Real, Barca mbinu ndani nje Send to a friend Tuesday, 26 April 2011 20:52
MADRID, Hispania
KOCHA wa Real Madrid, Jose Mourinho yupo tayari kuifunga tena Barcelona hii ikiwa ni katika mechi ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya itakayochezwa leo jijini Madrid.Kama Real ikiifunga Barcelona na kuitoa katika mashindano hayo ya Ulaya, ikiwa ni wiki moja tangu ilipotwaa Kombe la Mfalme , basi utawala wa soka nchini Hispania utahama kutoka Barcelona na kwenda Madrid.
Mourinho ni kocha aliyefanikiwa akiiudhi Barca anapokutana nayo ingawa aliwahi kuwa kocha msaidizi wa klabu hiyo ya Catalan katika miaka ya 1990 wakati timu hiyo ilipokuwa ikifundishwa na Bobby Robson.
Mourinho wakati akiifundisha Inter Milan aliweza kuichapa Barcelona katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu uliopita na kuitoa.
Pia, Mourinho wakati alipokuwa akiifundisha Chelsea aliwahi kukutana na Barcelona mara tatu, ambapo mara mbili alifanya vizuri.
Harakati zake za kuisumbua Barcelona hazikuishia hapo kwa sababu hivi sasa akiwa na Madrid ameweza kutoka sare ya 1-1 na kuifunga Barcelona bao 1-0 na kutwaa kombe lake la kwanza akiwa kocha wa Real.
Hivi sasa Barcelona ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania, lakini Real Madrid ipo katika nafasi nzuri ya kutwaa taji la 10 la Ligi ya Mabingwa na Mourinho yupo katika nafasi nzuri ya kutwaa kombe hilo kwa mara ya tatu akiwa na timu tofauti.
Kuhusu mechi ya leo suala kubwa ambalo lilikuwa likizungumziwa ni kwamba waamuzi wanaweza kuipendelea Madrid pia mbinu ya kuachwa kwa nyasi ndefu kwenye uwanja wao wa Bernabeu ili kuzuia mchezo wa pasi wa Barcelona.
"Nyasi ni ndefu kwenye uwanja wa Bernabeu, lakini siwezi kulalamika, ni kawaida kwa Madrid kufanya hivyo wanapokutana na sisi, ni kama kinga yao ili kuzuia mchezo wetu wa pasi nyingi, Mourinho atatumia njia yoyote kutuzuia," alisema Gerard Pique.
"Lakini, Real Madrid hivi sasa ni timu nzuri ambayo ina washambuliaji wazuri sana,"alisema Pique.
Real Madrid imeonyesha kwamba inaweza kuwakabili wapinzania wao Barcelona kwa mbinu tofauti ambazo watu wengi hawakuzutarajia na kuondoa rekodi ya kocha Guardiola kushinda mechi timu hizo zinapokutana.
Madrid inajaza katikati ya uwanja viungo wakabaji watatu huku viungo hao wakiongozwa na beki wa kati ambaye amehamishwa na Mourinho kucheza nafasi ya kiungo mkabaji Pepe ambaye amekuwa akiwanyima nafasi viungo wa Barcelona kukaaa na mpira kama walivyozoea.
Baada ya kiungo mkabaji Sami Khedira kuumia inamaanisha leo Lassana Diarra ataanza na Mourinho anatarajiwa atacheza kama alivyocheza fainali ya kombe la mfalme na bila kutumia washambuliaji wanaocheza namba tisa tunaowafahamu ndani ya Madrid.
Katika ulinzi Real Madrid itamkosa Ricardo Carvalho, lakini Madrid haina tatizo katika ulinzi kama ilivyo kwa Barcelona ambayo itawakosa Eric Abidal, Adriano Correia na Maxwell ingawa hivi sasa Carles Puyol amerudi na anaweza kucheza beki wa upande wa kushoto na Javier Mascherano akacheza nafasi ya mlinzi wa kati.
Kama Barcelona itabadili leo mfumo wake wa 4-3-3 itamaanisha Real wamefanya kazi nzuri ya kuwashughulikia nyota watatu wa Guardiola ambao ni Xavi, Andres Iniesta na Lionel Messi.