Cameroon , Ivory Coast zaanza vyema CHAN 2011
Monday, 07 February 2011 20:44
KHARTOUM, Sudan
CAMEROON na Ivory Coast zimeanza vyema michuano ya mwaka huu ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN), mechi zilizochezwa mwisho wa wiki.
Cameroon, maarufu kama The Indomitable Lions waliwalaza watetezi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa mabao 2-0.
Nao Ivory Coast, The Elephants, wenyeji wa fainali za mwaka 2009 waliilaza Mali 1-0 , mchezo wa Kundi C kwenye Uwanja wa Al Merrikh mjini Omdurman.
Bao moja la kila kipindi kupitia kwao, Joseph Mamosso na Ousmaila Baba yalitosha kuipa ushindi Indomitable Lions dhidi ya DR Congo ambayo ilionekana timu ya kawaida.
Chipukizi Kone Zoumana aliipa bao Ivory Coast katika mchezo mwingine wa michuano hiyo dhidi ya Mali.
DRC waliwatumia wachezaji saba kutoka klabu bingwa ya Afrika, TP Mazembe,, ambao ni kipa Muteba Kidiaba, nahodha Mihayo Kazembe, Kabangu Mulota, Bedi Mbenza, Joel Kimwaki, Kasusula Kiritsho na Alain Kaluyituka Dioko.
Cameroon ambao wanashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza walianza vibaya kabla ya kujirekebisha licha ya kumpoteza mshambuliaji Valentine Atem aliyeumia dakika 10 za kwanza na nafasi yake kuchukuliwa na Monkam Arnaud.
Hata hivyo, kuondoka kwa Atem, ambaye amerejea kwao baada ya kucheza soka Ulaya hakukuiathiri Cameroon na kuwakabili The Leopards wa DRC ambao walionekana kukosa mbinu za kuwakabili wapinzai wao.
Walikosa nafasi ya kupachika bao la penalti baada ya Abouna Patrick kukosa mkwaju huo dakika ya 30 ya mchezo huo.
Sehemu ya kiungo ya DRC ikiwa chini ya Nkanu Mbiyavanga, Salakiaku Matondona Mbenza ilionekana kupwaya kwa kiasi kikubwa huku Kaluyituka akizuiwa na mabeki wa Cameroon.
Kipa Kidiaba aliwazuia Cameroon dakika ya 36 ya mchezo kwa kuzuia mkwaju wa Joel Babanda. Dakika ya 41, Joseph Momasso alipachika bao la kwanza kwa juhudi zake boinafsi kisha kumchambua kipa Kidiaba.
Kipindi cha pili, DRC walibadili mchezo na kupiga pasi ndefu kuwadhibiti Cameroon na kushambulia kwa kushtukiza.
Mchezaji aliyeingia kipindi cha pili, Kasongo Ngandu alikaribia kuziona nyavu, lakini mpira wake uligonga mwamba na kurejea uwanjani baada ya pasi murua ya Kasusula.
Baba aliiipa bao la pili Cameroon dakika ya 78 baada ya kutoelewana kwa kwa beki Gladys Bokese na Kidiaba.
Bokese alimrejeshea pasi ya nyuma kipa wake Kidiaba ambaye alikuwa ametoka langoni kwa kasi, akimwacha Baba akimalizia mpira wavu uliokuwa wazi.
Baadaye, Kone aliifungia Ivory Coast kwa kichwa dakika ya 21 kutokana na krosi ya Kouame Konan.
Mali, ambao pia wanashiriki kwa mara ya kwanza walionekana kukosa mbinu mbele ya lango la wapinzani wao na kushinda kutumia nafasi walizozipata.
Kwa matokeo hayo, Kundi C limeipa uongozi Cameroon na kufuatiwa na Ivory Coast huku DRC na Mali zikiwa hazina pointi.
Afrika Kusini na Niger, pia zilianza vyema michuano hiyo kwa ushindi Jumamosi. Afrika Kusini iliilaza Ghana iliyokuwa ya pili mwaka 2009 kwa bao 1-0. Niger, ambayo pia ni mshiriki kwa mara ya kwanza iliilaza Zimbabwe 1-0.