Kaseja, Ngasa, Fuso wagongana Taswa
• Hashim Thabit, Nizar, Mtagwa ndani
na Dina Ismail
MFUNGAJI bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2010/2011, Mrisho Ngasa, pamoja na kipa wa timu ya Simba, Juma Kaseja, ni miongoni mwa wanamichezo walioteuliwa kuwania tuzo ya mwanamichezo bora wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa).
Ngasa anayekipiga Azam FC ya jijini Dar es Salaam, Kaseja, beki wa Yanga Shadrack Nsajigwa ‘Fuso', pamoja na mchezaji kutoka Visiwani Zanzibar akikipiga katika klabu ya Zanzibar Ocean View, Khamis Mcha, watawania tuzo hizo ambazo hafla yake imepangwa kufanyika Mei 6, katika Hoteli ya Movenpick, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Taswa, Amir Mhando, aliwataja wanamichezo wengine kuwa ni pamoja na Asha Rashid ‘Mwalala', Mwanahamisi Omary ‘Gaucho' (Mburahati Queens) na Fatuma Omary (Sayari Queens) ambao watawania tuzo ya mwanasoka bora kwa upande wa wanawake.
Alisema tuzo nyingine itakayowaniwa ni ile ya Watanzania wanaocheza nje ambapo walioteuliwa ni pamoja na Hasheem Thabeet (kikapu), Henry Joseph, Nizar Khalfan (soka), Rogers Mtagwa (ngumi), ile ya wachezaji wa nje wanaocheza Tanzania itawaniwa na Emmanuel Okwi-soka (Simba), Yaw Berko-soka (Yanga) na Kanda Kabongo (kickboxing).
Kwa upande wa riadha (wanaume) wanaowania ni Samson Ramadhan,Marco Joseph na John Bazil huku kwa wanawake ni Zakia Mrisho, Mary Naali na Magdalena Mushi, katika wavu wanaowania kwa upande wa wanaume ni pamoja na Kevin Peter (Magereza Wanaume), Mbwana Ally (Mzinga Morogoro) na Ibrahim Cristopher ( Nyuki Zanzibar), huku kwa wanawake ni Hellen Richard Mwegoha (Magereza Wanawake), Yasinta Remmy na Zainabu Thabit (Jeshi Stars).
Wakati katika netiboli ni Lilian Sylidion (Filbert Bayi), Mwanaid Hassan na Sekela Dominick (JKT Mbweni ), huku katika karate kwa upande wa wanaume ni Sempai Steven Bella na Sempai Ayub Seleman, wakati kwa upande wa wanawake kuna jina moja ambalo haliwezi kutangazwa.
Walioteuliwa katika mpira wa kikapu kwa upande wa wanaume ni George Otto Tarimo (Savio-Dsm), Lusajo Samwel Mwakipunda (Oilers-Dsm) na Gilbert Batungi, huku kwa upande wa wanawake ni Faraja Malaki (Jeshi Stars-DSM), Zakhia Kondo (Lady Lioness-Dsm) na Doritha Mbunda ( JKT Stars).
" Karama Nyilawila, Mbwana Matumla na Francis Cheka watawania katika ngumi za kulipwa, huku katika ngumi za ridhaa watakaowania ni Revocatus Shomari (uzito wa Bantam), Selemani Kidunda (uzito wa Middle) na Said Dume (uzito wa Fly )", alisema Mhando.
Gofu (wanawake) ni Hawa Wanyeche, Madina Iddi na Vailet Peter, huku kwa upande wa wanaume ni Frank Roman, Adam Abbas na Isaac Anania.Katika Baiskeli inawaniwa na Hamis Clement, Richard Laizer na Said Jumanne kwa waunaume huku kwa upande wa wanawake ni Sophia Anderson, Martha Anthony na Ndashimba Kulia.
Katika mchezo wa kriketi (wanaume) wanaowania ni Kassim Nassor, Seif Khalifa na Benson Mwita huku kwa wanawake ni Hawa Salum, Mariam Said na Sophia Hemed. Tuzo ya mpira wa mikono kwa upande wa wanaume itawaniwa na Kazadi Monga (Magereza), Hemed Saleh na Abineri Kusena (JKT) na wanawake ni Happiness Mahinya, Zena Mohammed (JKT) na Teresia Kifukwe (Magereza).
Aidha, Mhando aliwataja watakaowania tuzo ya mwanamichezo chipukizi ni pamoja na John Bazil (riadha), Magdalena Cristian (riadha), Lilian Sylidion (netiboli) na Vailet Peter (gofu), wakati Khamis Azan Hussein, Abeid Omar Dola na Masoud Amour Kombo (Zanzibar) watawania tuzo katika mchezo wa judo huku tuzo ya heshima itatangazwa siku ya hafla.
Mshindi wa jumla katika tuzo hizo ambazo zimedhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) pamoja na Hoteli ya Movenipick atazawadiwa gari aina ya GX 100, lenye thamani ya shilingi mil. 13, pamoja na kulala usiku mmoja katika Hoteli ya Movenpick. Pia mshindi wa kila kipengele atazawadiwa shilingi mil. moja kila mmoja.