Kocha Hall atua rasmi Azam Wednesday, 15 December 2010 21:24
Clara Alphonce na Doris Maliyaga
BAADA ya mchakato wa miezi mitatu ya kutafuta kocha hatimaye Azam jana wamesaini mkataba na kocha wa timu ya taifa ya Zanzibar, Stewart Hall raia wa Uingereza amepewa baraka zote na waajiri wake, Chama cha Soka Zanzibar.
Kocha huyo amewabwaga makocha wengine maarufu, Stephen Keshi, raia wa Nigeria na Michael David kutoka Ujerumani.
Hall ameingia mkataba wa kuinoa timu hiyo kwa mwaka mmoja na nusu ambao umeanza rasmi jana.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Mohamed Said alisema kuwa kocha huyo amepatikana kutokana na ushirikiano na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na kocha mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen.
''Tulipokuwa tunaanza mchakato huo hatukutaka kukurupuka tulitafuta ushauri TFF, watuambie jinsi walivyopata kocha wa taifa na walitupa ushirikiano pia tuliomba ushauri kwa Poulsen na kazi hiyo ilifanywa na kamati yetu tulioichagua ambayoimeongozwa na katibu wetu,'' alisema.
Alisema awali walipata maombi ya makocha 25 kutoka nje ya nchi na ndani, lakini kamati yao ilichagua majina saba yenye sifa na vigezo vinavyotakiwa na kuyapeleka kwenye bodi yao ambayo iliitaka kamati hiyo kupunguza majina na ndipo walipopata majina matatu.
Kwa upande wa Stewart alisema kuwa amefurahi kufundisha timu hiyo ya Azam kwani toka awali alikuwa anapenda kufundisha klabu kuliko timu ya taifa ili aweze kutafuta wachezaji kutoka chini.
Alisema atahakikisha timu hiyo inazidi kwenda mbele na malengo yake ni kuhakikisha wanacheza klabu bingwa Afrika mwakani ingawa anajua kutakuwa na ushindani mkubwa kutoka kwa timu kubwa kama Simba na Yanga.
Kuhusu mkataba wake na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) alisema kuwa ameukatisha, lakini bado ataendelea kuwasaidia kwa miezi mitatu mpaka hapo watakapopata kocha mwingine kwa kuwa kwa sasa hawana mashindano yoyote.
Alisema kuwa jana alianza kazi rasmi na timu yake mpya, lakini bado wachezaji wake wa kigeni hawajaripoti ingawa wanatarajia kuripoti kesho na keshokutwa watakuwa na mechi ya kirafiki dhidi ya Yanga kwenye uwanja wa Uhuru.
Wakati huohuo, wadhamini wakuu wa Zanzibar Heroes, Kampuni ya Future Century Limited wameeleza kuwa mkataba wao na kocha huyo unamruhusu kuifundisha timu hiyo kwa makubaliano maalumu.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Helen Masanja ameliambia Mwananchi kuwa kampuni hiyo imefanya makubaliano baina ya kocha na Azam kuwa ataifundisha timu hiyo kwa kipindi ambacho Zanzibar hawana mashindano yoyote.
Kocha ataifundisha Azam kwa makubaliano maalumu na hii itakuwa kipindi ambacho ZFA haina michuano yoyote.alisema Masanja aliyedai wao wana mkata wa miaka mitano.
Suala hilo tumeliangalia kwa undani tukagundua kuwa kwa sababu ZFA ina michuano mmoja tu wa Cecafa kocha huyo hawezi kukaa hivi hivi ndiyo tukazungumza na kufikia mwafaka,alieleza Masanja.
Masanja aliongeza kuwa kwakuwa klabu hiyo ni wadau wazuri w kuendeleza vipaji ndiyo wakakubaliana hivyo.