Viingilio mechi ya Stars, Palestina vyatajwa
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 7th February 2011 @ 21:00
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetangaza viingilio vya mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Taifa Stars na Palestina itakayochezwa Jumatano kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF Boniface Wambura alisema, viingilio vilivyopangwa vimezingatia uwezo wa Watanzania walio wengi kwani wanataka kila mmoja aingie uwanjani.
Alisema katika mechi hiyo watakaokaa VIP A ni sh 10,000, VIP B Sh 7,000 na VIP C Sh 5,000. Kwa upande wa viti vya machungwa ni Sh 3,000, viti vya bluu ni Sh 2,000 na Sh 1,000 kwa watakaokaa jukwaa la kijani.
Tayari Palestina imeshawasili nchini tangu juzi kwa ajili ya mechi hiyo na Wambura alisema tiketi zitaanza kuuzwa leo.
"Waamuzi katika mechi hiyo ni Oden Mbaga atakayekuwa mwamuzi wa kati, akisaidiwa na Hamisi Maswa wa Zanzibar na Hamisi Chang'walu, mwamuzi wa akiba ni Ramadhani Ibada na Kamisaa ni Khamisi Kisiwa," alisema Wambura.
Hiyo itakuwa mechi ya kwanza ya kirafiki ya kimataifa kwa Stars tangu itoke Misri iliposhiriki michuano ya Bonde la Mto Nile na kushika nafasi ya sita, kati ya timu saba.
Katika hatua nyingine, Wambura alisema kutakuwa na mapitio ya Azimio la Bagamoyo lililotokana na semina ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa klabu za Ligi Kuu Desemba 2007 yatakayofanyika Februari 14 mpaka 18.
Alisema washiriki katika mapitio hayo ni wenyeviti, makatibu wakuu na maofisa habari wa klabu za Ligi Kuu.
Wakati huo huo, Wambura alisema Semina ya mawakala wa Fifa inatarajiwa kufanyika katika ofisi za TFF Machi 31 mwaka huu, na kwamba wanaotaka wawasiliane na Shirikisho hilo.