Casillas aanza kuota ubingwa
Friday, 04 February 2011 20:47
MADRID, Hispania
KIPA wa Real Madrid, Iker Casillas ana matumaini ya kutwaa Kombe la Mfalme mwaka huu kwa kuwafunga mahasimu wao Barcelona katika fainali itayopigwa mwezi Aprili 20.
Casillas atakuwa akicheza fainali yake ya tatu ya kombe hilo huku akiwa ameambulia patupu mara mbili, nyota huyo wa Hispania sasa natafuta kujaribu bahati yake kwa mara nyingine.
"Tumefurahi sana kwa sababu tutakuwa tukicheza moja ya mechi muhimu zaidi mwaka huu," alisema Casillas na kuongeza kuwa "hii ni moja ya kutimiza malengo yetu tuliyojiwekea msimu huu na tumefanikiwa kutimiza.
"Sasa tunaangalia kama tutakuwa na bahati ya kutosha kutwaa taji hilo. Ni faraja kufika fainali. Nimekosa ubingwa mara mbili kwenye fainali na hii ni mara ya tatu naamini bahati itakuwa kwangu."
Nyota huyo mwenye miaka 29, alizungumza hivyo baada ya kuishinda Sevilla 2-0 na kwenye mchezo wa marudiano uliofanyika kwenye Uwanja wa Bernabeu katikati ya wiki.
"Haikuwa mechi rahisi. Tulicheza mechi nyingi mwezi uliopita na wote tulikuwa kwenye hali ngumu.
"Pamoja na mazingira hayo tumeweza kucheza fainali. Tulikuwa na matatizo latika kipindi cha kwanza, lakini Sevilla walibadilika na kutoa nafasi kwetu ya kupata matokeo hayo mazuri.
"Sasa bado tunamechi tatu kabla ya Ligi ya Mabingwa, hivyo kuna vitu tunatakiwa kubadilika kidogo," aliongeza Casillas.
"Hatuwazi kitu kingine chochote zaidi ya mchezo wetu ujao. Katika La Liga hatupo kwenye nafasi nzuri, lakini ushindi huu umetuweka kwenye mazingira mazuri zaidi kwa mechi ijayo."