40 wahitimu mafunzo ya ukocha
Monday, 27 December 2010 09:22
Sweetbert Lukonge
ZAIDI ya makocha 40 mkoani Mwanza, wamehitimu mafunzo yao ya siku tatu ya mbinu za ukocha yaliyoendeshwa na kocha msadizi wa timu ya Taifa (Taifa Stars) Sylivester Marsh.
Akizungumza na Mwananchi jana Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoani Mwanza (MZFA) Jackson Songora alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kwa namna moja ama nyingine kuinua soka katika mkoa huo.
ìHatua hii ni changamoto kubwa kwa makocha wote waliofanikiwa kujifunza mengi kutoka kwa mtaalamu huyo, tunawaomba wajaribu kuhakikisha wanayafanyia kazi ili lengo letu liweze kutimia.
ìHaitapaendeza kuona kocha yeyote aliyebahatika kupata mbinu mpya za kiufundi ikiwa ni pamoja na kujifunza mifumo mbalimbali ya soka anaishia kuwa kocha wa semina tu bila ya kutumia ujuzi huo kuinua soka na kuibua vipaji mbalimbali vilivyojificha kwa faida ya soka letu,î alisema Songora.
Alisema kila kocha aliyepata mbinu hizo anatakiwa kujituma na kuwajibika ipasavyo zaidi katika soka la vijana kwa kutumia mbinu hizo ili kurudisha hadhi ya mkoa huo kuwa chimbuko la vipaji nchini.
Alisema Chama hicho kitakuwa kikiandaa timu mbalimbali za vijana ambazo makocha wote waliobahatika kupata mbinu hizo za kiufundi watakuwa wakizifundisha kwa kupokezana ili wasiishie kuwa makocha wa vyeti bila ya vitendo.