Sneijder kuikosa TP Mazembe fainali leo
Saturday, 18 December 2010 09:20
ABU DHABI, Falme za Kiarabu
INTER Milan ya Italia inakutana na TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwenye fainali za dunia za klabu bingwa leo bila kuwa naye kiungo wao, Wesley Sneijder ambaye ni majeruhi.
Inter, mabingwa wa Ulaya walifuzu kucheza fainali kwa ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Seongnam Ilhwa ya Korea Kusini mjini Abu Dhabi.
Hata hivyo, ushindi huo uliitokea puani timu hiyo baada ya kumpoteza kiungo huyo Mdachi, ambaye ana ndoto ya kushinda taji lake la tano mwaka 2010.
Sneijder, ambaye aliachwa kwenye orodha ya wachezaji waoanwania tuzo ya mchezaji bora duniani aliumia paja na alitolewa katika mchezo dhidi ya Ilhwa, Jumatano usiku.
Dejan Stankovic, Javier Zanetti na Diego Milito , walifunga bao dhidi ya mabingwa hao wa Asia na kumpa faraja kocha Rafa Benitez na kumsahaulisha machungu ya kumkosa Sneijder.
"Haikuwa rahisi mwanzoni , tulikuwa na wakati mgumu, sasa ni vigumu kumkosa Sneijder . Tunatakiwa kucheza bila kuwa naye ," alieleza Benitez.
"Ninadhani aliumia msuli, sina hakika kama ataweza kucheza fainali Jumamosi."
Wakati huohuo, Rais wa Inter, Massimo Moratti amemuunga mkono Benitez ambaye amekuwa akikabiliwa na wakati mgumu klabuni hapo.
Aliuambia mtandao wa Mediaset: "Yeye (Benitez) alijiandaa vizuri kwa mchezo huo . Nimefurahishwa na umakini wa wachezaji wake."