Simba, Yanga zimechoka!
Imeandikwa na Amiri Mhando; Tarehe: 30th January 2011 @ 08:34
WAWAKILISHI wa Tanzania Bara kwenye michuano ya kimataifa, Simba na Yanga leo wameshindwa kuanza vyema kwenye michuano hiyo baada ya kutoka sare kwenye mechi zao.
Yanga ikicheza nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam katika michuano ya Kombe la Shirikisho, ilitoka sare ya mabao 4-5 na Dedebit ya Ethiopia na ilibidi isubiri hadi dakika za majeruhi kushangilia bao la kusawazisha lililofungwa kwa shuti la mbali na kiungo Godfrey Bonny, ikiwa ni dakika mbili baada ya mwamuzi wa mezani Isreal Nkongo kuonesha kibao kwamba dakika zilizosalia mpira kumalizika zilikuwa tatu.
Ilikuwa furaha kwa mashabiki wa Yanga, ambao hadi dakika ya 86 walikuwa wamefungwa mabao 4-2, huku timu ikiwa haioneshi mipango ya kusawazisha na kufanya baadhi ya mashabiki kuanza kuondoka uwanjani hapo kwa hasira.
Lakini dakika ya 86 mpira uliopigwa na beki Shadrack Nsajigwa na kuonekana kama hauna madhara ulimtoka kipa Biryam Habitam na kumkuta Jerry Tegete aliyeukwamisha wavuni kirahisi.
Mashabiki wa Yanga ambao awali waliingia uwanjani wakiwa na matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi wa kishindo kujijengea mazingira mazuri ya kusonga mbele katika mchezo wa marudiano walijikuta wakilazimika kushangilia sare kutokana na namna timu yao ilivyokuwa ikichezewa kana kwamba ilikuwa ipo uwanja wa ugenini.
Wengi hawakuamini kama Waethiopia wangeweza kung'ara Dar es Salaam, bali walikuwa wakionekana ni timu ya kufungwa mabao mengi, lakini kadri muda ulivyokuwa ukienda ndivyo Yanga walivyopoteana na kuwapa nafasi Waethiopia kutawala mchezo na kuzima mbwembwe za Yanga inayoongoza Ligi Kuu Tanzanai Bara.
Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 16 mfungaji akiwa Nadir Haroub baada ya mpira wa adhabu uliopigwa na Omega Seme kupanguliwa na kipa wa Dedebit na mpira kumkuta Haroub.
Waethiopia walisawazisha dakika ya 24 kutokana na beki Issac Boakye kutoa pasi fupi iliyonaswa na Damit Tikadu aliyepachika wavuni na dakika ya 35 Yanga ikafungwa bao lingine, lililopachikwa wavuni na Birham Bogale.
Alifunga bao hilo ikiwa ni dakika chache baada ya kipa Yaw Berko wa Yanga kutolewa kutokana na kuumia na kisha kuingia Nelson Kimathi aliyekumbana na dhahama hiyo.
Timu ziliendelea kushambuliana kwa zamu, lakini umaliziaji haukuwa mzuri kwa pande zote, ambapo Davies Mwape wa Yanga, Tegete na Idd Mbaga nao walipata nafasi kadhaa za kufunga lakini umaliziaji ulikuwa butu.
Dakika ya 43 Dedebit ilipata bao la tatu mfungaji akiwa Tikabu kwa shuti la mbali na kuwanyima raha mashabiki wa Yanga waliokuwa wakiibeza timu hiyo ya Ethiopia kiasi cha kupigia hesabu kwamba kama itashinda kizingiti cha Dedebit itakutana na Haras El Hodoud ya Misri.
Nurdin Bakari aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 44 angalau kupunguza presha kwa mashabiki kwamba wakati wowote mambo yangekuwa mazuri.
Kipindi cha pili pia ilikuwa cha kushambuliana kila upande na dakika ya 63 Tadelle Bengesha aliifungia Dedebit bao la nne baada Waethiopia hao kugongeana vizuri na kuingia ndani ya eneo la hatari na kuanzia hapo Yanga walikuwa na kazi kubwa ya kuutafuta mpira.
Dedebit itabidi ijilaumu kwa kutoshinda mchezo huo hasa baada ya kuwa mbele kwa mabao 4-2, ambapo washambuliaji wake walikosa mabao mengi ya kufunga.
Lakini pia kipa Kimathi wa Yanga naye jana alifanya kazi ya ziada licha ya kufungwa mabao matatu, lakini aliokoa michomo ambayo ingeweza kuwa na madhara makubwa kwa timu yake.
Kocha wa Yanga, Fredy Minziro ambaye jana alikuwa kwenye benchi kutokana na Kocha Mkuu, Kostadin Papic kutokuwepo baada ya kutangaza kujiuzulu, alisema timu yake ilipoteana hasa baada ya kutanguliwa kufungwa, lakini anaamini mambo yatabadilika na kuwa hakuna lisilowezekana.
"Mkishafungwa mnachangikiwa hilo ndilo lililotukuta, lakini tunashukuru kwamba tumepata sare tutapambana kwao," alisema Minziro.
Kutokana na matokeo hayo,Yanga ili isonge mbele inahitaji ushindi wa aina yoyote ama sare ya kuanzia mabao 5-5, lakini sare ya mabao chini ya manne itakuwa imetolewa.
Yanga: Berko/Kimathi, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Haroub, Boakye/Job Ibrahim, Seme, Godfrey Bonny, Nurdin Bakari, Tegete, Davies Mwape na Idd Mbaga.
Wakati huohuo, habari zilizopatikana kutoka Moroni, Comoro jana ni kuwa Simba ya Dar es Salaam nayo ilibanwa mbavu na kutoka bila kufungana na Elan Club de Mitsoudje ya huko katika mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mashabiki wengi nchini wamekuwa wakizidharau timu za Comoro na walikuwa wakiipa Simba nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi ugenini na kisha zitakaporudiana jijini Dar es Salaam wiki mbili zijazo. Lakini kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka Comoro, Simba ilibanwa vilivyo kiasi wachezaji hawakuamini kama wapinzani wao wangecheza mchezo mkali.
Washambuliaji wa Simba wakiongozwa na Mussa Mgosi, Patrick Ochan na Gumbo nao walipata nafasi za kufunga ila umaliziaji ulikuwa butu.
Kutokana na matokeo hayo ili Simba isonge mbele italazimika kupata ushindi wa aina yoyote, wakati wapinzani wao watahitaji ushindi ama sare lakini yenye idadi ya mabao yoyote.
Simba ilianza: Ally Mustapha, Haruna Shamte, Juma Jabu, Juma Nyoso, Meshack Abel, Jerry Santo, Hillary Echesa, Rashid Gumbo, Mussa Mgosi, Emmanuel Okwi na Ochan.
Wakati huohuo, timu ya KMKM ya Zanzibar inayoshiriki katika michezo ya Kombe la Shirikisho, jana ilishindwa kuutumia vyema uwanja wa nyumbani baada ya kufungwa mabao 4-0 na DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar ulishuhudia vijana hao wa KMKM wakiwa katika wakati mgumu na kukubali kipigo hicho, hivyo ili isonge mbele itahitajika ishinde mabao 5-0 zitakaporudiana nchini DRC.