Machibya ataka bajeti ya michezo
Imeandikwa na John Nditi, Morogoro; Tarehe: 23rd December 2010 @ 23:35
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Issa Machibya amezitaka halmashauri za wilaya za mkoa huo katika mwaka ujao wa fedha kutenga bajeti itakayogharamia uendeshaji wa michezo ya aina mbalimbali kwa ngazi za Wilaya na Mkoa katika timu za shule za msingi na sekondari ili kujenga hamasa ya wachezaji kwenye mashindano katika kutetea ushindi wa kimkoa na kitaifa.
Agizo la Machibya limekuja baada ya kufahamishwa kuwa katika suala la michezo halijatengenezewa bajeti na halmashauri za wilaya wala mkoa, hali inayochangia timu zinazowakilisha mkoa ama wilaya kwenye mashindano mbalimbali kushindwa kufanya vyema.
Aliyasema hayo jana baada ya kukabidhiwa vikombe vya ushindi wa kwanza wa timu ya Netiboli ya Mkoa wa Morogoro ya shule za msingi na ushindi wa pili wa mchezo wa mpira wa miguu baada ya kuvitwaa wakati wa mashindano ya Umoja wa Michezo , Taaluma ya Shule za Msingi Tanzania ( UMITASHUMTA) yaliyomalizika hivi karibuni Mjini Kibaha, Pwani.
Awali, kabla ya kutoa agizo hilo Machibya aliwapongeza wachezaji wa timu zote zilizoshiriki soka, netiboli na riadha pamoja na watendaji waliofuatana na timu hiyo sambamba na walimu wao ambao kwa namna moja katika ushirikiano wao wamefanikiwa kuuletea heshima kubwa Mkoa wa Morogoro kupitia mashindano hayo ya UMITASHUMTA.
Kutokana na mafanikio hayo walioonesha vijana hao, Mkuu wa Mkoa alitumia fursa hiyo kumwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro , Mgeni Baruani , kutoa maelekezo kwa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya zote katika mkoa huo kwenye kipindi cha bajeti zao za mwaka ujao kutenga fedha kwa ajili ya shughuli za kuendeleza michezo shuleni.
"Leo (jana) nimejawa na furaha tele…kutoka kwa vijana hawa, wameuletea heshima mkoa wetu katika michezo, ubingwa wa netiboli wa mashindano haya kitaifa ni chachu ya kuendeleza michezo mkoani mwetu…pia ushindi wa pili wa soka ni kielelezo tosha kuwa michezo shuleni ikitengewa fedha itakuwa ni endelevu na mafanikio makubwa," alisema.
Naye Ofisa Elimu wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Kilimia, ambaye alikuwa ni Mkuu wa Msafara wa Timu ya Mkoa alisema kuwa jumla ya wachezaji 60 wakiwemo wavulana 37 na wasichana 23 walishiriki michezo hiyo.
"Vijana wetu wamefanya kazi nzuri sana na kupata ushindi wa kwanza katika netiboli na wa pili kwenye soka pia mkoa umetoa mchezaji bora wa mpira wa miguu na kijana wetu mmoja kupata medali ya dhahabu kwenye mbio za mita 100…haya ni mafanikio makubwa," alisema Kilimia.
Alisema ushindi huo ulitokana na mshikamano na ushirikiano uliokuwapo baina ya viongozi na vijana wao, nidhamu na moyo wa kujituma kwa vijana hao na kuwashukuru wadau waliochangia kuiwezesha timu hiyo kushiriki mashindano hayo ya kwanza tangu Serikali kurudisha michezo shuleni.
Katika mashindano hayo , Timu ya Netiboli ya Mkoa wa Morogoro, iliifunga Mbeya mabao 24 -16 na kwa upande wa soka Morogoro ilishika nafasi ya pili baada ya kufungwa na Mbeya mabao 4-1.
Mashindano hayo ya Umitashumta , ambayo ni ya kwanza tangu kusitishwa mwaka 2000 , yalishirikisha mikoa kumi ya Tanzania Bara ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Iringa, Dodoma, Singida, Mbeya na Morogoro , ambapo pia Mkoa wa Tabora ulipeleka wanafunzi wenye ulemavu na Mkoa wa Dar es Salaam, baadhi ya washiriki wake walikuwa ni wenye ulemavu pia.