Yanga cha mtoto kwa Azam
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 19th December 2010 @ 07:58
YANGA jana ililala kwa mabao 3-1 dhidi ya Azam katika mechi ya kirafiki na kutambulisha wachezaji wake wapya iliyofanyika kwenye Uwanja wa Uahuru Dar es Salaam.
Mshambuliaji wa Azam, John Bocco ‘Adebayor' ndiye aliyeanza kuzifumania nyavu za Yanga katika dakika 22 baada ya kumpiga chenga kipa wa Yanga, Ivan Knezevic kabla ya kuujaza mpira wavuni kirahisi.
Ni katika kipindi hicho cha kwanza, Yanga ikiyokuwa ikicheza bila Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Jerryson Tegete, Abdi Kassim ‘Babi' na kipa Yaw Berko, ilionekana kuelemewa hasa sehemu ya kiungo huku wachezaji wake wakiwa ‘hawaelewani' na kipa.
Patrick Mafisango aliipatia Azam bao la pili katika dakika ya 37 baada ya kupokea pasi ya Bocco kabla ya kuwachambua mabeki wanne wa Yanga na kufunga huku kipa akiwa ameshapotea golini.
Bocco aliifungia Azama bao la tatu zikiwa zimesalia sekunde chache kabla ya mapumziko, alifunga bao hilo baada ya kuwazidi maarifa mabeki wa Yanga kabla ya kuujaza mpira wavuni.
Kipindi cha pili, kilianza kwa kasi baada ya Yanga kubadilisha timu nzima kutokana na kipindi cha kwanza kuwachezesha wachezaji wengi wa timu B na ambao hawachezi mechi za mashindano na hapo ndipo Berko, Nsajigwa, Mwasika, Nadir Haroub, Isaac Boakye, Ernest Boakye, Babi, Omega Seme, Tegete na wachezaji wapya Juma Seif na Davis Mwape walionekana umuhimu wao.
Bao la kufutia machozi la Yanga lilifungwa na Mwape katika dakika ya 84 baada ya kupenyezeana pasi na Tegete ndani ya 18.
Kwa ujumla mechi ya jana timu zilikuwa zikishambuliana kwa zamu ambapo Azam ilifika langoni mwa Yanga mara kwa mara katika kipindi cha kwanza, huku Yanga ikifanya hivyo katika kipindi cha pili.
Timu hizo zinajiandaa na mzunguko wa pili wa ligi unaotarajiwa kuanza Januari 15, katika msimamo wa mwisho kabla ligi haijasimama Yanga iko nafasi ya pili ikiwa na pointi 25 na Azam ni ya tatu ikiwa na pointi 20, nafasi ya kwanza inashikiliwa na Simba yenye pointi 27.