Mabao yaadimika Kombe la Mfalme Hispania
Wednesday, 22 December 2010 19:29
MADRID, Hispania
SARE zimetawala mechi za Kombe la Mfalme wa Hispania zilizochezwa juzi, ikiwamo ile baina ya Barcelona dhidi ya Athletic Bilbao.
Katika mchezo huo wa kwanza wa hatua ya 16 bora, pia Valencia na Villarreal zilimaliza mchezo kwa suluhu 0-0.
Beki wa Barcelona, Dani Alves alikuwa kivutio katika mchezo huo baada ya kumdhibiti mshambuliaji wa Athletic Bilbao, Iker Muniain.
Mechi tatu za michuano hiyo zilichezwa Jumanne, mbili zikimalizika kwa suluhu 0-0, isipokuwa ile baina ya Cordoba na Deportivo La Coruna, mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya 1-1.
Katika mchezo baina ya Barca na Bilbao kwenye Uwanja wa Nou Camp , timu hizo zina rekodi safi kwenye michuano hiyo.
Barca imetwaa taji hilo mara 25 dhidi ya Bilbao ambayo imelitwaa mara 23 na ulikumbusha fainali ya mwaka 2009 ambako Barca ilishinda 4-1.
Kabla ya mchezo huo, Barca ilikuwa na wastani wa mabao manne katika kila mchezo ambao imekuwa ikicheza katika siku za karibuni.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Hispania, pia wameshinda mechi 10, lakini juzi walishindwa kupenya ukuta wa wapinzani wao licha ya kuwachezesha nyota wake, Xavi, Andres Iniesta na Pedro Rodriguez kaitka kikosi kilichoanza.
Barca iliwaingiza washambuliaji hatari, David Villa na Lionel Messi kipindi cha pili.
Vijana wa kocha Pep Guardiola walitawala mchezo huo, lakini Bojan Krkic na Iniesta walikosa nafasi za kupachika mabao baada ya ushujaa wa kipa wa Bilbao Gorka Iraizoz katika kipindi cha kwanza.
Beki Gerard Pique alipata nafasi nzuri karibu na mwisho wa mchezo kabla ya ule wa marudiano kwenye Uwanja wa San Mames baada ya Messi kumpigia pasi murua ambayo alishindwa kuitumia akiwa ndani ya lango la wapinzani wao.
Badala ya kutulia, beki huyo wa kimataifa wa Hispania aliupiga nje kwa mguu wake wa kushoto na kuwaacha Bilbao wakijipongeza kwa kazi nzuri.
Kwenye Uwanja wa Mestalla, wenyeji Valencia watajilaumu kwa kushinda kutumia nafasi walizopata kuimaliza Villarreal.
Kikosi hicho cha kocha Unai Emery waliwazidi kwa kila hali Villarreal, maarufu Yellow Submarine kwa sehemu kubwa ya mchezo huo, lakini Aritz Aduriz, Pablo Hernandez, Juan Manuel Mata, ambaye aligonga mwamba na Ricardo Costa walishindwa kufunga mabao.
Villarreal, ambao wana pointi tano mbele ya Valencia wakiwa katika nafasi ya nne ya Ligi Kuu (La Liga) walipata nafasi chache mno katika mchezo huo, ikiwamo ile iliyopotezwa na Nilmar, ambaye alizuiwa na kipa Vicente Guaita .
Katika mchezo mwingine wa juzi, Cordoba , mojawapo ya timu mbili ambazo hazichezi ligi kuu pamoja na Real Betis ilicheza kishujaa na kupata sare ya 1-1 dhidi ya Deportivo La Coruna katika mchezo ambao uliathiriwa na hali mbaya ya hewa.
Depor walipata bao la kuongoza dakika ya 17 kwa penalti baada ya Riki, kuangushwa na kipa wa Cordoba, Alberto Garcia, kumtungua mbaya wake.
Hata hivyo, Cordoba walisawazisha bao dakika ya 70 baada ya kipa wa Depor, Manu kufanya kosa la mwaka alipojaribu kupangua kwa mkono mpira wa Jonathan Sesma wa adhabu ndogo , akampa nafasi Pepe Diaz kuujaza wavuni.
Mechi zaidi za michuano hiyo zilitarajiwa kucheza jana usiku na zile za marudiano zitakuwa wiki ya kwanza ya Januari.