinedine Zidane na Steve McManaman walifunga mabao usiku ule na timu hizo zikatoka sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Bernabeu, kisha Real wakailaza Bayer Leverkusen ya Ujerumani kwa mabao 2-1 katika fainali kwa mkwaju wa ajabu wa Zidane.
"Kila mmoja atakubali kuwa ni kazi ngumu, lakini matokeo hayo yanatupa matumaini," uliandika mtandao huo."Ni historia pekee ambayo tunatarajia kuitumia, lakini tuna imani kwamba tunaweza kuwashinda Barca ."
Kipa na nahodha wa Real, Iker Casillas aliongeza sauti katika hilo akieleza kuwa kila mmoja ana matumaini.
"Majina ya timu mbili ambazo zitacheza fainali baadaye mwezi huu bado hayajaandikwa," alieleza kipa huyo aliyeiwezesha Hispania kutwaa Kombe la Dunia mwaka jana.
Alisema: "Huwezi kujua katika soka, kitu kama hicho kinaweza kutokea. Tutaikabili Barcelona tukijua kwamba fainali ipo mbele yetu baadaye mwezi huu na timu nne zilizoingia nusu fainali zinaweza kufuzu."
Mchezo wa kwanza baina ya timu hizo ulitawaliwa zaidi na hasira, lakini mchezaji bora wa dunia, Lionel Messi alifunga mabao mawili na kuipa ushindi timu yake huku Real ikimpoteza beki wa kati, Pepe.
Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) limefungua malalamiko dhidi ya Real, Barca na kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho.Mourinho amelalamikiwa kwa kumdhalilisha mpinzani wake, Pep Guardiola akidai kuwa mafanikio yake ni ya kubahatisha huku Real ikiwatuhumu wachezaji wa Barca kwamba ni waongo.
Rais wa Barca, Sandro Rosell amejaribu kupunguza shinikizo la mchezo huo kwa kuwaomba mashabiki wa klabu yake wawe watulivu, wenye nidhamu katika mchezo huo wakitumia akili.
"Mashabiki wetu ni mfano wa kuigwa kwa tabia nzuri, nina hakika kwamba watafanya hivyo leo, Jumanne kwani macho yote ya walimwengu yatakuwa kwenye runinga.
"Ninawataka waiunge mkono timu yao, wasahau vitu vingine vyote, wajiepushe na uchokozi wa aina yoyote ."
Barca na Real ziliwapumzisha nyota wao na kufungwa katika mechi za Ligi Kuu, La Liga mwisho wa wiki. Barca walitangulia kufunga lakini wakalazwa 2-1 na Real Sociedad huku Real wakifungwa 3-2 na vibonde Real Zaragoza.
Lakini, kwa matokeo hayo Barca imeendelea kuongoza kwa tofauti ya pointi nane dhidi ya Real , zikiwa zimebakisha mechi nne.Ukuta wa Barca umeandamwa na majeruhi na Jumamosi walipata pigo jipya kwa kuwapoteza Gabriel Milito na Martin Montoya.
Lakini, kulikuw na habari njema kwa kiungo Andres Iniesta ambaye amekuwa majeruhi na kukosa mechi ya kwanza baina ya timu hizo baada ya Jumapili kufanya mazoezi.
Real itamkosa Pepe katika mchezo huo huku beki mwingine Sergio Ramos akiwa amefungiwa. Mourinho, ambaye alitolewa benchi kwa kadi nyekundu kwa kupinga kadi nyekundu ya Pepe atakuwa jukwaani akifuatilia mchezo huo.
"Madridismo inafahamika kwa upiganaji wake wa kutoka nyuma na kushinda," alieleza Mkurugenzi Mkuun wa Real, Jorge Valdano.
"Kama kuna timu inajivunia ushujaa , basi hakuna zaidi ya Real Madrid. Hakuna kitu kinachoweza kutuzuia kujiamini katika mchezo wa leo."
Katika mchezo wa Jumatano, Man United ambao wanaongoza Ligi Kuu England na waliofungwa 1-0 na Arsenal katika ligi, wataikaribisha Schalke 04 wakiwa na mabao 2-0 kibindoni. Fainali itachezwa Uwanja wa Wembley, London, Mei 28.